Mechi 3 za heshima Stars
FAINALI za Chan zinaanza leo Januari 16 nchini Cameroon. Zitapigwa mechi mbili za kundi A. Moja saa 1 usiku mwenyeji Cameroon kukipiga na Zimbabwe.
Saa 2 usiku Mali watacheza na Burkina Fasso. Tanzania ni miongoni mwa timu zinazoshiriki michuano hiyo na ipo kundi D na timu za Namibia, Guinea na Zambia.
Tanzania ina mechi tatu muhimu ambazo ikizichanga vizuri itafuzu hatua ya robo fainali.
Mechi ya kwanza itakuwa dhidi ya Zambia Jumanne ijayo - hii ikichezwa saa 11 jioni. Baada ya hapo wataikabili Namibia saa 4 usiku na mechi ya mwisho itakuwa dhidi ya Guinea Januari 27 - mechi hizo zikipigwa saa 2 usiku.
Stars imepania kufanya vizuri kwenye michuano hiyo kutokana na aina ya kikosi walicho nacho. Fainali hizo zinahusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani ambapo asilimia kubwa ya wachezaji wanaounda Taifa Stars wanacheza Ligi Kuu Bara na Zanzibar.
Wachambuzi wa soka wanaipa Tanzania maarufu kama Taifa Stars nafasi ya kufanya vizuri na kufuzu hatua ya robo fainali. Kocha wa Stars, Ettiene Ndayiragije amesema kwamba kikosi hicho kipo kwenye morali ya kiushindani na wana mzuka wa kufanya vizuri, ingawa kundi lao ni gumu.
Alisema kwamba wachezaji pamoja na benchi la ufundi wamejipanga kimkakati kukabiliana na kila mechi na mwisho wa siku msimamo wa kundi utaongea.
Anasema kwamba kipimo cha mechi ya kirafiki ya DR Congo kimewapa mwanga wa nini cha kubadili kwenye kikosi hicho na ana uhakika mambo yatakwenda vizuri. Hii ni mara ya pili Stars kushiriki Chan kwani mwaka 2009 ilikwenda na Marcio Maximo na kuishia hatua ya makundi.
Stars msimu huo ilikuwa kundi moja na Zambia, Senegal na Ivory Coast ikamaliza na pointi nne kwa kushinda mechi moja, droo moja na kupoteza moja. Stars ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Senegal, Mrisho Ngassa akaifunga Ivory Coast bao moja kabla ya kulazimisha sare na Zambia kwa penalti ya Shadrack Nsajigwa dakika ya 88. Zambia na Senegal zikafuzu robofainali. DR Congo ikabeba ubingwa msimu huo.