Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

 SELEMANI ZUGO: Nilikatwa kilo mpaka mate yakakauka kupigana na Kiduku

Muktasari:

  • Zugo si kocha tu ni kocha mchezaji ambaye ulingoni anaingia na ana uwezo wa kuonyesha kwa vitendo jinsi ya kupiga ‘jab’, ‘uppercut’, na kucheza na ‘light’ uwanjani.

UKIKUTANA naye mitaani, unaweza kudhani ni mwanamichezo wa kawaida tu anayepita na mfuko wa mazoezi mabegani. Lakini huyu si mwingine bali ni Selemani Zugo, moja ya makocha wanaovuja jasho na akili nyingi katika kukuza mchezo wa masumbwi nchini kupitia kituo chake cha Zugo Gym.

Zugo si kocha tu ni kocha mchezaji ambaye ulingoni anaingia na ana uwezo wa kuonyesha kwa vitendo jinsi ya kupiga ‘jab’, ‘uppercut’, na kucheza na ‘light’ uwanjani.

Katika mahojiano ya kina na gazeti la Mwanaspoti, Zugo amefunguka maisha yake kuanzia jinsi mama yake mzazi alivyomuingiza kwenye ngumi kwa “fimbo na mtumbi,” siri ya kufuta simu za mabondia kambini, hadi jinsi alivyopigwa ulingoni kwenye pambano lake la kwanza lakini majaji wakampa sare.


MAMA BONDIA NA KARATE

Baadhi ya simulizi za wanamichezo wengi Tanzania zinaeleza kuwa awali wazazi wao hawakutaka waingie kwenye mchezo fulani, lakini baadaye walibadilika baada ya kuona kipaji au mapenzi makubwa ya watoto wao.

Kwa Selemani Zugo, simulizi hiyo ni tofauti kidogo kwani mama yake ndiye aliyekuwa mwalimu wa kwanza wa mapambano, akimfundisha misingi ya kujilinda nyumbani kabla hata hajafahamu maana ya kuwa bondia.

Zugo anasimulia kuwa akiwa mtoto, mama yake alikuwa akimfundisha namna ya kupigana na kujilinda kwa kutumia mbinu alizokuwa akizifahamu, huku wakati mwingine akichanganya mafunzo ya ngumi na yale ya karate. Haikuwa aina ya mafunzo ya kawaida ya mazoezi ya gym, bali ilikuwa sehemu ya maisha ya kila siku nyumbani.

ZUG 02

“Mama ndiye aliyenifundisha kwanza. Tulikuwa tunapigana nyumbani, ananifundisha kwa fimbo na mtumbi. Alikuwa anachanganya ngumi na karate, kwa hiyo nilianza kujifunza mapambano kabla hata sijajua nitakuja kuwa bondia,”  Zugo anasimulia.

Zugo anasimulia kituko cha nyumbani kwao ambapo mama yao alikuwa na sheria zake. “Tukikoseana kinyumbani, mama alikuwa hachukui jukumu la kukupiga viboko mara moja. Kwanza alikuwa anatukutanisha kwenye ‘mtumbi’  tupigane ngumi! Baada ya hapo, ndipo anamchukua yule aliyeshindwa au mdogo na kumtandika viboko”.

Baada ya kuona kila siku yeye anapoteza na kuishi kwa unyonge, Zugo aliamua kuanza kufanya mazoezi kwa bidii ili kufuta uteja huo. Na hapo ndipo alipoanza kushabiki mchezo wa ngumi.  Hapo ndipo mapenzi yake ya ngumi yalipozaliwa, huku baba yake mzazi akiwa amefariki akiwa bado mdogo sana. Baadaye alilelewa na mwanamichezo mwingine, Mzee Pingu, ambaye alikuwa mtu wa soka.


KUTOKA VYUMA

Kabla ya kuingia kwenye ngumi za kulipwa, Zugo alikuwa mnyanyua vyuma mahiri (bodybuilding) na hata kufanikiwa kutwaa taji la Mr. Tanzania. Alianza ngumi za ridhaa tangu mwaka 2006 akiwa jeshini kabla ya kuingia rasmi kwenye ngumi za kulipwa mwaka 2013 au 2012. Zugo anasisitiza kuwa enzi zao walikuwa wakipigana kweli sio ngumi za michongo za sasa hivi.


MECHI YA KWANZA

Zugo anasema pambano lake la kwanza la kulipwa hatalisahau kutokana na ugumu alioupata. “Lilikuwa pambano gumu na zito sana dhidi ya Seba Temba kule Morogoro”.

“Mimi nimetoka kwenye vyuma, ngumi kwangu hazikuwa kipaji bali nilijifunza tu. Tulizichapa raundi sita. Kiukweli nilipigwa kweli kweli, ule ndio ukweli usioweza kufichika! Lakini ubishi wangu ulinisaidia, hata nikidondoka nanyanyuka tena, mwisho wa siku majaji wakatoa sare.

ZUG 03

Zugo alicheza jumla ya mechi  21, akishinda mechi 15 na kupoteza mechi nne tu (mbili nje ya nchi na mbili ndani) vipigo viwili dhidi ya Masha Kimkemo na mbabe Twaha Kiduku.

