MATOLA -4: Masatu akosa penalti, Simba ikaichapa Yanga

KATIKA mfululizo wa makala ya maisha ya Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, toleo la kwanza tuliona jinsi ambavyo kocha huyo alivyotoka mkoani kwao Kigoma na kuanzia safari yake ya soka, Toto African ya Mwanza, baadaye alijiunga na Kagera Star.
Lakini toleo la jana tulimuona Matola akianza kwenye kikosi cha kwanza Simba, lakini akieleza jinsi ambavyo kundi maarufu la Friends Of Simba lilivyoiteka timu hiyo na kwenda kuificha Morogoro, akasimulia kuhusu ugomvi mkubwa kambini baada ya kichapo dhidi ya Yanga mkoani Arusha, leo Matola anaendelea kueleza kuhusu hali ilivyokuwa kwenye kikosi cha Simba, shuka nayo...
SIMBA YAFYEKA NYOTA 20
“Baada ya msimu kumalizika, viongozi walikasirika sana, tukatangaziwa kuwa wachezaji 20 lazima wakatwe kwenye timu kweli mwisho wa msimu wachezaji waliondolewa tukabaki watu 10 tu kwenye timu viongozi wakasema kuwa wataongeza wachezaji wengine, lakini hata Kibadeni naye aliondoka timu ikawa chini ya Syllersaid Mziray.
“Muda mrefu kabla ya ligi kuanza tulitakiwa tuwe kambini Dar, tulikuja na kuanza mazoezini pale Jangwani kwenye Uwanja wa Simba, wachezaji wengi walikuwa wanakuja pale kutafuta nafasi, tuliobaki tulianza kuongeza juhudi mara mbili zaidi.
“Walikuja kina Shekhan Rashid, Mohammed Mwameja alirudi tena alikuwa akitokea England, George Masatu alitokea Indonesia akaja naye mazoezini, akaja William Fanibuller huyu alikuwa raia wa Liberia, akawepo Ally Yusuf ‘Tigana’ na Mwanamtwa Kihwelo, wengi kati ya hawa walisajiliwa timu ikawa mpya kabisa.
“Hapa nilijifunza mambo mengi sana kwa kuwa wachezaji wengi walikuwa wazoefu na wengine walitoka timu mbalimbali kubwa na walikuwa na uzoefu mkubwa, nilikuwa nafanya mazoezi na wakati huohuo najifunza.”
KOMBE LA NYERERE, WAPEWA YANGA
Matola anaendelea kusema wakati wanajiandaa na ligi walielezwa kuwa kuna kombe jipya limeanzishwa linaitwa Kombe la Nyerere ambalo kama timu ikiwa bingwa basi inakwenda kucheza Kombe la Shirikisho.
Anasema mfumo wa timu gani inacheza na nani, ulikuwa unapangwa kwa droo, wakati wanapanga Simba wakapangwa na Yanga kwenye mchezo wa kwanza, hali ilikuwa tofauti sana kwao baada ya droo ile.
“Huwezi kuamini droo ilipotoka tukawa tumepangwa na Yanga kila mtu alishtuka kwa kuwa Yanga walikuwa bora sana kipindi hicho, siyo bora tu yaani walikuwa sawa haswa, lakini kilichotupa moyo ni kwamba tulikuwa tumefanya usajili mzuri kipindi hicho tukawa na imani kuwa tunaweza kufanya vizuri.
“Kila timu ilikuwa inatakiwa kuchagua uwanja wake, sisi tulichagua Arusha, Sheikh Amri Abeid na Yanga walichagua Uwanja wa Taifa, sasa Uhuru, wakati huo Yanga walikuwa na mastaa kama Edibily Lunyamila, Peter Manyika, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, Ephraim Makoye, yaani walikuwa vizuri haswa nchi nzima gumzo lilikuwa Yanga tu.
“Mechi ya kwanza, ilikuwa Arusha, hatufahamu kocha alipatwa na nini siku hiyo, alibadilisha sana kikosi bila hata sababu, mastaa wengi hawakucheza nikiwemo mimi, lakini Mwanamtwa ambaye alikuwa namba mbili kwenye hiyo mechi kocha akampeleka namba sita, mechi ilimalizika tukachapwa bao 2-1 mabao ya Yanga yalifungwa na Aziz Hunter na Vincent Tendwa na lile la Simba lilifungwa na Ally Yussuf ‘Tigana’ pamoja na kwamba Yanga waliacha mastaa wao wengi Dar es Salaam lakini walitutawala haswa, walipiga pasi na walikosa nafasi kadhaa za wazi.
VURUGU ZAIBUKA KAMBINI, STAM AZICHAPA
Matola anasema baada ya mechi kumalizika wachezaji walikasirika sana, lakini pia baadhi ya mashabiki walikuwa wakali na kulalamika kuwa timu imehujumiwa.
