Mgombea Uenyekiti Simba asusa kikao
Mgombea nafasi ya Mwenyekiti kwenye uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba, Moses Kaluwa ameondoka ukumbini baada ya kuambiwa mkutano huo wa kujinadi kwa wanachama haukumhusu yeye.
Mwongoza mkutano huo unaofanyika leo Januari 23 jijini Dar es Salaam alitangaza kwa wanachama kuwa mpinzani wa Kaluwa ambaye ni Mwenyekiti anayemaliza muda wake Murthaza Mangungu ndiye mwenye mkutano huo pamoja na wagombea wengine.
Baada ya kutangaza hivyo, Kaluwa aliomba kuzungumza; "Naomba niweke sawa, niliambiwa kikao hiki ni cha pamoja lakini nashangaa muda huu naambiwa changu kitapangwa siku moja kabla ya uchaguzi na sio kwamba mimi nimeomba hivyo."
Baada ya kuzungumza hayo Kaluwa na wapambe wake waliamua kuondoka ukumbini.
Alipoulizwa juu ya tukio hilo Kaluwa amejibu kwa ufupi; "Samahani mwandishi, nikimaliza nitakupigia."
Hata hivyo, wanachama waliokuwepo ukumbini hapo wamedai kuondoka kwa mpinzani wa Mangungu ni kutokana na kile kilichodaiwa wapambe wa mpinzani wake kumpiga madongo.
Uchaguzi mkuu wa Klabu ya Simba unatarajia kufanyika Januari 29 ambapo mwisho wa kampeni ni Januari 28 mwaka huu