Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Moto wa Ngorongoro Heroes CECAFA U-20

NGORONGORO Pict

Muktasari:

  • Timu hiyo imefuzu hatua ya nusu fainali baada ya kumaliza kileleni mwa kundi A ikikusanya pointi sita baada ya kuzitandika Rwanda mabao 3-0 na Ethiopia mabao 4-0.

TIMU ya Taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes imeendelea kuonyesha ubora mkubwa kwenye mashindano ya CECAFA U-20 yanayoendelea hapa nchini.

Timu hiyo imefuzu hatua ya nusu fainali baada ya kumaliza kileleni mwa kundi A ikikusanya pointi sita baada ya kuzitandika Rwanda mabao 3-0 na Ethiopia mabao 4-0.

Sasa Ngorongoro Heroes inakwenda kucheza nusu fainali dhidi ya Burundi na ikishinda, itajikatia tiketi ya kucheza fainali na kufuzu AFCON U-20. Mechi hiyo itachezwa kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuanzia saa 12:00 jioni na Burundi imemaliza kinara kundi C ikikusanya pointi sita ikizifunga Kenya 2-0 na Sudan Kusini 4-0. Mechi nyingine ya nusu fainali ni Uganda dhidi ya Sudan ambayo itachezwa mapema siku hiyo saa 8:00 mchana.

Kwa kiwango cha Ngorongoro Heroes, kuna wachezaji ambao wameonyesha uwezo mkubwa na kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya timu.

Baadhi yao wanatoka kwenye klabu kubwa za Ligi Kuu Bara Simba na Yanga, huku wengine wakitokea KMC, lakini kitu kinachowaunganisha ni kiwango walichokionyesha ndani ya mashindano hayo.

Ngorongoro imekuwa miongoni mwa timu zilizovutia kutokana na namna ilivyocheza, ikifunga mabao saba bila kuruhusu bao hadi sasa.

Hawa hapa ni baadhi ya mastaa ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye safari hiyo.


NGORO 02

BASHIRI KIBAILA – SIMBA

Kiungo huyo mshambuliaji anayekipiga timu za vijana za Simba, amekuwa akipata nafasi ya kucheza katika kikosi cha wakubwa mara kadhaa, jambo linalompa uzoefu wa kukabiliana na ushindani wa kiwango cha juu.

Katika ushindi wa mabao 4-0, Kibaila alifunga mabao mawili na kuonyesha kwa nini anaonekana kuwa mchezaji mwenye uwezo wa kuleta tofauti mbele ya lango.

Kinachomfanya awe na nafasi ya kuaminika ni uwezo wake wa kucheza nyuma ya washambuliaji, pia kuingia kwenye eneo la hatari.

Hata hivyo, akiwa Simba amekuwa akipata nafasi za kucheza mara kadhaa.

Msimu uliopita alicheza mechi nne za ligi, akipata dakika mbili dhidi ya TRA, saba dhidi ya Namungo, 27 dhidi ya Tanzania Prisons na dakika 90 dhidi ya KMC.

Msimu huu bado hajaanza kupata nafasi ya kutosha, lakini kiwango anachokionyesha Ngorongoro kinaweza kumsaidia kupewa nafasi nyingine kwenye kikosi kilichojaa mastaa kibao.


NGORO 03

ABDULNASSIR MOHAMED 'CASEMIRO' – YANGA

Kama kuna eneo Ngorongoro imekuwa na nguvu, basi ni kiungo ambalo linaongozwa na Abdulnassir Mohamed Casemiro.

Huyu ni mmoja wa wachezaji wanaoonekana kama injini ya timu kutokana na uwezo wake wa kuunganisha safu ya kiungo na washambuliaji.

Kwenye mashindano hayo Casemiro amekuwa akipiga pasi ndefu zinazoweza kuibadilisha hali ya mchezo na kuwaweka washambuliaji katika nafasi nzuri.

Amecheza mechi zote mbili za hatua ya makundi na kuwa sehemu ya kikosi kilichofanikisha safari ya kwenda nusu fainali.

Uzoefu wake wa kucheza katika mazingira ya Yanga pia umekuwa msaada kwake, kwani anapata nafasi ya kujifunza namna ya kucheza chini ya presha na matarajio makubwa.

Casemiro alijiunga na Yanga msimu uliopita akitokea Mlandege ya Zanzibar na sasa mashindano haya yamekuwa jukwaa jingine la kuonyesha kile alichonacho.


NGORO 05

JUMA ISSA ABUSHIRI – YANGA

Kwenye upande wa pembeni, Juma Issa Abushiri amekuwa miongoni mwa wachezaji walioleta tofauti.

Winga huyo amekuwa akitumia kasi na uwezo wake wa kukabiliana na mabeki kuisumbua safu ya ulinzi ya wapinzani.

Hadi sasa amefunga bao moja na kutoa asisti moja, akionyesha mchango wake hauishii kwenye kufunga pekee bali pia kutengeneza nafasi kwa wenzake.

Abushiri alijiunga na Yanga msimu huu akitokea Fountain Gate, klabu ambayo ilihusika katika kukuza kipaji chake.

Hilo ni jambo muhimu kwake kwa sababu kucheza kwenye mashindano ya aina hii kunampa nafasi ya kuonyesha kama anaweza kuendeleza kiwango hicho hata anapokutana na ushindani mkubwa zaidi.


NGORO 04

ABDUBAKAR NIZAR ‘NINJU’ – YANGA

Kama safu ya ushambuliaji imekuwa ikifunga, basi nyuma kuna watu wanaohakikisha lango linabaki salama.

Abdulkarim Nizar ‘Ninju’ ni mmoja wao.Beki huyo wa kati wa Yanga amekuwa sehemu muhimu ya safu ya ulinzi ya Ngorongoro, akishirikiana na Shomvi Rajabu, Roonly Gerry na Ismail Ally kuhakikisha wapinzani wanapata wakati mgumu kufika langoni.

Takwimu ya kutoruhusu bao hadi sasa ndiyo ushahidi mkubwa wa namna safu hiyo imefanya kazi.

Ngorongoro imefunga mabao saba bila kuruhusu bao, hivyo kazi ya Ninju na wenzake haiwezi kutenganishwa na mafanikio hayo.


NGORO 01

JUMA SAGWE – KMC

Katika mchezo dhidi ya Ethiopia, mshambuliaji huyo alifunga mabao mawili na kutoa asisti moja, akionyesha ubora wake katika eneo la mwisho.

Sagwe ni miongoni mwa wachezaji wanaokipiga KMC na uzoefu anaoupata kwenye soka la ushindani umemsaidia kuonyesha kiwango kizuri kwenye mashindano haya.

Ana uwezo wa kutumia nafasi anazopata, pia kuwahusisha wenzake, jambo lililoonekana kwenye mchango wake wa mabao na asisti.

Sagwe pia ni miongoni mwa vijana waliowahi kuonyesha kiwango kizuri kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana U-17 mwaka 2024 hivyo huo ni muendelezo tu wa kile alichokifanya.

Kile kinachoonekana kwenye Ngorongoro Heroes ni namna ambavyo uzoefu wa wachezaji hawa kwenye klabu zao unavyoweza kuisaidia timu ya taifa ya vijana.