Mashami alitaja tatizo Dodoma Jiji
Muktasari:
- Amesema wakati wakijiandaa na mwendelezo wa ligi hiyo, anahitaji ushirikiano wa wenzake kwenye benchi na uongozi akiahidi kuboresha eneo la ushambuliaji na kusahihisha makosa safu ya ulinzi ili kufikia malengo.
POINTI moja waliyovuna mechi mbili za ugenini imeonekana kumvuruga Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Vicent Mashami, akieleza kuwa ipo kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha timu hiyo inabadilika haraka.
Amesema wakati wakijiandaa na mwendelezo wa ligi hiyo, anahitaji ushirikiano wa wenzake kwenye benchi na uongozi akiahidi kuboresha eneo la ushambuliaji na kusahihisha makosa safu ya ulinzi ili kufikia malengo.
“Yapo makosa binafsi kwa wachezaji, lakini wanakosa maamuzi ya haraka wanapofika kwenye goli la wapinzani, lazima nifanyie kazi maeneo yao na ili kufikia malengo lazima tuwe na ushirikiano wa pamoja,” amesema kocha huyo.
Dodoma Jiji ambayo msimu uliopita ilionesha kiwango bora ikizisimamisha timu kubwa nchini za Simba na Yanga, msimu huu imeanza kwa kuchechemea, ikivuna pointi moja kwenye mechi mbili.
Akizungumza jijini Mbeya, Mashami amesema matokeo hayo si mazuri sana kwao kwani hesabu na mipango yao ilikuwa ni kuvuna pointi sita akikiri ugumu wa michezo ya ugenini kwa wenyeji kujipanga kushinda kwao.
Amesema kwa sasa akili zote zinahamia mechi ijayo dhidi ya Polisi Tanzania watakayocheza nyumbani jijini Dodoma, akieleza kuwa wanahitaji ushindi ili kuianza rasmi Ligi Kuu msimu huu 2026-2027.
“Ligi imeanza kwa ugumu na timu zinajipanga zaidi kushinda nyumbani, pointi moja katika mechi mbili si matokeo mazuri sana badala yake lazima tujipange upya kuanzia mechi ijayo tuanze upya msimu,” amesema Mashami.
Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Rwanda, Polisi Rwanda na APR FC, ameongeza kuwa licha ya matokeo hayo, lakini ameridhishwa na kiwango cha nyota wake japokuwa yapo makosa binafsi wanafanya.
Aliahidi kuwa ubora ulioonekana msimu uliopita utaendelea kuwapo msimu huu kwa kuwa anaendelea kusuka kikosi na kutengeneza muunganiko bora.