Matola -6: Waarabu wawawekea Simba video za ngono

JANA tuliishia sehemu ambayo wachezaji wa Simba wamepewa hoteli yenye vurugu za kutosha, ilikuwa sehemu yenye fujo sana na ipo katikati ya jiji wakiwa ghorofa ya pili, lakini juu yao kuna ukumbi wa disco, hivyo kelele ni nyingi sana.
Lakini kumbuka huko nyuma tulishaona sehemu ambayo Selemani Matola alianzia soka lake na kupambana hadi kufikia kuwa mchezaji wa kutegemewa kwenye kikosi cha Simba akiwa ameshaanza kuonja ladha ya makombe.
Tumeona hajacheza mechi ya kwanza Dar es Salaam kutokana na kuwa na majeraha ya kidole, kuna maswali mengi kama atacheza mchezo wa pili kwa kuwa aliyecheza mchezo wa kwanza alikuwa bora kwelikweli.
Je, nini kitafuata, Simba itahama hoteli au itaendelea kufanyiwa vituko? Tiririka nayo...!
TIMU YATINGA HATUA YA MAKUNDI
Matola anasema Simba ilifanikiwa kutinga hatua ya makundi baada ya awali kuitupa nje timu kutoka Botswana na baadaye waliitupa nje Santos kutoka Afrika Kusini, anasema wakati huo timu yao ilikuwa na kasi ya juu sana na Kocha Aggrey Siang’a alikuwa na ubora wa hali ya juu.
“Baada ya hapo, hali ilikuwa tofauti kwetu kwani tulivaana na Zamalek ya Misri, kumbuka wakati huo ndiyo ilikuwa klabu bora na maarufu zaidi kwenye soka la Afrika, ilikuwa na mastaa kibao na ilikuwa imeshatwaa ubingwa wa Afrika mara mbili hivyo maandalizi yetu hayakuwa ya mchezo hata kidogo.
“Nakumbuka wakati huo ilikuwa na mastaa wakubwa kama Hossan Hassan, Mohammed Barakat pamoja na mastaa wengine kama Mohammed Abuutrika, ukweli jamaa walikuwa sawa hawa na sisi viongozi walikubaliana tuende tukaweke kambi Zanzibar, ambapo tulikaa Zanzibar Beach Resort, baadaye tulirudi Dar es Salaam kwa ajili ya mechi.
MATOLA AKAA JUKWAANI
Anasema maandalizi ya mchezo wa kwanza yalikamilika chini ya Siang’a ambapo walirejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo, lakini wakiwa kule Zanzibar aliumia kidole, hivyo hakucheza mchezo wa hapa Dar.
“Kule Zanzibar niliumia kidole, mchezo wa kwanza dhidi ya Zamalek hapa Dar sikucheza, alianza dogo mmoja anaitwa Amani Mbaruku, alicheza vizuri sana hii mechi nakumbuka nilikuwa jukwaani.
“Baada ya kufanikiwa kuwachapa Waarabu bao 1-0, walizunguka uwanjani wakiwa wanashangilia, walitushangaza sana, sisi tumewafunga lakini wao ndiyo wanashangilia, lakini tukaambiwa kwa Waarabu kwao ni kawaida kufurahia kufungwa bao moja kwa kuwa wanaamini wanakwenda kushinda zaidi ya mabao manne kwao.
“Jamaa walifurahi sana, hii ilitupa maswali mengi na nguvu zaidi ya kujiandaa kabla ya kwenda kwenye mchezo wa pili.
FRIENDS WAKUTANA, TIMU YAENDA OMAN
Matola ambaye ni kati ya wachezaji wa zamani wenye mafanikio makubwa zaidi nje ya soka hapa Tanzania, anasema baada ya mechi hiyo viongozi walikutana na kukubaliana timu inatakiwa kwenda kwenye nchi za Kiarabu na wapate baadhi ya michezo ya kirafiki huko hivyo wakakubaliana iende Oman.
