Manduta asaini mmoja Uturuki
Muktasari:
- Kiungo huyo anajiunga na Antalya inayoshiriki ligi kuu nchini Uturuki, baada ya mipango yake ya kwenda Lithuania kukwama kutokana na changamoto ya VISA.
KIUNGO mshambuliaji wa Tanzania, Nasma Manduta amesaini mkataba wa mwaka mmoja katika klabu ya Antalya Spor ya Uturuki akitokea Ceasiaa Queens ya Iringa.
Kiungo huyo anajiunga na Antalya inayoshiriki ligi kuu nchini Uturuki, baada ya mipango yake ya kwenda Lithuania kukwama kutokana na changamoto ya VISA.
Akizungumza na Mwanaspoti Meneja wa mchezaji huyo, Mustafa Mtupa amesema awali walikuwa wamepata timu nchini Lithuania, lakini mpango huo ukakwama baada ya kupata changamoto ya visa iliyozuia safari yake kukamilika kwa wakati.
"Tulipata timu Lithuania kukawa na shida ya visa, ikabidi tukaombe Afrika Kusini. Timu ikaandaa barua kama mara mbili, haijajibiwa," amesema Mtupa.
"Tukafanya mpango aende Ghana ili tujaribu, lakini gharama ikawa kubwa," amesema Mtupa
Mtupa ameongeza kuwa njia rahisi ilikuwa kumpeleka akacheze Uturuki na hapo ndipo itakuwa nafuu ya kwenda Lithunia ambako anadai wana fedha ndefu.
"Kuna timu Antalya iko Uturuki, yuko na mkataba binafsi. Kwa hiyo amesaini mwaka mmoja lakini anaweza asimalize haitakuwa ngumu, ni rahisi," amesema Mtupa.
Kiungo huyo ambaye aliwahi kuitumikia Yanga Princess, Baobab Queens, Get Program na nyinginezo tayari ameshawasili nchini Uturuki kuanza majukumu mapya.