Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MATOLA - 3 : Simba yafyeka wachezaji 20

KATIKA mfululizo wa makala hii maalumu ilitokana na mahojiano na nyota wa zamani wa Simba aliye kocha msaidizi wa timu huyo, Seleman Matola na kuona namna alivyosajiliwa kwa Sh 100,000 huku akichunuwa na aliyekuwa Katibu Mkuu, Kassim Dewji ‘KD’.

Leo tunaendelea na Matola akieleza namna mabosi wa klabu hiyo walivyofyeka wachezaji 20 akiwamo kipa mkongwe, Mohammed Mwameja na straika Emmanuel Gabriel ‘Batgol’ na jinsi kundi la Friends of Simba lilivyoibuka na kuiteka timu. Tiririka naye...!


TIMU YAKIMBILIA MOMBASA

Anaendelea kusema baada ya kufanya mazoezi kwa wiki moja, viongozi walienda mazoezini na kuwaeleza timu inatakiwa kwenda Mombasa kwa ajili ya kambi ya kujiandaa na ligi.

“Hii ilikuwa safari yangu ya kwanza kwenda Mombasa, tulijiandaa na timu ikaondoka na mastaa wake wote kwenda Kenya ambapo nakumbuka tulicheza michezo miwili ya kirafiki, mchezo wa kwanza tulicheza na Bandari, kwenye mechi hii nilianza lakini nikachezeshwa namba 2, mechi ilimalizika nafikiri tulishinda mabao 3-0, lakini wachezaji wakongwe wa Simba walinisifu sana pamoja na kwamba sikucheza kwenye nafasi yangu, nakumbuka mechi ya pili tena nilianza nikacheza namba tatu, tukatoka sare ya 0-0.


FRIENDS OF SIMBA YAITEKA

Anasema baada ya kurudi Dar es Salaam wachezaji wanaotoka mkoani wengi walitakiwa kurudi kwenye ile Lodge lakini wale wa Dar es Salaam walitakiwa kuendelea kwenda nyumbani na kuja mazoezini asubuhi na jioni.

“Tuliporudi Dar shida ndiyo ilianza rasmi sasa na nikafahamu ukubwa wa Simba, hayo mambo huko nyuma nilikuwa sijayaona, kundi la Friends of Simba ndiyo lilikuwa limeanza na walikuwa wanaitaka timu kwa madai kuwa haiwezi kufanya vizuri kama haitakuwa mikononi mwao.

“Tukiwa kambini tumekaa alikuja nahodha wetu wa kipindi hicho alikuwa anaitwa Musa Msangi, alikuwa mchezaji ambaye tunamsikiliza sana kwa kuwa alikuwa mkongwe na mara nyingi alikuwa anaweza kutusaidia hata kutatua shida zetu, akatuambia kuwa Friends wanaitaka timu na kila mchezaji anatakiwa kufunga begi lake, gari litakuja kutuchukua tuende hoteli nyingine.

“Tulikuwa wachezaji wengi akiwemo Doyi Moke, Kimuna Mwita, Omar Hussein, Patrick Betwel, Said Maulid, na wengine wengi, tukaweka mabegi yetu tayari kwa siri, baada ya muda ikaja Coaster na kutuchukua mpaka hoteli moja tukaenda City Ambassador Hoteli tukawakuta viongozi wa Friends wamekaa pale wanatusubiri.

Tuliwakuta viongozi wengi wa kundi hilo kama Juma Salum, Juma Nkamia, Mulam Mngwabi na hata Kassim alikuwepo, tulipofika pale tukawakuta na wachezaji wengine ambao hawapo kambini wapo pale, wakasema timu ipo chini yao kuanzia muda huo na itaondoka usiku kwenda Morogoro kuweka kambi.


WATUA MORO, KOCHA AGOMA

Matola anasema baada ya kukaa pale hotelini kwa muda, giza liliingia na wakaanza safari ya kwenda Morogoro ambapo walitakiwa kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na ligi, lakini kocha wao mkuu aligoma kwenda kwa kuwa alikuwa upande wa viongozi waliokuwa madarakani.

