Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo matano yatakayombeba Mtanzania Arsenal

MBONGO Pict

Muktasari:

Baum mwenye umri wa miaka 20 ametambulishwa Arsenal akitokea RB Leipzig ya Ujerumani baada ya kuonyesha kiwango kikubwa kwenye msimu mmoja tu aliocheza Ujerumani.

USAJILI wa kiungo Lisa Baum kwenda Arsenal inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake England haukuvutia tu baadhi ya mashabiki kwa sababu ni mchezaji mwenye asili ya Tanzania bali pia ni aina ya mchezaji anayekidhi mahitaji ya soka la kisasa.

Baum mwenye umri wa miaka 20 ametambulishwa Arsenal akitokea RB Leipzig ya Ujerumani baada ya kuonyesha kiwango kikubwa kwenye msimu mmoja tu aliocheza Ujerumani.

Kiungo huyo alizaliwa mwaka 2006 nchini Tanzania, akiwa na baba Mjerumani na mama Mtanzania. Alikulia akizungumza kiswahili kabla familia yake kuhamia Ujerumani alipokuwa na umri wa miaka minne.

Kumekuwa na sintofahamu kwanini nyota huyo ni Mtanzania lakini ukweli ni kwamba bado asili yake ni Tanzania kutoka kwa mama yake.

Lakini pia ana uwezo wa kuitumikia timu ya Taifa ya Tanzania, Twiga Stars kutokana na kwamba bado hajacheza timu ya Taifa ya wakubwa ya Ujerumani alizitumikia timu za vijana tu. Mwanaspoti imechambua mambo matano yanayombeba Baum Arsenal.

MBONG 01

UBORA WAKE

Ingawa baadhi wanamtambua nyota huyo anacheza nafasi ya winga, lakini ukweli ni kwamba Baum ana uwezo wa kucheza nafasi tofauti uwanjani.

Ana uwezo wa kucheza winga wa kushoto, winga wa kulia, kiungo mshambuliaji anayesogea nyuma ya mshambuliaji na hata kutumika kama mshambuliaji wa pembeni kwenye mfumo wa washambuliaji watatu.

Silaha yake kubwa ni namna anavyoisoma nafasi. Anapocheza kulia hupenda kuingia katikati kwa kutumia mguu wake wa kushoto wenye nguvu, hali inayompa nafasi ya kupiga mashuti au kutoa pasi za mwisho.

Akihamishiwa kushoto hubaki huru zaidi na kutumia kasi yake kuwapita mabeki kabla ya kutengeneza nafasi kwa wenzake.

Katika mfumo wa Arsenal unaopenda kubadilishana nafasi kila wakati, uwezo huo unampa kocha chaguo kubwa. Mara nyingi washambuliaji wa Arsenal hubadilishana nafasi wakati wa mchezo ili kuwavuruga mabeki wa wapinzani na Baum anaelewa vizuri aina hiyo ya mpira.

Mbali na kushambulia hushuka kusaidia kukaba, hupeleka presha kwa wapinzani na hukimbia kwa nguvu kurejesha umiliki wa mpira, na sifa hizo ndio zimeifanya Arsenal kuvutiwa naye.

MBONG 02

MALEZI YA SOKA

Kiungo huyo amekulia kwenye malezi ya soka kiufupi alianza kucheza tangu ngazi ya shule. Alianza kucheza katika MTV Ahrensbok kabla ya kuhamia TSV Pansdorf ambako alikuwa msichana pekee kwenye timu ya wavulana. Mazingira hayo yalimsaidia kujenga kujiamini, kasi ya kufanya maamuzi na uimara wa kimwili.

Baadaye alijiunga na Hamburger SV ambako alipitia mfumo mzima wa maendeleo ya vijana. Aliisaidia timu ya chini ya miaka 17, kutwaa ubingwa kabla ya kupandishwa kikosi cha wakubwa mwaka 2022.

Akiwa Hamburger alikuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo iliyopanda kutoka daraja la chini hadi Bundesliga ya Wanawake. Katika mechi 68 alifunga mabao 21, rekodi iliyoonyesha uwezo wake wa kubeba majukumu ya ushambuliaji.

