Simba, Yanga CAFCL kitapigwa Amaan Complex
Muktasari:
- Hatua hiyo imekuja wakati timu hizo nne za Tanzania zikijiandaa kuwakilisha nchi katika mashindano ya klabu Afrika msimu wa 2026/27, huku kukiwa na changamoto ya upatikanaji wa viwanja vinavyokidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hasa baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwa kwenye matengenezo ya muda mrefu na Uwanja wa Uhuru kutokidhi vigezo.
SIMBA nayo imeingia kwenye hesabu za kuutumia Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kama uwanja wake wa nyumbani katika mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiungana na watani wao Yanga pamoja na Azam FC ambao pia wamewasilisha maombi ya kutaka kucheza mechi zao za kimataifa kwenye uwanja huo.
Hatua hiyo imekuja wakati timu hizo nne za Tanzania zikijiandaa kuwakilisha nchi katika mashindano ya klabu Afrika msimu wa 2026/27, huku kukiwa na changamoto ya upatikanaji wa viwanja vinavyokidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hasa baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwa kwenye matengenezo ya muda mrefu na Uwanja wa Uhuru kutokidhi vigezo.
Akizungumza na Mwanaspoti, mmoja wa viongozi wa Uwanja wa New Amaan Complex alisema maombi ya klabu hizo yamepokelewa na uongozi wa uwanja, akibainisha kuwa si Yanga pekee iliyotaka kuutumia uwanja huo bali hata Simba wameomba na wao wamewakubalia.
“Si Yanga pekee iliyowasilisha maombi ya kutaka kutumia Amaan. Simba nayo imepeleka maombi, Azam pia wamefanya hivyo. Kwa hiyo, tuna maombi ya klabu zaidi ya moja zinazotaka kuutumia uwanja huu kwa mechi zao za nyumbani katika hatua ya makundi,” alisema kiongozi huyo.
Aliongeza: “Kimsingi, klabu hizi zinaangalia namna ya kupata uwanja ambao unaweza kutumika kwa mechi za mashindano ya CAF. Amaan ni miongoni mwa viwanja vinavyoangaliwa kwa sababu tayari kuna maboresho yaliyofanyika.”
Kiongozi huyo alisema Uwanja wa Uhuru hauwezi kutegemewa katika hali yake ya sasa kwa sababu una nyasi bandia na bado unahitaji maboresho mengine ili kufikia mahitaji ya mashindano hayo.
“Uwanja wa Uhuru bado una changamoto. Kwanza una nyasi bandia, lakini pia kuna maeneo mengine yanahitaji kufanyiwa maboresho. Hatuwezi kusema kwamba unaweza kutumika moja kwa moja bila kufanyiwa kazi zinazotakiwa,” alisema.
Kuhusu Amaan, alisema: “Hapa maboresho yaliyokuwa yakihitajika yalishafanyika na uwanja ulifanyiwa tathmini ya CAF. Kwa hiyo, tunaamini unaweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto inayozikabili klabu zetu.”
Hata hivyo, alisema uongozi wa uwanja umekuwa ukipokea na kupitia maombi ya klabu hizo, akibainisha kuwa Amaan umekuwa nje ya matumizi kwa takribani miezi miwili, hivyo kurejea kwa mechi za kimataifa kungeongeza matumizi yake.
“Uwanja umekaa karibu miezi miwili bila kutumika. Kama maombi haya yatakamilika na ratiba kupangwa vizuri, utakuwa umetumika tena katika mashindano makubwa. Sisi tunachofanya ni kuhakikisha taratibu zote za matumizi zinafuatwa,” alisema.
“Tunatambua umuhimu wa klabu hizi kucheza nyumbani. Maombi yao tumeyapokea na tunatarajia taratibu zitakapokamilika, uwanja utakuwa sehemu ya mipango ya kuziwezesha timu zetu kushiriki mashindano ya Afrika.”
SHERIA ZA CAF
Kwa mujibu wa Kanuni za Viwanja za CAF za mwaka 2022, mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho zinahitaji uwanja wenye hadhi ya Daraja la Tatu (Category 3).
Kanuni hizo zinaeleza kuwa uwanja lazima uwe umekaguliwa na kupitishwa na CAF kabla ya kutumika katika mashindano yake. Pia, uwanja unatakiwa kuwa na maeneo yanayokidhi mahitaji ya timu na waamuzi, vyumba vya kubadilishia nguo, vifaa vya huduma ya kwanza, taa za kutosha kwa mechi za usiku, maeneo ya waandishi wa habari, vyumba vya mikutano na miundombinu ya matangazo ya televisheni.
Kuhusu nyasi, kanuni hizo hazizuii moja kwa moja matumizi ya nyasi bandia. Hata hivyo, zinahitaji nyasi hizo ziwe na leseni na uthibitisho wa ubora kutoka FIFA. Hivyo, changamoto ya Uhuru haiishii kwenye aina ya nyasi pekee, bali pia ni kukidhi vigezo vingine vya Daraja la Tatu.
REKODI ZA KLABU NNE
Kwa upande wa rekodi, Simba ndiyo inaongoza kwa idadi ya kushiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika miongoni mwa klabu za Tanzania, ikiwa imefika mara saba, ikiwamo msimu huu. Yanga itakuwa inashiriki kwa mara ya tano, huku ikifikisha misimu minne mfululizo katika hatua hiyo. Yanga pia ilifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2024/25 na fainali ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2022/23.
Azam FC na Singida Black Stars nazo zinaingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya pili mfululizo. Azam ilifuzu baada ya kuiondoa ZED FC ya Misri kwa jumla ya mabao 2-1, huku Singida ikiitoa Tusker ya Kenya kwa jumla ya mabao 2-1.