Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mlipili uwanjani noma, kitaani ndo usipime

Muktasari:

  • Huyu ni Yusuph Mlipili ambaye alitua Simba kwa mkataba wa miaka mitatu akianza mechi yake ya kwanza na ya pekee chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu Joseph Omog dhidi ya Njombe Mji. Baada ya hapo alisubiri hadi alipokuja Kocha Djuma na kumwamini na kucheza mara kwa mara.

BEKI kisiki. Unampitaje kwa mfano. Amewasumbua sana washambuliaji wa timu pinzani na kuwa mhimili mkubwa ndani ya kikosi cha Simba tangu aanze kuaminiwa na kocha msaidizi wa klabu hiyo, Masoud Djuma.

Huyu ni Yusuph Mlipili ambaye alitua Simba kwa mkataba wa miaka mitatu akianza mechi yake ya kwanza na ya pekee chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu Joseph Omog dhidi ya Njombe Mji. Baada ya hapo alisubiri hadi alipokuja Kocha Djuma na kumwamini na kucheza mara kwa mara.

Hakuishia hapo, amekuja pia Mfaransa Pierre Lechantre na kujikuta akizidi kuaminiwa na kucheza hadi mechi zote za kimataifa. Mechi dhidi ya Gendarmerie na ile ya Al Masry Kombe la Shirikisho Afrika na sasa ni kama ameikalia nafasi hiyo moja kwa moja na kumkalisha benchi beki mwingine kisiki Juuko Murshid.

Hata hivyo, ukiacha masuala ya ndani ya uwanja, Mpaka Home kama kawaida yake wiki hii ilimtembelea beki huyo nyumbani kwake anapoishi maeneo ya Kimara Bonyokwa jijini Dar es Salaam, ambako amepanga. Hapo sasa, tuliweza kupiga stori mbili tatu juu ya maisha yake na jinsi anavyojichanganya na washkaji zake.

Maisha yake tangu atue Simba

Kutua Simba kumebadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa jambo ambalo anajivunia.

“Maisha yangu yamebadilika kwa miezi sita tangu nitue Simba, nimefafanya baadhi ya maendeleo ambayo nilishindwa kufanya kabla ya kufika hapa,” anasema.

“Kitu kikubwa ambacho naweza kujivunia kwa sasa ni kuweza kujenga nyumba ambayo ndani ya mwezi mmoja ujao ninaweza kuhamia na kuachana na maisha haya ya kupanga kama ninavyoishi sasa,” anasema.

Maisha ya nyumbani

Anasema kwa kawaida huwa anaamka saa tano kwa siku ambazo yupo mapumziko na hutumia muda mwingi kufanya mambo yake kuhakikisha yanakuwa sawa ikiwamo kusafisha vifaa vyake vya kazi, maeneo ambayo yanamzunguka na baada ya hapo hutumia muda mwingi kupumzika tu ndani na familia yake na wakati mwingine hupiga stori na washkaji zake.

“Huwa napenda sana kuwa na familia yangu au nawaita washkaji zangu ili kubadilishana nao mawazo na hunishauri baadhi ya mambo muhimu kwani wengine wamenizidi umri, mfano kaka yangu Juma Kinto.

“Pia, napenda kukaa na mchumba wangu na kujadili mambo ya msingi ya kimaendeleo ya maisha,” anasema na kufichua, “Mchumba wangu huwa mkali sana pindi tunapoweka mipango kisha mimi nishindwe kuifanikisha kwa sababu ambazo zipo ndani ya uwezo wangu.”

Jikoni ni noma

Suala la njaa wala halimsumbui Mlipili, anaweza kulidhibiti vilivyo kama tu anavyowamudu washambuliaji wa timu pinzani. Msikie kuhusu mapishi.

“Si mtaalamu sana wa kupika vyakula vingi lakini uwezo wa kupika ninao. Naweza kupika ugali, wali na mboga kama nyama na samaki, wakati mwingine napika kwa ajili ya familia yangu.

“Lakini huwa napenda ugali, maharage na mlenda na nikila vyakula hivyo huwa naona mwili wangu unakuwa vizuri na haiwezi kupita muda mwingi bila kuhakikisha napata chakula hicho,” anasema Mlipili na kuongeza, muda wa kula hupendelea kukaa mezani kula pamoaja na familia yake.

