Migne apewa mechi 4 Dar
Muktasari:
Uongozi wa Yanga kupitia kwa Senzo Mazingisa licha ya kutoweka wazi jina la Kocha huyo lakini amethibitisha kwamba atatua nchini kabla ya mechi ya kwanza ya mashindano. Mwanaspoti limejiridhisha kwamba Kocha mpya wa Yanga ni Mfaransa,Sebastian Migne ambaye amewahi kuipeleka Yanga kwenye Afcon.
KOCHA mpya wa Yanga, amepewa mechi nne mfululizo kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam kuwasoma vijana wake na ikiwezekana aongeze maujuzi.
Uongozi wa Yanga kupitia kwa Senzo Mazingisa licha ya kutoweka wazi jina la Kocha huyo lakini amethibitisha kwamba atatua nchini kabla ya mechi ya kwanza ya mashindano. Mwanaspoti limejiridhisha kwamba Kocha mpya wa Yanga ni Mfaransa,Sebastian Migne ambaye amewahi kuipeleka Yanga kwenye Afcon.
Yanga mechi ya kwanza itacheza dhidi ya Prisons kwenye Kombe la FA, Jumatano ijayo mkoani Rukwa lakini Mwanaspoti linajua kwamba Migne ataitazama kwenye televisheni akiwa tayari Dar es Salaam kama alivyoanza kutazama video kibao zilizopita za Yanga akiwa kwao akiagaaga na kufungasha.
“Kuna mambo tunakamilisha Kocha mpya atatua kabla ya kuanza mechi zetu,”alisema Senzo licha ya kutomtaja jina na siku anayowasili. Habari ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Yanga wamekubaliana na Migne kwamba atazitumia mechi hizo nne za Dar es Salaam kuifanyia tathmini ya kina timu yake na kuongeza ujuzi kwani mechi hizo ni muhimu kwenye Ligi Kuu Bara na kuendelea kushikilia usukani.
Mechi nne ambazo Yanga itacheza kwenye Uwanja wa Taifa mfululizo ni dhidi ya KMC Jumamosi ya Aprili 10, kisha watawavaa Biashara Aprili 17, dhidi ya Gwambina Aprili 20 na Azam Aprili 25 mechi zote zikichezwa usiku kwenye Uwanja wa Mkapa.
Yanga inaendelea na matizi, Kigamboni Jijini Dar es Salaam chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mwambusi ambaye amesisitiza kwamba kwake yeye ni soka la kushambulia tu na ushindi ni muhimu.
Ameliambia Mwanaspoti mazoezini kwamba Yanga ina mastaa wengi wenye uwezo na ana imani kwamba itafanya maajabu kwenye mechi zijazo.
“Mimi ni muumini wa ‘direct football’ ndiyo nahitaji Yanga icheze,tunafanya mazoezi ya ufiti na mbinu, tunakwenda vizuri na bahati nzuri wachezaji wamejitoa, sina shaka kwamba Ligi itakapoendelea tutazidi kuwa bora zaidi na kufanya vema,” alisema.
“Ligi bado sana na kwenye msimamo Yanga ndiyo tunaongoza, suala la ubingwa ni la muda tu, hivyo tupeni muda na nasisitiza lengo liko pale pale,” alisema kocha huyo mzawa aliyewahi kutamba na Mbeya City, Prisons, Azam na Moro United.
Kocha wa zamani wa Simba, Patrick Aussems ambaye kwasasa yupo Kenya akiinoa AFC Leopards, amelithibitishia Mwanaspoti kwamba Migne amempigia simu akimuuliza Yanga ilivyo na maisha ya Simba na Yanga yalivyo na yeye alimwambia kila kitu akasema freshi.
SAIDO NA MUKOKO
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli wachezaji Saido Ntibazonkiza wa Burundi na Mukoko Tonombe wa DR Congo kuna uwezekano mkubwa wakatua nchini kesho.
Anasema kila kitu kuhusu wachezaji hao kiko sawa changamoto imekuwa ni ratiba za ndege, ila wameshapata ufumbuzi. Saido aliyekuwa majeruhi ameshakaa sawa na anaweza kucheza kama ilivyo Mukoko ambaye gari lake kwa sasa limewaka.