Mhilu kulamba dili jipya Geita Gold
Muktasari:
- Geita Gold iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, imerejea Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, baada ya kuibuka mabingwa wa Ligi ya Championship, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza nafasi ya pili na Polisi Tanzania iliyopanda kwa ‘Play-Off’.
UONGOZI wa Geita Gold, uko katika hatua za mwisho za kumwongezea mkataba wa miaka miwili nahodha wa kikosi hicho, Yusuph Mhilu, baada ya kuonyesha kiwango kizuri kilichochangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kurejea Ligi Kuu Bara.
Geita Gold iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, imerejea Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, baada ya kuibuka mabingwa wa Ligi ya Championship, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza nafasi ya pili na Polisi Tanzania iliyopanda kwa ‘Play-Off’.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Geita Gold, Samwel Dida alisema kuna wachezaji wanaoendelea na mazungumzo nao ya kuongeza mikataba mipya, japo ikiwa makubaliano kati ya pande zote mbili yatafikiwa watayaweka wazi.
“Tumeanza kutambulisha wachezaji wapya lakini tunaendelea na baadhi yao walioipigania timu msimu wa 2025-2026, kwa lengo la kuwaongezea mikataba kutokana na ripoti ya benchi letu la ufundi, kisha tutakapokamilisha tutatangaza,” alisema Dida.
Licha ya kauli ya Dida, Mwanaspoti linatambua Mhilu aliyewahi kuzichezea pia timu za Kagera Sugar, Yanga na Simba, amefikia maku baliano ya kusaini mkataba wa miaka mingine miwili, baada ya kuonyesha kiwango cha kuvutia kwa msimu wa 2025-2026.
Kwa msimu wa 2025-2026 katika Ligi ya Championship, Mhilu aliifungia Geita Gold mabao matano na kuonyesha kiwango bora kwa wachezaji wenzake akiwa ndiye nahodha, jambo lililowavutia mabosi wa timu hiyo kumwongezea tena miaka miwili.
Wakati Mhilu akisaini mkataba mpya, timu hiyo imemsajili mfungaji bora wa Ligi ya Championship kwa msimu wa 2025-2026, Mzambia Obrey Chirwa aliyeifungia Kagera Sugar mabao 18, aliyeondoka kwenye kikosi hicho baada ya mkataba wake kuisha.
Chirwa aliyechezea Yanga, Azam FC, Namungo FC, Ihefu kwa sasa Singida Black Stars, KenGold na Kagera Sugar za Tanzania, ameungana na mshambuliaji, Maulid Shaban ambao wote kwa msimu wa 2025-2026 kila mmoja alifunga mabao 18.