Mghana Yanga aanza na mkwara
KOCHA mpya wa viungo wa Yanga, Mghana Eden Mortosin amesisitiza kwamba yeye falsafa yake ni ushindi tu na haamini kwenye matokeo mengine.
Eden ambaye amekulia Canada akifanikiwa zaidi na klabu ya FC Edmonton katika nafasi ya kiungo, ameongeza kwamba hata kilichomfanya astaafu kucheza na kuhamia kwenye ukocha ni ari ya ushindi na kutotaka kushindwa kwa namna yoyote ile.
“Mashabiki wategemee ushindi kutoka kwangu, nitafanya kila kinachowezekana kuhakikisha timu inashinda, huwa sikubali kushindwa,” alisema ambaye kwa mujibu wa rekodi za mitandaoni hajafikisha miaka 30.
“Naamini nimefanya uamuzi mzuri kujiunga na Yanga na nitafanya mambo mazuri, kikubwa zaidi kikiwa ni ushindi,” aliongeza Eden ambaye wakati anatua Dar mitandao yote ya Ghana iliripoti Yanga imesajili kiungo wakijua kwamba anakuja kucheza.
Eden ameshiriki kozi mbalimbali barani Ulaya jambo lililomjengea kiburi Kaze na kuamua kumuinulia simu aje Jangwani.
Kocha Kaze ameliambia Mwanaspoti kwamba ameamua kuingiza damu changa kwenye benchi lake la ufundi ili kuendana na mabadiliko yaliyokp kwenye soka la kisasa.
Alisema kwamba uwepo wa Eden na Kocha Msaidizi, Nizar Khalfan utamsaidia kuchangamsha kikosi kwani wamecheza soka kwa mafanikio kwa ngazi mbalimbali, hivyo itakuwa rahisi hata kwa wachezaji kupambana zaidi kwa vile watakuwa wanaona mifano halisi.
“Soka limebadilika duniani, mambo mengi ni ya kisasa hivyo ni lazima uwe na vijana ambao wanaelewa mambo mengi, ndio maana nikaweka damu changa na ambao wanajua mambo mengi, hii itasaidia hata wachezaji kukazana zaidi kwa vile wanaona mifano halisi,” alisema Kaze ambaye anaamini kwamba kikosi chake kitakuwa fiti mpaka mechi za ligi zitakaporejea wikichache zijazo.
Yanga inaanzia mzunguko wa pili Jijini Mbeya kwa kucheza na wenyeji Mbeya City. Hadi Ligi inasimama Yanga ilikuwa haijapoteza mchezo wowote na katika dirisha dogo imeongeza mastaa wawili wa kigeni, Saido Ntibazonkiza na Fiston Abdul Razak wote raia wa Burundi alikotoka Kocha Kaze na yule wa Makipa, Vladmir Niyonkuru ambaye ni staa wa zamani wa Azam.
Mzawa Yanga imesajili mmoja tu kwenye dirisha dogo ambaye ni Dickson Job beki aliyekuwa tegemeo ndani ya Mtibwa.