“Kuna mwanachama mmoja kama sikosei alikuwa anaitwa Juma Mnonji alikuja kambini akatukana sana na kusema timu imehujumiwa, Mwanamtwa alikuwa siyo muoga akaanza kujibizana naye mwisho wakaanza kuzichapa nje ya hoteli, wakati watu wanaamua ugomvi huko, ndani zikaanza ngumi kati ya Amri Said ‘Jaap Stam’ na Ben Luoga watu wakaenda ndani pia kuamulia ugomvi.
“Hii ilionyesha kuwa watu walichukia sana kufungwa, hakuna aliyekuwa anaongea na mwenzake na tulianza kukata tamaa kuwa ndiyo basi tena hatuwezi kuibuka na ushindi Dar es Saalam wikiendi inayofuata, kumbuka wachezaji 20 ni wapya.
“Kesho yake asubuhi, tukaelekea Dar es Saalam lakini bado watu walikuwa na kinyongo sana wengine wakiendelea kutukana kwenye gari na wengine wakiwa kimya. Tulipofika Chalinze wakati tunakuja Dar, Mwanamtwa na Tigana wakasema hawaendi kwenye mechi hiyo na wanataka kushuka kwenye gari, wakamwambia dereva, akaweka gari pembeni wakachukua mabegi yao wakashuka sisi tukaendelea mbele.
Matola alipoulizwa nini kilitokea baada ya hapo alisema: “Unajua kipindi hicho siyo sawa na sasa, baada ya pale, alisimama Luoga kwa ujasiri mkubwa na kusema kuwa hakuna mtu yeyote kuwa na hofu, kila kitu kitaenda vizuri, lakini akamalizia kwa kusema kuwa mechi ya Dar lazima acheze na tutashinda.
WAINGIA UWANJANI, MASATU AKOSA PENALTI
Kocha huyo ambaye kwa sasa ni msaidizi Simba, anasema walijiandaa vizuri sana na mechi hiyo na walikuwa wanaamini kuwa lolote linaweza kutokea pamoja na kwamba Yanga walikuwa na mastaa wengi ambao waliwaacha Dar kwenye ule mchezo wa kwanza.
“Tulifika uwanjani, uwanja ulikuwa umejaa tele, mashabiki walikuwa wengi sana uwanjani, lakini tulishajiandaa kuwa lazima tupate ushindi kwenye mechi hiyo.
“Kumbuka mechi hii wengi tulianza wale ambao tulikosa nafasi kule Arusha, kocha akarudi kwenye mfumo sahihi nikapewa namba sita yangu, mapema tu baada ya mechi kuanza, tulipata penalti Yanga hawakuamini kwa kuwa walijiona wao ni wakubwa sana, penalti yetu alienda kupiga Masatu, tulikuwa tunamwamini kwa kuwa kwanza alikuwa na uzoefu sana na soka alikuwa analijua.
“Huwezi kuamini wakati anakwenda kupiga mashabiki walishanyayuka wakijua kuwa anafunga alikuwa mtaalamu sana wa penalti, Masatu alikosa mashabiki wote wakanywea na wa Yanga wakaamka na kuanza kushangilia.
“Yanga wakaendelea kutawala mchezo kwa kasi kubwa sana, mashabiki wetu wakatulia, ghafla Luoga akafunga bonge moja la bao matokeo yakawa 1-0, jumla 1-1 mechi ikamalizika, tukaenda kwenye matuta tukashinda 4-3, tukawatupa Yanga nje.
SIMBA WAPAGAWA
Matola anasema walipomaliza mechi hiyo kila mmoja alikuwa na furaha sana wakiwemo wale viongozi wa Friends Of Simba ambao walikuwa na timu wakati huo kwani kama wagefungwa basi mashabiki lazima wagewageukia, lakini ushindi ule ulikuwa wa furaha sana kwao.
“Unajua mechi ilikuwa na mashabiki wengi sana, tuliposhinda kila mmoja alichanganyikiwa kwa furaha kutokana na ukweli kwamba baada ya mchezo wa kwanza, timu iligawanyika sana, kila mmoja alifurahia baada ya mchezo na Yanga hawakuamini kwa kuwa walikuwa na kikosi imara sana kuliko sisi.
“Nakumbuka, sisi ilikuwa ngumu sana kufungwa kwa penalti kwenye kipindi chetu chote tulichocheza, tulikuwa na utamaduni wa kushinda kila mchezo tukiwa kwenye mikwaju ya penalti.
“Tulipofika kambini mashabiki walikuwa nje, nakumbuka viongozi walifurahi sana na kuzungumza nasi wakitueleza tumepambana sana, hapa ndiyo neema ya kucheza soka ilianza kuonekana tulikuwa hatukosi vijisenti kidogo tukishinda mchezo kama huu.”
Simba wamefanikiwa kuichapa Yanga, je unataka kufahamu nini kiliendelea? Fuatilia kwenye toleo la kesho.