Mtanzania akiri ugumu Hispania
Muktasari:
- Marco, ambaye awali alikuwa akicheza soka la vijana katika akademi ya Nastic Tarragona, amesema kuhamia kwenye soka la wakubwa kumemfundisha umuhimu wa uvumilivu na kupambana ili kupata nafasi, hasa kutokana na kukutana na wachezaji wenye uzoefu zaidi yake.
Kiungo mshambuliaji wa Tanzania, Eric Marco amesema licha ya kuanza vizuri maisha yake mapya katika soka la watu wazima nchini Hispania, bado anakabiliwa na ushindani mkubwa wa kuwania nafasi katika kikosi cha kwanza cha Tortosa Ebre FC, kinachoshiriki Ligi Daraja la Sita nchini humo maarufu Segunda Catalana.
Marco, ambaye awali alikuwa akicheza soka la vijana katika akademi ya Nastic Tarragona, amesema kuhamia kwenye soka la wakubwa kumemfundisha umuhimu wa uvumilivu na kupambana ili kupata nafasi, hasa kutokana na kukutana na wachezaji wenye uzoefu zaidi yake.
Mshambuliaji huyo tayari amecheza mechi nane za ligi hiyo, tatu akianza kikosi cha kwanza na tano akianzia benchi kwenye dakika 348, huku akiwa amefunga mabao mawili na kusababisha penalti mbili. Kabla ya kucheza Tortosa Ebre FC, Marco alikuwa sehemu ya akademi ya NÃ stic Tarragona ambako alifanya vizuri katika mashindano ya vijana, akicheza mechi 35 na kufunga mabao 30 katika ligi za vijana za Catalonia msimu uliopita.
Akizungumzia nafasi yake uwanjani, Marco amesema anaweza kucheza kama mshambuliaji wa kati au winga ya kushoto, nafasi ambazo anazitumia kuonyesha uwezo wake.
Anakiri kuwa kutoka kwenye ligi za vijana kwenda soka la watu wazima si jambo rahisi, hasa kwa mchezaji anayehitaji kujenga nafasi yake mbele ya wachezaji wenye uzoefu.
“Ukiangalia nimetoka kucheza level ya vijana kuja kupata nafasi ya kuanza ni ngumu kidogo, kwa sababu kuna watu wenye uzoefu. Napambana na lazima niwe mvumilivu. Nashukuru kocha na viongozi wanaona juhudi zangu,” amesema Marco.