Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MKALI WENU: Nilinusurika kifo kwa wizi ndani ya daladala

MKALI Pict

Muktasari:

  • Mkali Wenu mwenye umri wa miaka 24 amesimulia baadhi ya matukio aliyoyafanya wakati anajitafuta, ndani yake yamejaa mafunzo, huzuni na kuchekesha alipofanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti.

MCHEKESHAJI maarufu nchini, Miraji Supakila 'Mkali Wenu' amesema haikuwa kazi rahisi kufika hapo alipo kutokana na changamoto alizokutana nazo na kama siyo kuwa na roho ngumu huenda angeishia njiani.

Mkali Wenu mwenye umri wa miaka 24 amesimulia baadhi ya matukio aliyoyafanya wakati anajitafuta, ndani yake yamejaa mafunzo, huzuni na kuchekesha alipofanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti.

Katika mahojiano hayo yaliyozaa makala haya, Mkali Wenu anasema kuna vitu anavitoa kama somo kwa vijana akiwataka kuacha kusaka pesa haramu, kwani huwa hazina maendeleo, akikumbushia tukio lililokaribia kumpeleka ahera kwa kuiba ndani ya daladala. Ebu endelea naye...!

MKA 02

KWA NINI NGUMI

Mkali Wenu anataja sababu za kuingia kucheza ngumi katika uzani wa kilo 66 hadi 69 ni kutafuta Sh200 milioni kupitia mapambano atakayocheza, baada ya hapo ataangalia ni kitu gani kingine anapaswa kukifanya.

"Historia ya maisha yangu ni duni, napambana kwa halali kwa kadri niwezavyo ili kujitengenezea kipato kama kijana, wakati naingia kucheza ngumi nilisema nahitaji kutengeneza Sh200 milioni, nimecheza mapambano manne, tayari nimeishaanza kuona mwanga," anasema Mkali Wenu na kuongeza:

"Pambano la kwanza nilipigana na Ajibu Salum nilimshinda kwa TKO lilikuwa la raundi sita, lingine ni dhidi ya Ambokile Chausa nilimshinda kwa pointi, kabla ya kupigana naye nikaingia kuangalia CV yake niliogopa sana, moyoni nilikuwa natetemeka ila usoni nilikuwa nacheka ili kujikaza.

"Pambano dhidi ya Seleman Jalile meneja aliposema nitapigana naye nikaingia kuangalia CV yake nikaona amewahi kupigana na Pacquiao nikasema sipo tayari, meneja akasema nimechukua pesa za watu, nikasema nitazirudisha akasema kuanzia maandalizi utakuwa na Sh40 milioni, ikabidi niombe pesa nikadanganye mama anaumwa, nikaenda kujichimbia Afrika Kusini kufanya mazoezi, lakini nilishinda kwa pointi.

"Niliahidiwa Sh5 milioni nikamwambia meneja aongeze Sh1 milioni ili iwe sita, akafanya hivyo nikaenda Sinza kufanya masaji ya mwili, nikanyoa vizuri, kusema ukweli pale nilijua ngumi zinauma, mwingine niliyepigana naye pia nikashinda kwa pointi ni Bakari Dume."

Anasema kinachomsaidia ni umaarufu, kwani kuna mabondia ambao wanapata pesa ndogo, anachosisitiza anapenda ngumi kutokana na pesa ndefu anazopata kwa mkupuo: "Sina maana nimeacha uchekeshaji, nafanya vyote ila katika uchekeshaji unaweza ukawa unapata Sh200,000 kwa mfano kila siku, hiyo haitoshi pekee napaswa kupambana.

"Nagawa muda wangu kwa kuamka saa 11:00 alfajiri kila siku nafanya mazoezi hadi saa 3:00 asubuhi, napata muda wa kupumzika kisha naanza kushuti, kuediti na kuzipandisha video zangu."


MTUNZI WA NYIMBO

Kitu wasichokijua wengi nyuma ya pazia, amewaandikia nyimbo wasanii mbalimbali wa Bongo Fleva, anawataja Marioo, Juma Jux, Billnass, Whozu na Ali Kiba: "Mfano Marioo kaniajiri ingawa mkataba wetu siyo wa makaratasi, mfano wimbo wa Oluwa na nyingine nyingi."

Anaongeza: "Mfano nyimbo za Ali Kiba ni kama Mediocre, December, waliyoimba Billnass ft Whozu wa Bodaboda, naandika sana sema ni vile watu wananifahamu zaidi katika vichekesho na ngumi kwa sasa."

Anasema akiona mambo hayaendi katika ngumi basi atahamishia majeshi katika kuimba, lengo ni kuhakikisha anakuwa na hatua za kimaisha tofauti na hali duni aliyotokea.

