Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mandonga kukiwasha Zanzibar leo

MANDONGA Pict

Muktasari:

  • Pambano hilo la Mandonga na Michael William litakuwa sehemu ya shughuli kubwa ya usiku huo na pambano kuu litakuwa kati ya Joshua Tusingwire kutoka Uganda dhidi ya Mtanzania, Hamis Magazeti.

VISIWA vya marashi ya karafuu, Zanzibar, vitakuwa na bashasha kubwa kuelekea tamasha kubwa la ngumi la Boxing in Paradise linalotarajiwa kufanyika leo Septemba 29, 2026, kuanzia saa 12 jioni na pambano linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki ni lile la bondia maarufu, Karim Mandonga ‘Mtu Kazi’ dhidi ya Michael William.

Akimzungumzia mpinzani wake, Michael William ameweka wazi hii ni mara yake ya kwanza kufika visiwani Zanzibar na amekuwa hapo kwa miezi kadhaa akifanya mazoezi makali ya kujiandaa na pambano hilo ili kuhakikisha anapata ushindi.

Michael ameongeza kwa utani anatumai Mandonga atatokea ulingoni kwani alipata taarifa alikuwa kwenye starehe za ‘7G’ hadi usiku wa manane, hivyo anatamani kumwona ulingoni ili kumaliza kazi aliyoianzia mazoezini. 

Kwa upande wake, Mandonga amejibu mapigo hayo kwa kujiamini na kusisitiza safari hii amedhamiria kushinda ili kuiwakilisha vyema Tanzania na kulinda heshima ya bendera ya taifa kama alivyofanya nchini Kenya licha ya kudharauliwa hapo awali.

“Mimi ni bondia wa tofauti sana duniani, hakuna bondia aliyezalisha maneno, ngumi na majina kama mimi. Hili nimejiandaa vizuri na ndoto yangu sijawahi kupigana na mtu mweupe, naamini Mzungu nitampiga kivyovyote na kuipa nchi yangu ushindi mkubwa.”

Kwa mujibu wa takwimu za mtandao wa kurekodi matokeo ya ngumi duniani wa BoxRec, Karim Mandonga amepanda ulingoni katika mapambano 21 ya kulipwa (ushindi mapambano saba, vipigo 10, na sare nne), huku akiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa TKO dhidi ya Daniel Wanyonyi nchini Kenya na Kenneth Lukyamuzi.

Mpinzani wake, Michael William, anaingia ulingoni akiwa na rekodi na uzoefu wa mapambano ya kimataifa, ambapo ametumia miezi kadhaa kisiwani humu kujenga utimamu wa mwili na mbinu za kumkabili Mandonga.

Pambano hilo la Mandonga na Michael William litakuwa sehemu ya shughuli kubwa ya usiku huo na pambano kuu litakuwa kati ya Joshua Tusingwire kutoka Uganda dhidi ya Mtanzania, Hamis Magazeti.