Metacha kuikosa nusu fainali Cecafa
GOLIKIPA wa Tanzania Boniface Mnata Metacha ataikosa mechi ya nusu fainali dhidi ya Sudani Kusini mchezo utakaopigwa leo saa 5:45 asubuhi katika mashindano ya ukanda wa Afrika Mashariki na kati (CECAFA) U-23, katika uwanja wa Bahir Dar, Nchini Ethiopia.
Metacha anaikosa mechi hiyo baada ya kupata kadi za njano kwenye michezo ya hatua ya makundi dhid ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mechi dhdi ya Uganda.
Benchi la ufundi la Tanzania’ likiongozwa na Kocha mkuu wa timu hiyo Kim Poulsen itabidi kufanya mabadiliko kwenye idara hiyo kwa kutoa nafasi kwa magolikipa Daniel Mgore au Wilbol Maseke.
Poulsen alisema kuwa “Ni bahati mbaya kwa Metacha kukosa mchezo huo muhimu wa nusu fainali kwa sababu ameonyesha kiwango kizuri katika michezo miwili iliyopita ila hatuna budi kufanya marekebisho kwenye kikosi cha leo"
Tanzania imetinga hatua hiyo ya nusu fainali baada ya kuifunga DR Congo kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza huku ikitoa sare ya 1-1 dhidi ya Uganda, huku wapinzani wetu Sudan Kusini wakianza vyema mashindano kwa kuifunga Kenya mabao 2-0, na kuifunga Djibouti kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa pili wa hatua ya makundi.
Michuano hii inayoendelea nchini Ethiopia imeanza kutimua vumbi Julai 18 huku ikitarajiwa kufikia tamati Julai 30 ambapo itakuwa ni siku ya fainali.
IMEANDIKWA NA DAUDI ELIBAHATI