Clara anavyorudisha pesa za Washington!
Muktasari:
- Ingawa mshambuliaji huyo wa Tanzania hajapata dakika nyingi za kucheza tangu aliposajiliwa Marekani, kila anapopewa nafasi amekuwa akionyesha kwa nini klabu hiyo iliamua kuwekeza fedha nyingi.
UAMUZI wa Washington Spirit kutumia fedha kumsajili Clara Luvanga kutoka Al Nassr ya Saudi Arabia unaanza kuonekana kuwa na maana kubwa ndani ya uwanja.
Ingawa mshambuliaji huyo wa Tanzania hajapata dakika nyingi za kucheza tangu aliposajiliwa Marekani, kila anapopewa nafasi amekuwa akionyesha kwa nini klabu hiyo iliamua kuwekeza fedha nyingi.
Clara alijiunga na Washington Spirit Septemba 2026 kwa mkataba wa miaka minne hadi mwisho wa msimu wa 2029.
Ingawa dau lake la usajili kutoka Al Nassr halikutangazwa lakini ripoti mbalimbali zinaeleza uhamisho huo ume gharimu Dola 2.3 milioni sawa na takribani Sh5.9 bilioni ukivunja rekodi ya usajili ghali duniani.
Kabla ya kuhamia Marekani, Clara alikuwa amejitengenezea jina kubwa Saudi Arabia, ambako alishinda mataji matatu mfululizo ya ligi akiwa na Al Nassr, huku msimu uliopita akimaliza akiwa mfungaji bora baada ya kufunga mabao 24 katika mechi 14.
TAKWIMU ZINAZOONYESHA THAMANI YAKE
Kwa mujibu wa takwimu, Clara alicheza mechi tano, akianza mbili na tatu akiingia akitokea benchi. Katika dakika 235 alizocheza, alifunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao. Hiyo ni wastani wa mchango mmoja wa bao kila baada ya dakika 78.
Bao lake la kwanza lilikuwa dhidi ya Houston Dash Oktoba 4, na aliifungia Washington bao la ushindi dakika ya 84 katika ushindi wa mabao 3-2. Hilo halikuwa bao la kawaida, kwani lilimfanya kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga katika historia ya Ligi ya NWSL. Zaidi ya historia hiyo, lilionyesha uwezo wake wa kuamua matokeo hata anapopewa nafasi kwa muda mfupi.
Oktoba 25, Clara alifunga tena dhidi ya Kansas City Current, ingawa Washington ilipoteza mchezo huo kwa mabao 2-1.
Novemba Mosi, alitoa pasi moja ya bao katika ushindi wa Washington wa mabao 2-0 dhidi ya Chicago Stars, akitoa asisti ya Trinity Rodman aliyefunga dakika ya 85.
PORTLAND
Kama kulikuwa na mtu aliyekuwa na mashaka juu ya kiasi cha fedha kilichotumika kumsajili Clara, basi mchezo wa robo fainali dhidi ya Portland Thorns Novemba 8 unaweza kuwa umeongeza imani yake.
Washington ilishinda mabao 4-1 na Clara alikuwa miongoni mwa wachezaji walioifanya siku hiyo kuwa ya kipekee. Alifunga bao dakika ya 34 baada ya kutumia makosa ya kipa Mackenzie Arnold, kabla ya kutengeneza pasi ya Rodman aliyefunga dakika ya 35 na 58.
Kwa maana nyingine, Clara alihusika moja kwa moja katika mabao matatu kati ya manne ya Washington. Aliifungia moja na kutoa pasi mbili za mabao, mchango ambao ulimfanya awe mmoja wa wachezaji wawili wa kwanza katika historia ya NWSL kufikisha mchango wa mabao matatu katika mchezo mmoja wa mtoano.
Jambo la kuzingatia zaidi ni Clara alicheza dakika 67 tu kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Ashley Hatch. Hivyo, ndani ya dakika hizo 67 aliweza kutoa mchango wa mabao matatu.
Ukijumlisha takwimu za ligi na robo fainali hiyo, Clara sasa ana mabao matatu na pasi tatu za mabao katika dakika 302 alizocheza, kwa hesabu inayojumuisha dakika 235 za ligi na dakika 67 za mchezo wa Portland. Hiyo ni michango sita ya mabao, wastani wa mchango mmoja kila baada ya dakika 50.3.
WASHINGTON INA SABABU YA KUTULIA
Washington ina sababu nyingine ya kutabasamu kutokana na namna Clara alivyoanza kuendana na mahitaji ya timu hiyo.
Takwimu za msimu huu zinaonyesha timu hiyo imefunga mabao 43 katika mechi 30 za ligi, ikilinganishwa na mabao 42 iliyofunga katika mechi 26 msimu uliopita. Kinachovutia zaidi ni mchango wa Clara katika safu hiyo ya ushambuliaji.
Katika muda mfupi aliocheza uwanjani, amekuwa akionyesha uwezo wa kufunga na kutengeneza mabao, jambo linaloongeza machaguo ya Washington katika eneo la ushambuliaji.
Pamoja na hilo, umri wake mdogo na mkataba unaomfunga klabuni hapo hadi 2029 vinaipa Washington nafasi ya kunufaika naye kwa misimu kadhaa, huku kiwango chake kikiendelea kukua.
Hivyo Clara anaweza kuifanya timu hiyo iwe na nguvu zaidi ya ushambuliaji na uwekezaji huo unaweza kuwa na faida ya muda mrefu.