Mikakati mipya ya Pep Baryen ni kupiga pasi nyingi
Muktasari:
- “Bado kuna kazi kubwa ya kufanya na tutaanza na hilo msimu ujao, nimefundisha kiasi cha kutosha kwa msimu huu na tunachohitaji ni kuifanyia kazi katika mechi za mashindano, msimu ujao tutakwenda mbele zaidi, tunaweza kupoteza mechi zaidi lakini kijumla uchezaji wetu utakuwa bora.
TOLEO lililopita kwenye kitabu cha Pep Confidential, mwandishi Marti Perarnau aliendelea na mazungumzo yake na Kocha Pep Guardiola ambaye alifunguka kuhusu mikakati yake kwa msimu wake wa kwanza Bayern akiwa tayari na taji la Bundesliga mkononi pamoja na maandalizi ya msimu ujao. Sasa endelea…
“Bado kuna kazi kubwa ya kufanya na tutaanza na hilo msimu ujao, nimefundisha kiasi cha kutosha kwa msimu huu na tunachohitaji ni kuifanyia kazi katika mechi za mashindano, msimu ujao tutakwenda mbele zaidi, tunaweza kupoteza mechi zaidi lakini kijumla uchezaji wetu utakuwa bora.
“Wachezaji watakuwa na mwaka mmoja wa lugha hii mpya ya kiuchezaji na watakuwa wameimarika zaidi, tutajaribu mbinu nyingine kwa mapana, kuna siku tutacheza na mabeki watatu na siku nyingine na mawinga wanaokaba kwenye eneo lao na tutatawanya mipira katikati ya uwanja kwa kumtumia namba 10 na viungo washambuliaji, kijumla naamini msimu ujao timu itaimarika zaidi.
Anauzungumzia mpira ndiyo msingi wa kila kitu, “Ni mpira ambao unakupa kasi, uwezo wa kutoa pasi. Katika mpira wa kikapu unapouchezea mpira kila wakati, mabeki mambo yao yanakuwa rahisi lakini ukitoa pasi za haraka haraka unawapa wakati mgumu kwa wapinzani wako.
“Ni hivyo hivyo katika soka, nakupa pasi unanirudishia hapo hapo na unamfanya mpinzani wako anaunga tela akikukimbiza huku ukionekana kama vile haufanyi kazi yoyote kubwa. Ndiyo maana nafanya kila linalowezekana kuhakikisha tunapeana pasi mara kwa mara na kwa haraka tukiwa nusu ya uwanja eneo la wapinzani.
“Nataka washambuliaji wangu wawili kuwabana mabeki wa timu pinzani, kwa ubora zaidi nataka kulifanikisha hilo nikiwa na mshambuliaji mmoja ingawa mshambuliaji huyu anatakiwa awe mtaalamu hasa katika kufanikisha jambo hili ili kuwawezesha washambuliaji wengine kupeleka mipira mbele na kutengeneza vyumba hasa katika eneo la kati.
“Toa pasi, toa pasi si tu kwa sababu ya kutaka kuumiliki mpira, badala yake iwe ni kwa sababu ya kuwavuruga wapinzani wenu, kwenda na pasi kwa staili hiyo kunatuweka katika utaratibu mzuri na kuwaacha wapinzani wakiwa wameparaganyika.
“Makocha kama kina Juanma Lillo (kocha Mhispaniola ambaye ni kama mwalimu kwa Pep) na Raul Caneda (kocha aliyewahi kufanya kazi na Lillo Mexico na Hispania) mara zote wamekuwa wakilisema hili, inaweza isionekana kama mnafanya sana, lakini pasi za kasi na haraka si tu zinawaweka katika utaratibu mzuri bali pia zinaifanya timu nyingine kuharibikiwa,” anafafanua Pep.
“Hata hivyo, hakuna kati ya hilo linalowezekana kama wachezaji wenu hawachezi katika mfumo, au ecolo qua (kama anavyopenda kusema Pep akinukuu msemo maarufu wa Kitaliano) na hapo hapo linakuja swali la msingi, unawezaje kuwashawishi wachezaji wako kukusikiliza na kukubali dhana mpya? Namaanisha kuhamasisha si kushawishi.
“Kwa kilichotokea Barca si kwamba nilishindwa kuwashawishi, wale ni wachezaji wazuri na watu wa aina yake, hapana nilichoshindwa ni kuwahamasisha, nilibuni mbinu nyingi mpya katika miaka minne na hatua iliyofuata haikuwa rahisi.
“Unawaangalia wachezaji wako machoni na inakuwa kama vile unamwangalia mpenzi wako, unaona hamasa na utayari wa kuhamasishwa au unaona hamasa imeondoka, kitu hicho hicho kinaweza kutokea hapa Bayern.
“Baada ya miaka michache ijayo, nitakuwa tena sina ule uwezo wa kuwahamasisha wachezaji wangu na huo utakuwa wakati wa kuondoka, kila kitu kitakuwa kikionekana machoni, hapo suala kubwa ni uwezo wa kuhamasisha wachezaji.”
Itaendelea Jumamosi