“Tulipofika Morogoro tuliwakuta Friends wengine kule, alikuwepo kiongozi mmoja nakumbuka alikuwa anaitwa Shaaban Mnyaa na mwingine alikuwa anaitwa Hassan Bantu, hawa ndiyo walitupokea pale na kutupeleka hotelini, lakini kumbuka kuwa hapo kocha Nzoyisaba hayupo na timu kwa kuwa aligoma kuwapa ushirikiano Friends na kusema kuwa anaunga mkono uongozi wa Simba uliopo madarakani.

“Tukiwa pale hotelini tulitangaziwa kuwa sasa timu ipo chini ya Amri Ibrahim, tulifanya mazoezi chini yake kwa wiki moja tukacheza mechi ya kwanza ya kirafiki nilicheza namba sita kwenye mchezo huo kwa kuwa kocha alikuwa ameniona vizuri mazoezini sikumbuki tulicheza na timu gani, lakini tulishinda.


NZOYISABA AIBUKIA KAMBINI

Matola anasema baada ya mechi ile, Nzoyisaba aliibuka kambini na kufanya kikao na wachezaji ambapo alichimba mkwara mzito sana huku akionekana kuwa na hasira.

“Tulipoimaliza mchezo na kurudi kambini, nakumbuka tulifika tukamkuta kocha amefika na akataka kukaa na wachezaji wote na kuongea nao, tulikubali tukaenda ukumbini, akaja akaongea sana lakini akasema kama kuna mtu anafikiri hawezi mazoezi yake bora aondoke mapema kwa kuwa anataka watu wa kazi, huyu kocha alikuwa anajua sana na mazoezi yake yalikuwa magumu haswa ni wachache walikuwa wanaweza kuhimili.

Tulifanya mazoezi magumu sana kwa wiki moja chini ya Nzoyisaba, nafikiri kwenye kipindi nacheza hapa ndiyo nilikutana na mziki, baada ya mazoezi ya wiki moja tulicheza mechi ya kirafiki na CDA ya Dodoma.

“Kocha aliwaweka wachezaji wengi mastaa nje, mimi mwenyewe niliwekwa nje, mwisho tulichapwa mabao 3-0, viongozi walichukia sana kwa kuwa baada ya kuichukua timu mashabiki waliamini itakuwa inashinda tu, lakini ambacho niligundua ni kwamba walikuwa hawamuamini kocha, walihisi kama anawahujumu.

“Kesho yake tukiwa mazoezini uwanja wa Veta lilikuwa gari la uhamiaji akashuka mtu mmoja na kwenda moja kwa moja kwa Nzoyisaba wakamchukua na kuondoka naye hadi Dar, kesho yake tukaambiwa amepewa kesi ya kufanya kazi nchini bila kibali, akapandishwa mahakamani akakubali kosa, akapigwa faini na kupelekwa kwao Burundi, tulihisi kama vile kuna mchezo ulichezwa.


SIMBA YAMNYAKUA KIBADENI

Baada ya kocha wao kuondoka, timu ilirudi tena Ibrahim yule ambaye alianza nao kambi, baada ya kukaa kwa wiki moja, timu ya Kajumulo ambayo ilikuwa Brazil kwenye kambi ya maandalizi ya ligi ilirejea nchini.

“Kajumulo kipindi hicho ilikuwa timu haswa, baada ya siku chacha tulisikia kuwa wamerudi kutoka Brazil, Friends wakati huo walikuwa na ushawishi mkubwa sana, wakamchukua kocha wao Abadallah Kibadeni ambaye alikuja na mfumo ulikuwa unaitwa Horizonto Brazil.

“Tulifanya mazoezi vizuri ligi ikawa inaanza wiki moja mbele lakini Kibaden alitusaidia sana kwa kuwa alikuwa mmoja kati ya makocha wenye uwezo wa juu sana. tulienda kwenye mechi ya kwanza ya ligi tulicheza na Lipuli nikaanza namba sita, tukashinda mabao 6-0, tuliendelea kushinda nyingi nyingi, lakini mwisho hatukufanikiwa kupata nafasi ya kimataifa, bingwa alikuwa Yanga, nafasi ya pili Kajumulo sisi tukamaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo.