Mastaa Tanzania Prisons hawana muda kabisa
Muktasari:
- Prisons ilishuka daraja msimu uliopita kupitia play off baada ya kudumu Ligi Kuu miaka 15 na sasa wanashiriki Championship ambapo wamekuwa na matokeo mazuri wakiwa nafasi ya pili kwa pointi 16 baada ya mechi nane wakizidiwa mbili na vinara KMC.
‘TUNARUDI’. Ni kauli ya nyota wa Tanzania Prisons wakichekelea matokeo waliyonayo kwenye Championship wakiiota Ligi Kuu msimu ujao, huku wakitoa tahadhari kwa wapinzani wa ligi hiyo.
Prisons ilishuka daraja msimu uliopita kupitia play off baada ya kudumu Ligi Kuu miaka 15 na sasa wanashiriki Championship ambapo wamekuwa na matokeo mazuri wakiwa nafasi ya pili kwa pointi 16 baada ya mechi nane wakizidiwa mbili na vinara KMC.
Timu hiyo inatarajia kuwa kibaruani kesho Jumamosi kuwakabili IAA ya jijini Arusha, huku ikijivunia matokeo ya ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya TMA katika mchezo uliopigwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Nahodha wa timu hiyo, Lambart Sabiyanka amesema wanafahamu ugumu ulivyo kwenye ligi hiyo akieleza kuwa bado hawajafikia malengo kwa mechi nane walizocheza licha ya nafasi waliyopo.
Amesema hesabu zao ni kumaliza kileleni mzunguko wa kwanza na pengo la pointi nyingi dhidi ya wapinzani, hivyo nguvu na akili ni kutafuta pointi tatu kila mchezo ukiwamo dhidi ya IAA utakaopigwa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
“Tunataka kurudi, hivyo ili kufikia malengo lazima tushinde kila mchezo, hatupo pabaya lakini hatujafikia malengo yetu kwakuwa tunahitaji raundi ya kwanza tuwe kileleni kwa pengo kubwa la pointi dhidi ya wapinzani” amesema Sabiyanka.
Kwa upande wake kinara wa mabao kikosini, Oscar Paul ambaye juzi alifunga mabao matatu ‘Hatitriki’, amesema kiu yake ni kuona anairudisha Prisons Ligi Kuu na kuwania kiatu cha mfungaji bora.
“Nashukuru kwa mwenendo mzuri wa matokeo, kikubwa ni kuipambania timu kuhakikisha tunafikia malengo yetu, lolote linawezekana kwakuwa ligi haijaisha” amesema nyota huyo mwenye mabao manne.