Mpira wa Simba na Yanga na uungwana wa fedha-1
Muktasari:
- Tumekuwa tukizitaka timu tunazoshabikia au ambazo sisi ni wanachama zishinde au zisajili wachezaji wazuri au zifike mbali katika mashindano ya ukanda na ya Afrika lakini hatujiulizi haya: Klabu zinapata wapi pesa za usajili na uendeshaji? Klabu zinatumia kiasi gani mpaka ligi inakwisha?
NI Jumatatu iliyojaa mikiki na harakati katika Kituo cha Mabasi Ubungo (UBS) jijini Dar es Salaam. Nahaha kupenya kwenye msitu wa watu ili ninunue tiketi niliyotumwa na rafiki yangu anayesafiri kuelekea mkoani.
Si kazi rahisi, watu ni wengi, kila mpiga debe analazimisha ununue tiketi kwa wakala wake ingawa hajui safari yako inaishia wapi.
Ghafla naona umati wa watu ukiwa umewazunguka vijana wawili wenye miili iliyoshiba waliokuwa wamekamatana koo, mara Polisi aliyekuwa karibu akaingilia na kuhoji kulikoni, anaambiwa chanzo ni mechi ya watani wa jadi iliyochezwa siku mbili nyuma.
Kijana aliyevaa fulana ya udhurungi, shabiki wa Simba aliendelea kutokwa na maneno akisisitiza Yanga wamefunga watoto, hawajafunga tano na kwamba Haruna Niyonzima wanamchukua.
Upande wa pili kuna huyu kijana kavaa fulana ya kijani aliyovaa jezi ya Yanga. Anatokwa na povu akidai Simba wamefulia na Yanga ndiyo iliyomnunua Emmanuel Okwi na kumuegesha Tunisia. Hadi naondoka eneo la tukio malumbano yalikuwa yamevuta watu wengi.
Natoka hapo, naelekea Mwenge Sokoni. Nanunua gazeti na kama kawaida yangu naanzia kurasa za mwisho. Nagundua lugha ni ileile niliyoisikia Ubungo Terminal, hali inaendelea hivyo hadi sasa.
Vichwa vya habari vinanadi uhamisho wa Hamis Kiiza, Mrisho Ngassa, Shomari Kapombe, Juma Kaseja, Baba Ubaya, Haruna Niyonzima, Yaw Berko hata Abdallah Kibaden na Themi Felix.
Kwa vyombo vya habari, angalau vimekwenda hatua moja zaidi na kuandika tathmini ya ligi iliyokwisha hivi karibuni. Hata hivyo nasita kuziita tathmini kwani kwa kiasi kikubwa ilikuwa ni kukumbusha uhalisia (facts) wa yaliyotokea. Vilevile wamejaribu kuelezea nani kashindwa na nani na kwa nini.
Kuna mambo kadhaa au upande muhimu wa mpira ambao tuliowengi hatuuangalii sana.
Klabu zinapata wapi fedha?
Kama walivyokuwa wale vijana mashabiki wa Ubungo ndivyo tulivyo wengi miongoni mwa waandishi, viongozi wa klabu, wanachama na hata wadau wakuu ambao ni shirikisho na vyama shiriki.
Wakati mwingine hata wajumbe wa kamati za usajili na zile za fitina hawana majibu ya uhakika na uchumi wa klabu zao kwa maana ya vyanzo na matumizi. Tumekuwa tukizitaka timu tunazoshabikia au ambazo sisi ni wanachama zishinde au zisajili wachezaji wazuri au zifike mbali katika mashindano ya ukanda na ya Afrika lakini hatujiulizi haya: Klabu zinapata wapi pesa za usajili na uendeshaji? Klabu zinatumia kiasi gani mpaka ligi inakwisha?
Imepatikana faida au hasara kiasi gani? na kwa nini? Je klabu zinazoshuka zitasalimika vipi huko zilikodondokea? Klabu zinazopanda zina tofauti na zilizoshuka? Je uchumi wa ligi unapanda au unashuka kulingana na hali halisi ya kiuchumi?
Yako mengi ya kujiuliza lakini kwa upande mwingine haishangazi sana kwani wataalamu wanasema kwamba watu na taasisi zao ni matokeo ya utamaduni wao. Tunavyoendesha maisha yetu ndivyo tunavyoendesha klabu. Ligi imekwisha, ukiangalia juu kwenye msimamo kuna Yanga, Azam na Simba na chini kuna African Lyon, Toto African na Polisi Morogoro.
Msimamo wa ligi yetu kwa namna moja au nyingine unaonyesha hali ya uchumi wa klabu ulivyokuwa kwenye msimu huo wa ligi au katika hatua fulani ya ligi. Kama nilivyosema hapo juu, maisha yetu na taasisi zetu ni matokeo ya utamaduni wetu. Bahati mbaya kwetu ni kwamba mpira hautoi ruksa kwetu kuuendesha kwa mila na tamaduni zetu.
Mpira una mila desturi na utamaduni wake na Dunia nzima inapaswa kuufuata na mafanikio ya klabu na hata timu za taifa hupimwa dhidi ya utamaduni wa mpira kidunia, haijalishi una wachezaji na vipaji kiasi gani lakini kama mpira wako hauchezwi na kuongozwa kwa mujibu wa taratibu za ulimwengu basi utakuwa nyuma.
Ni bahati mbaya sana kwamba mabadiliko ya siasa na uchumi wa nchi yetu kwa kiasi kikubwa yameshindwa kubadilisha utamaduni wa mpira wakati mpira uliingia kwenye utandawazi mapema huku Dunia ya siasa na uchumi ikiwa kwenye vita baridi.
Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) lina kanuni inaitwa uungwana katika matumizi ya fedha ‘Financial Fair Play’ kanuni hii inamuwezesha yule mpiga debe wa Ubungo kujua pesa ya kumnunua Niyonzima, Kaseja,Twite na Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na wengineo inatoka wapi. Kanuni hii inamfanya mwananchi na mwanachama ajue mapato ya mchezo dhidi ya mtaji wake ni kiasi gani bila kusubiri kusikia TFF wameamua watutajie kiasi gani.
Kanuni inaweka mstari kati ya fedha za mwanachama na fedha za klabu na inazuia klabu kutumia kuliko wanavyopata.
Mpaka sasa klabu kama Real Madrid, Manchester City, PSG, Galatasaray na wengine wako kwenye hatari ya kuondolewa kwenye mashindano ya Europa na Ligi ya Mabingwa kwa sababu ya kutokuwa na nidhamu au uungwana katika matumizi yao ya fedha.
Nashawishika kusema kwamba utamaduni wetu ndio umemkosesha Azam ubingwa na ndio umemshusha African Lyon daraja. Nasisitiza, kama mazingira yangekuwa ya kinidhamu huenda tungekuwa na bingwa mwingine na aliyeshuka daraja mwingine.
Kama nilivyodokeza hapo nyuma, msimamo wa ligi kwa kiasi kikubwa unaonyesha hali ya kifedha ilivyokuwa kwa klabu zetu katika msimu uliopita au katika wakati fulani wa msimu uliopita.
Itaendelea Jumanne
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga.