Matola atumiwa nauli aingia mitini

MOJA ya makocha chipukizi wazawa ambao wanaaminika kuwa ni bora kwenye soka la Tanzania kwa sasa basi ni kocha msaidizi wa Simba Suleiman Matola ambaye amefanya mambo makubwa kadhaa kwenye soka la Tanzania.

Matola ambaye aliweka baadhi ya rekodi akiwa na Lipuli ya Iringa sehemu ambayo alitambulika sana, lakini pia akawa na Polisi Tanzania na kufanya tena mambo makubwa akiwa na Simba, siyo jina geni sana baada ya kukaa pia kwenye kikosi cha Simba kwa muda mrefu.

Amepitia mambo mengi akiwa na Simba, kuna wakati ameonja joto ya jiwe kutoka kwa mashabiki, kuna wakati ameshangiliwa na mashabiki haohao, hawa ndiyo watu wa soka, lakini katika maisha ya soka, Matola ana mambo mengi ambayo wengi hawayajui kwa kuwa siyo muongeaji sana na mara nyingi imekuwa ikielezwa kuwa ni mtu msiri sana kuhusu maisha yake ya nyuma ya soka.

Mwanaspoti huwa halishindwi, tumempata Matola na leo tunaanza safari ya makala kadhaa ambazo zitaeleza Matola ni nani na ametokea wapi, kuna mengi sana kumhusu ambayo huyafahamu, basi songa nasi;


NI ZAO LA UJIJI KIGOMA

Matola ni mzaliwa wa Ujiji Kigoma; “Nilinzia kucheza nikiwa darasa la nne mpira wa makaratasi, hivyo nafasi ambayo nilikuwa nakuta haina mtu ndiyo nilikuwa nacheza, isipokuwa kuwa kipa tu. Nilikuwa nasoma Shule ya Msingi Ujiji ni shule maarufu sana pale Kigoma.”

“Kigoma ukiwasikia mastaa wake, muulize alicheza kwenye uwanja gani, atakuambia lazima alipita Kawawa Stadium huu ni uwanja ambao umezalisha wachezaji wengi mastaa ambao wametoka Kigoma, ukiwataja wachezaji kama Said Sued, Makwa Suleimani, Hemed Maloboya na wengine wengi walitokea kwenye uwanja huu.“Mimi mtaani kwetu nilikuwa Kawawa Star ambayo ilikuwa inatumia uwanja huo, ilikuwa ni moja ya timu bora sana, tulikuwa tunashiriki makombe mengi. Ilikuwa inajaza wachezaji wengi mastaa wa Kigoma, kipindi hicho mimi nilikuwa nacheza beki namba mbili, nilikuwa bora, lakini siku moja tukiwa mazoezini akanifuata Maka kipindi hapo ameshastaafu soka awali alikuwa anaichezea Pamba ya Mwanza akaniambia kutokana na umbo langu sitakiwa kucheza beki wa pembeni niende namba sita.

“Nilipoanza kucheza hapo kila mmoja akawa ananisifia akiniambia kuwa ni sehemu ambayo inanifaa zaidi, unajua nilikuwa na umbo dogo na nilikuwa nacheza na wachezaji ambao wengine wanacheza ligi kuu, hivyo ilikuwa rahisi watu kuniona.”


MANYEMA NA MBANGA FC

Anasema baada ya muda iliazishwa timu inaitwa Mbanga FC na baadaye ikaanzishwa Manyema ambazo ziliendelea kuleta upinzani Kigoma.

“Baadaye zilianza timu nyingi, lakini viwanja vikiwa hakuna, nakumbuka mwaka 1993, tulicheza Ligi Daraja la Nne, tukiwa kundi moja pamoja na timu inaitwa Nation, lakini wakati tunatafuta nafasi ya kwenda daraja la tatu tukashindwa kupanda wenzetu Nation wakapanda.

“Siku moja baada ya Nation kupanda, kocha wao alikuwa anaitwa Shaaban Msafiri ambaye aliwahi kuichezea RTC ya Kigoma akanitaka, nilipata nafasi kikosi cha kwanza nikiwa nacheza namba sita, tukafanikiwa kufuzu kwenda Kanda Tabora.

“Hii ilikuwa safari yangu ya kwanza kwa ajili ya soka, kule tulishika nafasi ya pili, tukaenda Daraja la Pili kituo chetu kikapangwa Kigoma, kilichotusaidia tulikuwa wapambanaji, kila mechi tulikuwa tunajitoa haswa, tulifanikiwa kufuzu sisi na Toto African.


ATUMIWA NAULI YA TOTO, AINGIA MITINI

Matola anasema pamoja na kwamba Nation walipanda daraja sawa na Toto, lakini vijana hao wa Mwanza walimtaka na kocha wao kipindi hicho alikuwa anaitwa Choki Abedi moja kati ya makocha ambao Matola anasema walikuwa bora sana kipindi hicho.

“Toto walinifuata nikawaambia hakuna shida, basi wakasema wanaenda Mwanza halafu watatuma nauli kwenye basi. Kipindi hicho kulikuwa hakuna simu za mkononi, pale jirani kwetu kulikuwa na mzee mmoja ana simu ya mezani, nikawapa namba ya pale ili wakituma nauli wanieleze niende Mwanza.

Siku moja nikiwa nimekaa nyumbani na mama yangu, kwanza unajua mimi kwetu ndiye nimekaa na mama muda mrefu wengine walikuwa wameshatoka Kigoma na wengine wapo kwa ndugu, tukiwa tumekaa nje akaja mtoto kutoka jirani akaniambia simu yangu itapigwa saa nane mchana, basi muda ulipofika nikaenda kwa jirani, nikapigiwa simu na kuelezwa kuwa nauli imetumwa kwenye basi.

“Nikaenda kituoni, nakumbuka nilipewa shilingi 20,000, kwa wakati huo ilikuwa nyingi sana. Huwezi kuamini, nilichukua ile hela nikaila, sikwenda Mwanza wala wapi, nikaendelea na mazoezi kwenye timu yangu ya Nation kwa ajili ya kwenda kwenye kituo Shinyanga.

“Nilijiuliza mambo mengi sana, niende Mwanza kuichezea Toto, wakati timu yangu nayo ipo kwenye mashindano hayo hayo, nikaona haiwezekani, wakawa wakipiga simu siendi kuongea nao, mwisho wakakaa kimya.

“Bahati mbaya, tukapangwa kwenye kituo kimoja na Toto, Shinyanga, jaribu kujiuliza hali inakuwaje, watu umekula hela yao, simu zao hujapokea halafu mnakutana kwenye kituo cha kazi.

“Bahati nzuri sisi tulianza kucheza kabla yao, siku ya mchezo mchana wake, viongozi wa Toto wakiwa pamoja na Choki, wakawafuata viongozi wa timu yangu wakawaambia waniambie nirudishe hela yao haraka, vinginevyo nitakoma, wakawaeleza viongozi mkanda mzima ulivyokuwa.

“Kwenye timu yetu kulikuwa na viongozi wengine jasiri sana, kulikuwa na mzee mmoja anaitwa Mbayo Simba, akaniita na kuniambia nisiogope, nicheze mpira hakuna mtu atakayenigusa, huo ulikuwa muda mfupi kabla ya kuanza mechi yetu na Maji Mara, nikiangalia jukwaani nawaona viongozi na wachezaji wa Toto wamekaa wanaangalia mechi.”

“Kutokana na kiwango cha juu ambacho nilikionyesha baada ya mechi kumalizika, niliwaona wale viongozi wa Toto wamekaa kikao pembeni wanaongea, baadaye wakashauriana kuachana na suala la kunidai hela yao, Choki akaja akaniambia kuwa ligi ikimalizika anataka kuongea nami pamoja na viongozi wao, nikamjibu poa nikaondoka.


BOSI ASAFIRI KUMFUATA KIGOMA

Matola anasema; “Nilirudi Kigoma na Nation lakini siku moja akaja kiongozi kutoka Mwanza akiwa ameshakata tiketi na hela ya kula njiani anayo anakaniambia natakiwa Mwanza kujiunga na Toto, unajua mama alikuwa amenizoea sana, ikawa ngumu kumuaga, lakini nilipomweleza kwa undani akanielewa nikaondoka na yule jamaa kwenda Mwanza kujiunga na Toto.”


ASAJILIWA KWA LAKI, AKOSA NAMBA

“Nilisaini mkataba nakumbuka walinipa laki moja kama fedha ya usajili, ilikuwa hela nyingi huu ulikuwa mwaka 1998 na ndiyo ilikuwa fedha yangu kubwa ya soka.

“Lakini nilipokwenda mazoezini siku ya kwanza nikakutana na changamoto, mimi nilikuwa natakiwa kucheza namba sita, pale kwenye ile nafasi nilimkuta nahodha kipindi hicho wa Toto anaitwa Kasa Mrisho, jamaa alikuwa anajua sana.

