MCL: Tusaidieni kumpata Azory
Muktasari:
Akizungumza na waandishi wa habari ikiwa tayari zimepita siku 100 tangu mwandishi huyo atoweke, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai alisema wanawakaribisha wenye mapenzi mema ya kusaidia kupatikana kwa mwandishi huyo kutoka ndani na nje ya nchi, lakini inawapasa wafuate taratibu za kidiplomasia na sheria za nchi.
KAMPUNI ya Mwananchi Communication Limited (MCL), imesema yeyote mwenye mapenzi mema kutoka katika vyombo vya ndani au nje ya nchi, ajitokeze kusaidia kumtafuta mwandishi wake aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha, Azory Gwanda.
Akizungumza na waandishi wa habari ikiwa tayari zimepita siku 100 tangu mwandishi huyo atoweke, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai alisema wanawakaribisha wenye mapenzi mema ya kusaidia kupatikana kwa mwandishi huyo kutoka ndani na nje ya nchi, lakini inawapasa wafuate taratibu za kidiplomasia na sheria za nchi.
"Uamuzi huu haumaanishi kwamba hatuna imani na vyombo vya ndani, tunaamini baada ya mkutano huu juhudi za kumtafuta Gwanda zitaongezeka na atapatikana akiwa hai na mwenye afya njema, ”alisema Nanai.
Gwanda aliyekuwa akiishi na kufanya kazi Wilayani Kibiti, Pwani alitoweka Novemba 21, 2017 na tangu wakati huo hajaonekana na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusu mustakabali wake.
Mara ya mwisho, Azory alionekana akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe na kwa mujibu wa Anna Pinoni, ambaye ni mkewe , alichukuliwa na watu wasiojulikana akiwa katika eneo ambalo hupenda kukaa akiwa na wenzake.
Nanai alisema Wafanyakazi na wanajumuiya ya MCL wanakemea kitendo hicho cha Gwanda kuchukuliwa na watu wasiojulikana.
Alifafanua kuwa kitendo hicho ni dhambi kubwa mbele za Mungu kwa waumini dini na madhehebu yote na ni kitendo cha uvunjaji wa haki za binadamu na ni utamaduni mbaya, udhibitiwe haraka ndani ya nchi yetu ambayo ilikuwa ni kioo cha Amani, Upendo na Mshikamano kwa jirani zetu na duniani kote.
Alisema , “Tunaomba tena, Azory arudishwe akiwa mzima na mwenye afya njema ili aungane na familia yake katika kuendesha maisha yao na ujenzi wa taifa letu. Tunachukua nafasi hii kutoa pole kwa Watanzania wote waliopatwa na majanga mbalimbali ya kutekwa ama kuuawa ama yote mawili. Tunamwomba Mungu awe mfariji wenu.”