Ni msafi kinoma

Mbali na kupika, Mlipili huwa anapenda kufanya usafi na kuhakikisha vitu vyake vinakuwa katika mwonekano mzuri. Wakati mwingine humsaidia dada wa kazi kazi mbalimbali kama kufagia ndani na nje ya nyumba na kupiga deki.

“Wakati mwingine huwa nafua nguo zangu na kumsaidia dada wa kazi. Huwa nafanya haya vizuri na kwa uhakika kwani siku nikiwa na ratiba ya mazoezi napata muda mchache sana kukaa nyumbani, kwani muda mwingi huwa naishi maisha ya kambi ambayo tunakuwa chini ya uangalizi wa kila kitu,” anasema.

Tambi, nyama kambini

Akiwa nyumbani hupendelea zaidi kula ugali ambao hupika mwenyewe, ni tofauti na akiwa kambini na anaweka wazi “Nikiwa kambini mara nyingi napendalea kula tambi na nyama,” anafunguka na kuongeza:

“Kama ninavyopenda kula maharage, mlenda na ugali nikiwa nyumbani, basi kambini napenda kula hivi kwani najihisi mwili wangu kuwa sawa na tayari kwa kufanya mazoezi au mechi,” anasema.

Maskani kwake

Mlipili anasema baada ya kumaliza kufanya usafi wa nyumbani kwake huwa anapenda kwenda maskani kupiga stori na washkaji.

“Baada ya kumaliza kazi zangu na kupumzika natenga muda kwa ajili ya jamaa zangu lakini ambao muda mwingine nawafuata maskani na nakaa nao kupiga stori nyingi tu na huwa nachukua yale ya muhimu na mengine huwa nayaacha hapo hapo,” anasema.

“Napenda kwenda maskani kwani pindi ninapokuwa kambini huwa washkaji ndio wanalinda mali zangu na nyumbani kwetu kuwa salama na hakuna shida yoyote ambayo inaweza kutokea yaani wanakuwa kama walinzi pale kwangu,” anasema.

“Kingine kinachonifurahisha zaidi, marafiki zangu wote mtaani kwangu pale wananikubali na wengine kuamua kutafuta jezi za Simba na kuandika jina langu nyuma mgongoni mwa jezi, hii ni ishara tosha kuwa wanaelewa kazi ninayoifanya,” anasema Mlipili.

Maisha ya ustaa

Mlipili anasema tangu aliposajiliwa na Simba maisha yake yalibadilika na alianza kujulikana sana tofauti na ilivyokuwa hapo zamani. Kwa sasa amekuwa staa zaidi kwani watu wengi wanamfahamu, japokuwa mtaani kwake kuna mambo mengi anayokutana nayo, ya faida na hasara.

“Hasara zinakuwa pale ninapotoka kucheza mechi halafu matokeo yanakuwa tofauti na ushindi huwa napokea maneno mengine ambayo kama si mvumulivu unaweza kujikuta unachukia. Kuna siku nilikwenda kununua chipsi watu walikuwa wananishangaa na kuniuliza kwa nini nakula chakula hicho,” anasema.

“Muda mwingine unakuta watu wa hapa hapa mtaani wanakutumia meseji ambazo si nzuri. Huko kwenye mitandao ya kijamii ndio usiseme. Hata hivyo, nashukuru Mungu kwa hilo nimekuwa na uvumilivu nalo,” anasema.

“Faida kama nilivyosema hapo awali, watu wa mtaani hasa washkaji zangu wanakuwa walinzi wa mali zangu hapa nyumbani na kama nilivyosema tukiwa maskani yanaongewa mengi, hivyo ninachofanya ni kuchukua yale yenye faida na kuyafanyia kazi.”

Anawaogopa akina dada

Kama kuna kitu ambacho staa huyu anaogopa basi ni kuwa karibu na wanawake kutokana na changamoto zao.

“Nimejifunza kutoka kwa wachezaji waliotutangulia kabla yetu, ukiwa unapenda sana starehe ya wanawake huwezi kucheza soka katika kiwango chako na ukadumu katika soka kwa muda mrefu,” anasema Mlipili na kuongeza.

“Pia, sipendi kutumia pombe au kilevi cha aina yoyote na nikiwa kambini au nyumbani huwa natenga muda wangu kufanya ibada na hata viongozi wangu na wachezaji wenzangu ni mashahidi kwa hili,” anasema beki huyo ambaye aliwahi kutamba na Toto Africans ya jijini Mwanza kabla ya kuta Simba.