Mwaka 2025 alisajiliwa na RB Leipzig ambako alipata uzoefu wa kucheza katika mazingira yenye ushindani mkubwa zaidi wa ligi ya Bundesliga.

Malezi hayo yanaifanya Arsenal kupata mchezaji ambaye tayari amezoea mifumo ya kisasa ya soka la Ujerumani, ligi inayotambulika kwa nidhamu ya kiufundi, presha kubwa na kasi ya mchezo.

MBONG 03

UMRI UNAMBEBA

Baum anaingia Arsenal akiwa na miaka 20, umri ambao unaonekana kuwa mtaji mkubwa kwake kama ataendelea kupambana na kuonyesha uwezo wake.

Soka la wanawake nchini England linatumia nguvu, kasi na mabadiliko ya kutoka ulinzi hadi kwenye mashambulizi. Ili kuhimili mfumo huo, klabu nyingi zimewekeza kwa wachezaji vijana wenye uwezo wa kukimbia kwa dakika zote 90 au zaidi.

Arsenal ni miongoni mwa timu zenye wachezaji wengi vijana ambao wamekuwa wakiwatumia kwenye mashindano mbalimbali hivyo kama Baum ataonyesha kiwango chake atakuwa mmoja wa nyota wa kutumainiwa.

Umri wake unampa muda wa kuendelea kujifunza, kuzoea mazingira ya soka la ushindani na msingi wa muda mrefu wa Arsenal.

MBONG 04

KASI

Moja ya silaha ambazo Arsenal imekuwa ikizitumia kwa mafanikio ni washambuliaji wanaoweza kuwashinda mabeki katika hali ya mmoja dhidi ya mmoja.

Baum ni miongoni mwa nyota wenye sifa hizo. Ana kasi, uwezo wa kubadili mwelekeo kwa haraka na kuondoka kwa hatua chache mbele ya beki anayemkaba. Hii humlazimisha mpinzani kuvunja mfumo wa ulinzi ili kumzuia, jambo linalofungua nafasi kwa washambuliaji wengine nyuma kushambulia.

Mbali na kukimbia na mpira, Baum hutumia mwili wake vizuri kulinda umiliki na ana uwezo wa kuvuta mabeki wawili kwa wakati mmoja kabla ya kutoa pasi sahihi.

Katika mechi ambazo wapinzani hujilinda, aina hii ya mchezaji mara nyingi ndiyo huamua matokeo kwa sababu anaweza kutengeneza nafasi ambayo haikuwepo.

MBONG 05

NJAA YA MAFANIKIO

Tofauti na nyota wengi wanaojiunga na Arsenal wakiwa tayari wamejizolea umaarufu mkubwa Ulaya, Baum bado ndio kwanza msimu wake wa pili anacheza ligi kuu.

Amefika Emirates akiwa na kiu ya kuonyesha kuwa anaweza kucheza katika moja ya klabu kubwa zaidi duniani. Hilo linaweza kuwa faida kubwa kwa Arsenal kwa sababu wachezaji wenye njaa ya mafanikio mara nyingi huongeza kiwango cha kujituma mazoezini na uwanjani.

Lisa Baum anakwenda kujiunga na moja ya klabu zenye historia kubwa zaidi katika soka la wanawake duniani. Arsenal W ndiyo klabu iliyofanikiwa zaidi nchini England ikiwa imetwaa mataji 15 ya ubingwa wa ligi, Kombe la FA mara 14, Kombe la Ligi mara saba, huku pia ikiwa klabu pekee ya England iliyoshinda Ligi ya Mabingwa Ulaya UEFA mara mbili, mwaka 2007 na 2025.

Mwaka 2026, Arsenal iliendelea kuandika historia kwa kutwaa pia Kombe la Dunia la Klabu Bingwa za Wanawake (FIFA Women's Champions Cup), jambo linaloonyesha kiwango cha ushindani na utamaduni wa mafanikio ambao Baum anakwenda kuukuta Emirate.


MSIKIE MWENYEWE

"Ligi hii ina ushindani mkubwa na Arsenal ni klabu kubwa. Nataka kushinda mataji na kuendelea kuimarisha kiwango changu, na nahisi Arsenal ndiyo sehemu sahihi ya kufanikisha malengo hayo," amesema Baum