Mlandege wababe Dabi ya Mtaa
Muktasari:
- Mara ya mwisho timu hizo kukutana, Mlandege ilishinda mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja, msimu wa 2025/26..
Mlandege imeendelea na ubabe katika Dabi ya Mtaa baada ya kuisulubu Muembe Makumbi bao 1-0, mechi ya Ligi Kuu Zanzibar iliyochezwa Septemba 18, 2026.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana, Mlandege ilishinda mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja, msimu wa 2025/26..
Mechi hiyo ilikuwa ya moto kuanzia dakika ya mwanzo hadi 90, huku kipindi cha kwanza kikimalizika bila ya bao licha ya Mlandege kumiliki zaidi mpira.
Mashambulizi ya hatari yaliyofanywa na Mlandege yalizaa matunda dakika ya 79, baada ya kiungo wa timu hiyo, Ramadhan Manzi kuifungia bao pekee akitokea benchi.
Baada ya mechi hiyo, Kocha Msaidizi wa Mlandege, Sabri China amesema ushindi huo umetokana na maandalizi ya mapema waliyoyafanya kwani mechi iliyopita dhidi ya Polisi walipopoteza 2-0, hawakutaka kupoteza mfululizo. Amesema kabla ya mechi hiyo, alichukua nafasi ya kuwasoma wapinzani wao waliotoka kupoteza mbele ya Zimamoto kwa mabao 2-0.
“Nimepata muda mzuri wa kusoma mbinu za mpinzani wangu ndiyo maana nikaja na mbinu ya kushambulia zaidi kuliko kulinda, hatimaye tumepata ushindi,” amesema China.
Kocha huyo ameendelea kutoa pongezi kwa mashabiki wa Mlandege kuisapoti timu hiyo kwa kila hatua inayopiga.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa Mlandege msimu huu katika mechi tatu za Ligi Kuu Zanzibar na sasa imefikisha pointi nne ikishuka dimbani mara tatu, ikiambulia sare moja na kupoteza moja ikikamata nafasi ya tisa kabla ya mechi za jana Jumapili, huku Muembe Makumbi ikiwa ya sita na pointi sita ikicheza mechi nne.