Kiungo Simba arejea Zambia
Muktasari:
- Nyota huyo aliyejiunga na Simba Julai 1, 2024, akitokea Power Dynamos, alijiunga na Al Adalah Club ya Saudi Arabia katika dirisha dogo la Januari 2026 kwa mkopo, kisha mwisho wa msimu wa 2025-2026 Simba ikampa mkono wa kwaheri.
ALIYEKUWA kiungo mshambuliaji wa Simba, Mzambia Joshua Mutale, amekamilisha usajili wake wa kurejea Klabu ya Power Dynamos ya kwao Zambia, baada ya mkataba wake na kikosi hicho cha mitaa ya Msimbazi jijini Dar es Salaam kumalizika.
Nyota huyo aliyejiunga na Simba Julai 1, 2024, akitokea Power Dynamos, alijiunga na Al Adalah Club ya Saudi Arabia katika dirisha dogo la Januari 2026 kwa mkopo, kisha mwisho wa msimu wa 2025-2026 Simba ikampa mkono wa kwaheri.
Hatua ya mchezaji huyo kuichezea Al Adalah ya Saudi Arabia ilijiri baada ya dili lake la kujiunga na Kenya Police ya Kenya kukwama, kisha kutua kikosini humo na mkataba wake na Simba ulipoisha msimu wa 2025-2026, akaondoka rasmi.
Baada ya dili la nyota huyo kwenda Kenya kukwama, Al Adalah Club iliyoanzishwa mwaka 1984, ikiwa na miaka 42, ilionyesha nia ya kumsajili kwa mkopo, huku pia kukiwa na kipengele cha kumnunua moja kwa moja, ingawa haikufanikisha usajili huo.
Wakati nyota huyo anajiunga na Simba alisaini mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mwingine mmoja zaidi, japo vigogo hao hawakuwa tena na mpango naye jambo lililomfungulia mlango wa kutokea ili akatafute changamoto mpya.
Baada ya kuachana na Simba, nyota huyo amerejea Power Dynamos aliyowahi kuichezea kabla ya kujiunga na kikosi hicho cha mitaa ya Msimbazi, ambapo amesaini mkataba wa miaka miwili na muda wowote atatambulishwa.