Manji arejea na shangwe Yanga
Muktasari:
Manji akiwa madarakani Yanga walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu mfululizo kuanzia 2014-15 hadi 2016-17.
SHANGWE la mashabiki wa Yanga mitandaoni ni kwamba; “Chuma kimerudi”. Hizo ndio tambo zao baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wao, Yusuf Manji kurejea nchini kimyakimya.
Manji amerejea nchini kimyakimya ambapo Mwanaspoti linajua baada ya kufika kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, alihojiwa kwa muda na Takukuru. Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni alithibitisha kuwa walimhoji jana.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba vyombo hivyo vilikuwa vikitaka kujua kuhusiana na mambo mbalimbali ambayo Manji aliyaacha wakati anaondoka nchini ikiwamo ishu zake na Yanga.
Habari zinasema kwamba Manji aliwaeleza vigogo wa Yanga kwamba akishaweka ishu zake sawa ataangalia namna nzuri ya kurejea klabuni hapo kama muwekezaji.
Manji ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Yanga akiiongoza timu hiyo kuwa na ushindani mkubwa anatua ikiwa zimepita siku chache tangu kijana wake wa kiume Mehboub Manji naye kuja nchini ingawa baadaye naye aliondoka ndani ya siku chache.
Baada ya kuiongoza Yanga kuwa na ushindani bora, Manji alifikia uamuzi wa kujiuzulu Yanga Mei 22, 2017 akiona inatosha kwake kuiongoza klabu hiyo akimuachia nafasi hiyo aliyekuwa makamu wake Mhandisi Clement Sanga.
Hata hivyo, uamuzi huo wa Manji haukukubalika kwa wanachama na mashabiki wa timu hiyo na hata viongozi ambapo waliugomea na kumtaka arejee lakini baadaye alizuiwa na Yanga kutakiwa kufanya uchaguzi kupata viongozi wapya.
Jana mara baada ya taarifa za ujio wa Manji ambaye pia ni mfanyabiashara mkubwa kuenea, zilionekana kupokewa kwa furaha na wanachama na mashabiki wa Yanga wakisambaza taarifa hizo katika kurasa za mitandao ya kijamii wakiwakebehi Simba kwamba wakae mkao wa maumivu kwavile msimu ujao furaha inahamia jangwani.
Kurejea kwa Manji kunakuja siku chache tangu uongozi wa Yanga kutangaza Juni 27 kuwa na Mkutano Mkuu wa klabu hiyo ukiwa ni mkutano wa kwanza katika utawala wa mwenyekiti Dk Mshindo Msolla ambao pia huenda ukawa na ajenda ya mabadiliko ya kubadilisha mfumo wa uendeshaji.
Akizungumza na gazeti hili Mwenyekiti wa viongozi wa Matawi ya wanachama wa Yanga jijini Dar es Salaam, Shabaan Udah amesema wamesikia taarifa hizo ingawa hawana uhakika lakini zimewafariji na kuwafurahisha.
Udah alisema wako tayari kumkaribisha Manji hata katika mkutano wao mkuu kwa kuwa bado ni mwanachama wa klabu yao lakini pia akiwa amefanya mambo makubwa katika maisha ya Yanga.
“Nimeziona tu hizo taarifa katika mitandao sina uhakika lakini niseme binafsi nimefarijika kusikia amekuja na yuko salama kwa kuwa yule ni mwenzetu ndani ya klabu hii,” alisema Udah.
“Manji amefanya makubwa ndani ya hii klabu, naweza kusema ni kipenzi cha Wanayanga wengi ambao kama umeona wamekuwa wakifurahia kusikia amekuja tangu jana (juzi), ikiwa kama kweli amekuja tumefarijika na tunamuombea akipata nafasi basi aje kutujulia hali wenzake.
“Tuna Mkutano Mkuu kama ataona ana nafasi basi hatutasita kumkaribisha, tunachofanya sasa pia naye ni kiu yake aliyokuwa anataka kuifanya katika haya mabadiliko, tunamkaribisha aje tuungane naye kuendeleza mazuri ya Yanga na klabu anayoipenda,” alisema.
Manji enzi zake alisajili mastaa wakubwa ndani ya Yanga huku akiiwezesha kushindana kiuchumi na kuwa na uwezo wa kutamba popote.
WAWILI WATUA FASTA
Wakati mashabiki wakiwa na furaha ya bilionea wao wa zamani kurejea nchini, habari za ndani kutoka Yanga zinasema wachezaji wawili, winga Dickson Ambundo na beki wa kulia kutoka DR Congo, Djuma Shaaban wamemalizana na mabosi wa Jangwani ili kukipiga kikosini hapo kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.
Shaaban ni beki wa kulia aliyekuwa akitajwa pia kuwindwa na Simba, lakini mabosi wao waliamua kuachana naye kutokana na kumuongezea mkataba mpya, beki wake wa, Shomary Kapombe, huku Ambundo anayekipiga Dodoma Jiji, akinyakuliwa kuwa pacha wa Tuisila Kisinda.