Mbili zamuwania aliyeachana na Mwenge
Muktasari:
- Timu zinazotajwa kumuwania kocha huyo zote ni za Pemba ambazo ni Wawi Stars inavyoshiriki Ligi Daraja la Kwanza na Fufuni ya Ligi Kuu Zanzibar, huku mwenyewe akithibitisha kweli yupo katika mazungumzo na timu nyingine.
ALIYEKUWA KOCHA Mkuu wa Mwenge, Msellem Sultan Hemed, amethibitisha kuachana na timu hiyo baada ya kufikia makubaliano ya pande zote mbili, huku taarifa zikieleza kwamba timu mbili zinamuwania.
Timu zinazotajwa kumuwania kocha huyo zote ni za Pemba ambazo ni Wawi Stars inavyoshiriki Ligi Daraja la Kwanza na Fufuni ya Ligi Kuu Zanzibar, huku mwenyewe akithibitisha kweli yupo katika mazungumzo na timu nyingine.
Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu kuachana na Mwenge, kocha huyo amesema ameamua kujiweka pembeni kutokana na kutoridhirishwa na mazingira yake jambo ambalo lingemnyima fursa ya kazi yake.
“Ukiachana na sababu ya mfululizo wa matokeo mabaya kwa timu, lakini sijaridhishwa na mazingira yake ya mpira kwani sio ya mpira wa kisasa,” amesema.
Kocha huyo, amesema amekubaliana na uamuzi kwa amani na kueleza kuwa mpira wa miguu una matokeo ya aina tatu na mabadiliko ni sehemu ya mchezo.
Alibainisha kwamba, ameamua kuacha nafasi hiyo ili kutoa fursa kwa walimu wengine kuleta fikra na mbinu mpya zitakazoweza kuirejesha Mwenge kwenye ushindani na kufikia malengo yao.
Kocha huyo aliiongoza Mwenge katika mechi nne za Ligi Kuu Zanzibar msimu huu na kupoteza zote dhidi ya Muembe Makumbi (2-0), Raskazone (2-1), Uhamiaji (2-0) na Black Sailors (2-1).
Huyo anakuwa kocha wa pili kuondoka katika timu zinazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar msimu huu.