“Unajua wakati huo Friends walikuwa wanafanya kazi kubwa sana kwenye timu, hawa kina Try Again, Kassim Dewji ambaye wakati huo alikuwa katibu wa timu, Mulam Ng’wambi kina Crescentius Magori na mfadhili Mo Dewji walifanya kila jitahada kuhakikisha kuwa tunashinda michezo yetu yote ya mbele.
“Walituita usiku ule baada ya mchezo na kutupongeza, wakatuambia kuwa timu inatakwenda Oman, kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa marudio ambao kama sikosei ulitakiwa kupigwa siku 12 hivi mbele, tulielezwa asubuhi tutaondoka na kila mmoja anatakiwa kujiandaa kwa ajili ya safari na kweli asubuhi yake tuliondoka tukaenda uwanja wa ndege.
TALIB HILAL AUNGANA NA TIMU, AWAPA MBINU
Matola anasema baada ya kufika Oman walipokelewa na mchezaji wa zamani wa Simba, Talib Hilal na watu wengine ambao walionekana waliandaliwa maalumu kwa ajili ya kuwapokea na kuwapeleka hotelini.
“Tulipofika hotelini tuliitwa na Talib alitambulishwa kwetu kuwa tutakuwa naye kama kocha ambaye atasaidiana na Siang’a kwa ajili ya maandalizi ya mchezo uliopo mbele yetu. Kila mtu anaweza kusema lake, lakini ukweli Talib alitusaidia sana, alitufundisha mambo mengi ambayo hatukuwahi kuyafahamu huko nyuma.
“Tulianza maandalizi na Talib alikuwa anatufundisha mambo mengi kupitia kwenye kompyuta, alitueleza mbinu za Waarabu, akasema wana mbinu nyingi sana chafu, lakini alituambia hata uwepo wetu Oman na kila tunachofanya Zamalek wanafahamu, alitueleza walikuwa wanatufuatilia, lakini tukiamua kupambana hakuna linaloshindikana.
“Baada ya kumaliza maandalizi pale, siku tatu kabla ya mechi tulianza safari kwenda Misri, siku ya kuondoka asubuhi tukiwa uwanja wa ndege tulikutana na msafara ukiwa unatokea Tanzania ukiwa na watu kama 20 hivi pamoja na baadhi ya viongozi wa Friends, nakumbuka walikuwepo kina Dokta Ramadhani Dau, Waziri Juma Kapuya, Joseph Kusaga na wengine wengi, ambao walikuwa wana kila kitu kuanzia unga, maji, chumvi, sukari mafuta, juisi, mchele na vyakula vingine vingi.
“Mambo yote haya, yalianza siku nyingi sana, ukiwaona Simba leo wanasafiri na vyakula ujue walianzia mbali.
WAWEKEWA VIDEO CHAFU HOTELINI
Matola anasema wakati ule, timu mwenyeji ndiyo iliyokuwa na jukumu la kumwandalia ngeni kila kitu, chakula pamoja na hoteli hivyo walipofika Misri waliletea basi, wakachukuliwa na kupelekwa hotelini.
“Unajua Waarabu wa fitina sana, walituchukua vizuri na kutupeleka hoteli moja ipo katikati ya jiji, yaani kuna kelele mwanzo mwisho, hii hoteli ilikuwa na ukumbi wa disko juu, hivyo jamaa walituweka kwe eneo ambalo ni karibu sana na ule ukumbi.
“Kulikuwa na wanawake wanavaa ovyo kweli kweli, kelele zilikuwa nyingi kwenye korido wanawake wanapita kila mara wamevaa ovyoo, jamaa nafikiri walifanya hivi makusudi kabisa kututoa mchezoni.
“Lakini ukiachana na hilo jambo lingine ambalo jamaa walifanya la ajabu, walizima chaneli zote kwenye televisheni na kuacha mbili tu ambazo muda wote zinaonyesha picha chafu za ngono.
Nini kiliendelea? Usikose mwendelezo wa makala haya kesho