Anongeza kuwa pambano lake na Twaha Kiduku mwaka 2016 lilikuwa gumu kweli kweli , ambapo alipoteza kwa pointi. “Kwenye lile pambano nililazimika kukata kilo sana hadi mate yakawa hayatoki mdomoni! Niliingia ulingoni nikiwa mnyonge na dhaifu sana lakini nilipambana kiume”.


UKOCHA NI KIPAJI

Zugo anabainisha kuwa yeye kipaji chake hakikuwa kwenye ubondia bali alitamani siku moja awe kocha wa kuwafundisha mabondia tofauti.

“Nikiwa namsimamia bondia wangu, mimi ni rahisi sana kunipiga mimi ulingoni kuliko kumpiga mchezaji niliyemsimamia”. Zugo amesoma na kufuzu mafunzo ya ukocha ya BFT na ana vyeti vya One Star Coach na Refarii wa Kimataifa wa Dunia. Alisomea ukocha katika Chuo cha Polisi kikiwa kimeshirikisha makocha kutoka Afrika Mashariki na Afrika nzima.


MLO WA MABONDIA

Zugo anasema kwa sasa ana mabondia saba wanaoishi kambini, hivyo suala la chakula limekuwa sehemu muhimu ya maandalizi yao ya kila siku. Anaeleza kuwa wanapokuwa kambini wanazingatia mlo kamili na wenye uwiano.

Anasema mabondia hao hupewa chakula kinachowasaidia kupata nguvu za kufanya mazoezi, huku akisisitiza kuwa hawataki kula kwa kubahatisha kwa sababu kila bondia ana mahitaji yake kulingana na uzito, ratiba ya mazoezi na maandalizi ya pambano.

“Huwezi kumwambia bondia atumie nguvu wakati ana siku mbili hajala chakula cha maana, hawezi hata kumaliza robo ya dona! Sio sawa unakuta bondia anakula chipsi .

Zugo amefichua ratiba kamili ya chakula kwa mabondia wake anasema asubuhi huwa wanaanza na kupasha misuli moto kwanza ndipo wanak imbia. Wakirudi wanapata uji wa lishe au chai yenye viungo kamili.

ZUG 04

Kisha saa 4 asubuhi Chai, chapati, na mchuzi kidogo. Baada ya hapo wanatakiwa kulala hapo hapo sebuleni hata kama wana jasho ndipo baadae wataoga.

Saa 8:00 Mchana wanakula ugali wa Dona uliosindikizwa na mboga za majani, nyama, na dagaa kwa ajili ya kupata protini. Baada ya hapo wanapumzika tena.

Saa 10:00 Jioni, Karanga na uji wa lishe kabla ya kuingia kwenye mazoezi makali kisha saa 1 usiku wanapata chakula cha jioni. “Saa tatu usiku, simu zote tunazichukua! Simu zinapoteza muda wa kulala. Ukipoteza hata saa moja tu la kulala kama bondia, mwili unachoka na nguvu inapotea uwanjani,” anasisitiza Zugo kwa ukali. Anabainisha kuwa bondia anayefuata utaratibu huu hawezi kupigwa kirahisi hata acheze raundi 10 au 12.


MAPROMOTA

Zugo Gym kwa sasa ina wachezaji saba chini ya mkataba na menejimenti yake, wakiwemo mabondia wanawake watatu (mmoja tayari amepata ajira jeshini kupitia ngumi). Zugo anasisitiza kuwa hawataki mechi za michongo.

 Alitolea mfano wa kughairishwa kwa pambano la kukata na shoka kati ya bondia wake Sophia Hamis na Stumai Muki.

“Pambano la Sophia na Stumai si pambano la kawaida, ni kama Dulla Mbabe na Twaha Kiduku kwa upande wa wanawake. Hata hivyo, pambano hilo lilishindikana kwa sababu promota hakuwa mnyofu na alikuwa akisogeza mbele tarehe bila mawasiliano yoyote,” anasema Zugo

“Tunatamani tupate tena mechi na Stumai na namuomba promota Madam Latifa, tunakuomba uchukue pambano hili. Hatuna tamaa ya pesa, hata bure tupo tayari kupigana, lakini tunataka heshima na taarifa mapema ili tujiandae!”.

ZUG 05

MWAKINYO NA MANDONGA

Zugo amewataka wadau wa ngumi nchini kutoa maua yao kwa mabondia wawili waliopandisha chachu ya mchezo huo nchini, Hassan Mwakinyo aliyeliletea taifa mafanikio na Karim Mandonga.

“Licha ya kuwa ulingoni Mandonga ni bondia wa kiwango cha chini sana, lakini komedi zake zimefanya mchezo wa ngumi kufahamika zaidi  na kuvuta mashabiki wengi viwanjani”.

Zugo Gym inaendeshwa kama taasisi ya kifamilia ambapo Selemani Zugo anashirikiana na ndugu zake, akiwemo dada yake Tanga Adoso kama meneja, na mdogo wake Doto Zugo ambaye ni mwanajeshi kama kocha msaidizi.

Kupitia ngumi, Zugo anasema amejiwekeza kwenye mambo mbalimbali ikiwemo nyumba aliyoijenga Gongo la Mboto. “Ngumi si usela kama watu wanavyodani ingawa ni mchezo wa kimasikini, ni ajira na inalipa kama utakuwa na heshima na mchezo huo” anahitimisha Zugo.