“Nikaona naweza kukosa nafasi ya kucheza nikahamia namba nane, nikacheza nafasi hiyo kwa kipindi kifupi sana, kocha akanibadilisha akaniambia nicheza namba nne, nikarudi na kucheza huku nyuma, nilionyesha uwezo mkubwa sana kwenye nafasi hiyo, kila mmoja akawa ananipa sifa, tulikuwa kwenye hatua ya mwisho sana wakati wa kupanda daraja kwenda Ligi Kuu Bara kituo kikiwa Musoma.

“Nakumbuka kwenye pointi tulikuwa na nafasi ya kupanda daraja, lakini kulikuwa na kesi mahakamani walifungua Coastal, mwisho tulisikilizia na hawatukupata nafasi, tukarudi zetu Mwanza wakati huo ligi zote zimesimama.


ATUA NYAMAGANA, ATIMKIA KAGERA USIKU

“Ukienda Mwanza hata leo, uwanja maarufu kwa soka ni Nyamagana pamoja na uwepo wa CCM Kirumba, pale utawakuta mashabiki na utawakuta wachezaji wa kila aina, wakati nacheza nilikuwa naambiwa kuhusu uwanja huu.

“Basi tulipomaliza ligi tukawa tupo mapumzikoni Mwanza na Ligi Kuu pia hakuna hivyo wachezaji wengi mastaa wakawa wapo Mwanza. Nikawa nami naenda pale nafanya mazoezi, kwanza halikuwa jambo rahisi kupata nafasi ya mazoezi lakini kwa kuwa nilikuwa na uwezo niliweza kupenya kirahisi nikawa nafanya mazoezi na mastaa wengine, nakumbuka Pamba walinifuata, wakati huo walikuwa wapinzani wakubwa wa Toto, lakini sikupenda kwenda kwao.

“Kwa ukanda huo timu bora zaidi ilikuwa Kagera Star, kwanza jamaa walikuwa na fedha na walikuwa na mastaa wengi wakubwa na ilikuwa ligi kuu, siku moja kiongozi wa Kagera akawa amekuja Mwanza kwa ajili ya kuwachukua wachezaji wawili wa Toto, Hamis Kipinga huyu alikuwa kipa na Abuu Amran ‘Papaa’, yule kiongozi alipokuja alikutana na Choki na kuongea naye.

“Choki akamuuliza, kwanini usimchukue na Matola? jamaa akamuuliza anacheza namba ngapi, akajibiwa namba sita, nane na nne akamwambia nafasi hizo tayari zina watu hivyo hawataki kuongeza mchezaji mwingine.

“Yule jamaa alitakiwa kuondoka Mwanza saa mbili usiku kwenda Kagera, jioni akaja kuangalia mazoezi pale Nyamagana akiwa na Choki nikiwa uwanjani nafanya mazoezi, akaniona na kuniulizia, Choki akamwambia yule ndiye Matola ambaye nilikuwa nakuambia, akasema ni bora kuliko wale waliopo kule klabu kwake.

“Akatoka nje akapiga simu kwa mabosi wake akawaambia kuna mtu anaitwa Matola, wakamwambia aende nami, mimi nikiwa uwanjani nacheza, baada ya mazoezi kumalizika jamaa akiwa na Choki wakanifuata na kuniambia natakiwa kwenda Kagera usiku huo.

“Sikupinga kwa kuwa kwanza ilikuwa timu bora na ilikuwa inacheza ligi kuu, nikaenda nikaoga na kuondoka na huyu jamaa saa mbili kwenda Kagera, nakumbuka nilifika asubuhi, nikaenda kwa kiongozi tukaongea akanipa 150,000, nikasaini mkataba.


KOCHA KAGERA AMSHANGAA

“Siku ya kwanza nilipokwenda mazoezini, kocha msaidizi pale alikuwa anaitwa Nkama Ntare, alinishangaa sana kwa kuwa nilikuwa mdogo kiumbo, akaniita na kuongea nami lakini nilifahamu tu kuwa alikuwa amepata wasiwasi kama nitaweza.

“Pale kulikuwa na wachezaji maarufu kama Amosi Kiggi na Pascal Mayala ambao walikuwa na heshima kubwa wakati huo, nilipofanya mazoezini baada ya wiki moja yule kocha aliniita na kunieleza kuwa mwanzo alikuwa na wasiwasi nami lakini ameshangazwa na uwezo wangu ni wa juu.