MKA 03

"Tumetoka familia zenye maisha tofauti, nakumbuka nikiwa hali duni nilikuwa natamani kununua tv, kuwa na simu ya smati, nimevipata, ndiyo maana naishi katika uhalisia wangu, nikiwa sina sina, nikiwa nacho ninacho," anasema.


ALINUSURIKA KIFO

Anasema kuna kipindi alikuwa anaishi kwenye geto la mshikaji wake, lakini ilifikia kipindi rafiki yake alimwambia anataka kuoa anatakiwa ampishe, hapo ndipo shetani alipoingia kuchukua nafasi katika moyo wake.

"Nilikuwa katika usafiri wa umma (daladala) maeneo ya Kigogo, dada mmoja alifungua pochi ili atoe nauli, nilipochungulia na kuona pesa nikaona Mungu kanitembelea, nikaiiba na kushuka, huku na kule yule dada akaanza kupiga kelele na kunionyesha yule kaka kashuka na pochi yangu," anasema na kuongeza:

"Nikaanza kukimbizwa bahati nzuri nilikiona choo nikaingia humo, wale ambao walikuwa wananifukuza wakapitiliza kwa uoga nilikaa hapo kuanzia saa 12 jioni hadi saa 1:00 usiku, nilikuwa natetemeka nikisema Mungu nisamehe sitarudia tena, nilikuwa sina namna yoyote niliona kama umenionyesha njia.

"Nikatoka chooni huku mwili mzima unanuka maana kilikuwa kichafu sana, nilipoenda sehemu ya utulivu nikakutana na Sh89,000, pamoja na kwamba mimi ni Muislamu nikachukua Sh9000 nikaenda kutoa sadaka kanisani kumshukuru Mungu kuniepusha na kifo.

"Tangu hapo sikuwahi kurudia tena kukwapua vitu vya watu, nilianza kujituma katika harakati mbalimbali kuchekesha, nipo katika ngumi na ipo siku nitaimba."

MKA 01

Anaulizwa pesa iliyokuwa imebakia ulifanyia nini? Anajibu: "Pesa za haramu haziwezi kufanya kitu cha maana, nilikuwa na msichana nilimpenda sana nilimhonga yote, usinione hivi nikimpenda mtu nampenda kweli anaweza akawa ananipiga matukio ila siku nikichoka siwezi kurudi nyuma."

Anaongeza: "Pamoja na ubondia wangu huu kuna wakati kaka angu ananipiga makofi na kuniambia acha ujinga wewe ni bondia kaza, usiendekeze kupenda hivyo, mimi ni mtu wa watu lakini siyo wa kila mtu, nikimpenda mmoja namaanisha huyo huyo."

MKA 04

USHIKAJI NA HARMONIZE

Anasema ni washkaji kwa sababu tabia zinaendana za aina ya warembo wanaowapenda, jambo la pili wanatoka sehemu moja (Wamakonde).

"Pamoja na utani ambao namtania sana Harmonize wakitengana na Kajala nyuma ya pazia ni mtu ninayemshauri kwa ustarabu, ukimkuta Konde Boy ana msichana mwembamba basi mtu wake asiwe anamuwazia vibaya," anasema Mkali Wenu shabiki lialia wa Yanga.

Mkali Wenu anasema watu anaowakubali zaidi Yanga ni Pacome Zouzoua, Bakari Mwamnyeto, msemaji wa klabu hiyo, Ally Kamwe na mdhamini GSM: "Hao watu nawakubali sana kwa Simba namkubali Mohammed Dewji na msemaji wao Ahmed Ally pamoja na timu yao kutokufanya vizuri lakini bado anaipambania kwa kuizungumzia vizuri, wakikutana na Kamwe wanachangamsha mitandao ya kijamii."

Anasema mwanzoni wakati anaanza kuchekesha familia waliyozaliwa watoto sita, akiwa wa tatu haikukubaliana na kazi hiyo, walimuona ni mvivu asiyependa kujituma kwa bidii.

"Ujue uchekeshaji ulikuwa unaonekana kama hatuna akili, tofauti na kipindi hiki.

Anaongeza: "Iwe kwenye ngumi ama uchekeshaji sikuwahi kumwangalia mtu nikasema kupitia huyu nitafanya hivi, ila ninaowakubali nikiwatazama ni kama Joti, kwa upande wa ngumi kuna Hassan Mwakinyo, Karim Mandonga, Ibrahim Class, Mfaume Mfaume, Nasibu Ramadhani hao ni baadhi tu."


WALIKUTANAJE NA NABII MKUU

Anasema baada ya kumfuatilia Nabii Mkuu Dr. GeorDavie, akafanya video inayomhusu na baada ya kumfikia akamwalika kanisani kwake: "Baada ya ibaada alinizawadia gari, kanitamkia baraka na kanipa vitu mbalimbali."