Prime
Manqoba ataja njia ya kufuzu CAFCL
KOCHA Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi amesema mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United hakuwa mgumu na sasa wana kazi ya kutumia uwanjani wa nyumbani ili kufuzu hatua inayofuata.
Yanga ikiwa Botswana wikiendi iliyopita kwenye mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika iliambulia sare ya bao 1-1, huku ikisawazisha mwishoni kabisa kupitia kwa mshambuliaji wake mpya Selemani Mwalimu.
Awali mashabiki waliamiani kuwa Yanga ilikuwa na nafasi kubwa ya kupata ushindi kutokana na ubora wa kikosi chao na usajili ambao timu hiyo imefanya lakini mambo yakawa magumu pamoja na kwamba timu hiyo ilitawala mchezo kwa dakika zote tisini.
Akizungumza baada ya timu hiyo kurejea jijini Dar es Salaam, kocha huyo raia wa Afrika Kusini amesema kuna mambo kadhaa yalisababisha mchezo huo kumalizika kwa sare lakini suala kwamba ulikuwa mgumu siyo kweli na sasa wana kazi ya kuhakikisha wanapata ushindi Jumamosi.
“Mechi haikuwa ngumu, ni sahihi kusema hivyo, naamini kuna mambo yalisababisha matokeo yale, kwanza uwanjani ulikuwa mbaya, haukuwa unaruhusu mpira kutembea, jambo la pili hali ya hewa haikuwa rafiki kwetu kulikuwa na upepo mkali na baridi ya kiwango cha juu.
“Sasa tumerejea nyumbani na kazi yetu ni kuhakikisha timu inafuzu kwenda hatua inayofuata, tunakwenda kuhakikisha tunashambulia kwa nguvu kubwa, lakini pia kumfanya mpinzani wetu afanye makosa ili tuyatumie na kupata ushindi kwenye mechi inayofuata mbele ya mashabiki wetu,” amesema kocha huyo ambaye tayari ameshatwaa Ngao ya Jamii tangu alipojiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu.
Yanga itarejea kwenye Uwanja wa Azam Complex Jumamosi ijayo kwa ajili ya mchezo huo ambao mashabiki wanausubiri kwa hamu kubwa kuona kile ambacho mastaa wao wanaweza kukifanya ndani ya dakika tisini.
Timu hiyo ambayo haijapoteza mchezo wowote wa mashindano kati ya saba ambayo imecheza kuanzia imekuwa chini ya Mngqithi, imeshinda mchezo mmoja wa Ngao dhidi ya Simba, mitano ya Ligi Kuu ya NBC pamoja na kutoka sare kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Gaborone.
Yanga kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Habari Ally Kamwe imeshasema kuwa mchezo wa Jumamosi ni maalumu kwa ajili ya staa wao Selemani Mwalimu ambaye alifunga bao pekee kwenye mchezo uliopita, tayari huku nyuma Yanga imewahi kuitambulisha michezo kadhaa kama maalumu kwa wachezaji wake akiwemo Djigui Diarra, Ibrahim Bacca, Clement Mzize pamoja na Pacome Zouazoa.
Endapo Yanga ikipita kwenye hatua hii itakutana na mshindi kati ya CFFA ya Madagascar au Lijabatho FC ya Lesotho, katika mchezo wao wa kwanza CFFA ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani, huku ikionekana kuwa moja kati ya timu yenye safu nzuri ya ushambuliaji.