“Lakini kabla ligi haijaanza bado nilikosa nafasi ya kuanza kwa kuwa katikati kulikuwa na watu haswa, nakumbuka siku moja nikiwa mazoezini tulikuwa na beki mmoja anaitwa Issa Ally alikuwa mkubwa kuliko mimi, alikuwa anacheza namba mbili, akanifuata akaniambia wewe unauwezo mkubwa lakini hapo katikati huwezi kucheza, anza kucheza namba mbili mazoezini, halafu mimi nitakupisha hapa nitaenda namba tatu, wewe utapambana hapa najua waliopo utawazidi tu.

“Basi kesho yake nikamwambia kocha nataka kucheza namba mbili, kocha akaniambia sawa, nikamwona braza kaenda namba tatu, nilipocheza hapa kwa muda mfupi tu, nikaanza kuonyesha upinzani wa hali ya juu sana.

“Wiki moja mbele ligi ilikuwa inatakiwa kuanza na mechi yetu ya kwanza dhidi ya Simba, nilikuwa nawania namba mbili na beki mmoja alikuwa anaitwa Mkamwa jina la kwanza nimesahau, basi siku ya mechi ya Simba hadi saa nne asubuhi listi ilikuwa bado haijatoka kila mtu alikuwa anasubiri kuona nani ataanza kwenye eneo letu.

“Tukiwa nje tumekaa tunapiga stori akaja nahodha wetu alikuwa anaitwa Shaaban Kalonda akanitania kwa kusema nimezuia listi utata huko ndani ni nani aanze kwenye nafasi yetu, watu wakacheka, saa sita mchana listi ikatajwa nikaanzia nje, kwanza nilishukuru kwa kuwa aliyeanza kucheza alikuwa mzoefu sana.

“Kipindi cha pili, yule jamaa aliyeanza namba mbili alionekana kuchemka na nikaambiwa niingie, nilipoingia nilipania nikasema nataka kuwashangaza watu, nilicheza vizuri kwenye mechi hiyo nakumbuka tulitoka sare, michezo iliyofuata yote nikaanza, tulicheza na Pamba, tukacheza nafikiri ilikuwa timu moja pale Dodoma zote nikawa naanza, shida ikaja kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar.” “Tulipokwenda Manungu tulichapwa mabao 3-0, makosa mengi yakatokea kwenye beki wa kati, baada ya mechi wachezaji waliokuwa wananifahamu wakamfuata kocha na kumwambia mrudishe Matola pale katikati atatusaidia sana.

“Kocha akanifuata akaniuliza unaweza kucheza katikati nikamwambia ndiyo sehemu yangu muhimu, basi mechi iliyofuata ilikuwa dhidi ya Reli nikacheza namba nne, nikaupiga mwingi, mchezo huo nakumbuka wachezaji wetu watatu walipewa redi kadi hivyo kazi ikawa ngumu sana kule nyuma tukawa tunaokoa tu muda wote.

“Nakumbuka Reli walikuwa na mshambuliaji wao maarufu sana alikuwa anaitwa Clement Bazo nilimkaba baadaye akaona isiwe shida akanipiga ngumi, nikatibiwa nikarudi uwanjani, hii mechi ilipigwa Morogoro ikaisha 0-0, baada ya mchezo kumalizika mashabiki wa Morogoro walinichangia fedha wakanipa kama pongezi, tulipambana na mechi yetu ya mwisho ya msimu nakumbuka ilikuwa dhidi ya Yanga.


RAUL SHUNGU, KITWANA MANARA WAMFUATA

“Nakumbuka tukiwa kwenye mechi dhidi ya Yanga nilicheza kwa kujituma sana, wakati huo alikuwepo kocha wa Yanga, Raul Shungu baada ya mechi akiwa na Kitwana Manara ambaye alikuwa mmoja wa viongozi kwenye timu, baada ya mchezo kumalizika walinichukua tukaenda hotelini kwao.

“Wakanieleza kuwa wameshazungumza na Francis Kifukwe wanataka kunisajili, sasa timu ilikuwa inaelekea Tabora kumalizia mechi ya mwisho ya msimu wakasema nikienda kule nitakutana na mtu atanipa nauli baada ya mechi niende Dar es Salaam kujiunga na kambi ya Yanga, wakanipa namba wakaondoka zao.

“Nilijishangaa kwanza, kwa kuwa niliona napanda kwa kasi sana, halafu bado sikuwa mkubwa kiivyo, siku ya kuondoka ikafika asubuhi nikawa tunatakiwa kwenda Tabora kwenye mechi yetu ya mwisho ya ligi dhidi ya Milambo, hatukuwa na presha kwa kuwa tulishakusanya pointi za kutosha.”


Sasa kumbe bwana Matola alipotelea kwenye treni...unajua ilikuwaje. Usikose kesho.