Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Malota: Nilisajiliwa kwa mshahara wa sh200 tu!-2

Malota

Muktasari:

Pia aligusia pambano asilosahau likihusisha Simba na Al Ahly, akizungumzia pia namna ambavyo kuna utofauti mkubwa wa soka la enzi zao na lilivyo sasa. Leo tunaendelea na simulizi yake akifunguka mambo kadhaa.

WIKI iliyopita tulianza simulizi la straika wa zamani wa Simba, Malota Soma ‘Ball Jungler’ ambapo alieleza jinsi alivyosajiliwa Msimbazi kwa malipo ya samani na kulipwa Sh200 kwa mwezi, huku akigusia namna alivyokabiliwa na changamoto kutoka kwa kina Zamoyoni Mogella na wenzake.

Pia aligusia pambano asilosahau likihusisha Simba na Al Ahly, akizungumzia pia namna ambavyo kuna utofauti mkubwa wa soka la enzi zao na lilivyo sasa. Leo tunaendelea na simulizi yake akifunguka mambo kadhaa.

Wivu wa mafanikio

Malota anasema wachezaji wengi wa sasa hawajitumi wala kuwa na wivu wa mafanikio au maendeleo kama ilivyokuwa enzi zao.

“Kwa sasa wachezaji wengi hawajiamini na hawana wivu wa mafanikio ya wenzao.n

“Nyota wa zamani wamefika walipo kwa sababu walikuwa na wivu mkubwa wa kimaendeleo dhidi ya wenzao, mtu unapenda kuwa kama fulani na hivyo unajibidiisha kumfikia na hata kumpita mchezaji aliyekusisimua kwa umahiri na maendeleo yake. Leo hii wachezaji hawaoneani wivu na asilimia kubwa wanaonekana wameridhika,” anasema.

Ushirikina

Kuhusu vitendo vya kishirikina, Malota anasema havina msaada wowote, ila wanaoviendekeza vimekuwa vikiwabeba kwa imani zao.

“Ushirikina ni imani tu, katika soka mazoezi ndiyo kila kitu. Imani kama imani ni kitu cha ziada kwenye soka hivyo sioni mchezaji akishindwa kufanikiwa kama ana imani na anafanya mazoezi.

“Kama ukiamini mambo ya kishirikina, yanaweza kukusaidia kwa kuwa ndicho unachoamini kuwa kitakupa mafanikio. Hivyo wakati ninacheza, kuna wenzetu waliamini mambo hayo na kuwa mastaa na kufanikiwa.

“Hivyo ushirikina haukwamishi soka letu kwa kuwa unakuwa uko nje ya uwanja, mchezo na miguu ndiyo ndani ya uwanja. Hivyo mchezaji mwenyewe ndiye anayeweza kuamua lipi zuri na lipi baya.”

Malota anasema haamini kama kufeli kwa baadhi ya wachezaji kunatokana na ushirikina, bali ni wachezaji wenyewe kushindwa kujipanga na hasa kutofanya mazoezi ya kutosha na kujiamini.

Simba/Yanga

Mkali huyo anakiri kuwa ushirikiana kwa klabu za Simba na Yanga ni kama ibada kwao. Kila mtu uliyekuwa ukikutana naye iwe ni kutokana na mafanikio au kukosa mafanikio, alikuwa akiambiwa kuwa imetokana na ushirikina.

“Mimi sikuwahi kuona kama imani ya kishirikina zingenisaidia, lakini kwa Simba chochote tulichokuwa tukikifanya tulikuwa tunaambiwa na viongozi na baadhi ya wanachama kuwa tukajitengeneze.

“Mfano mashabiki na wanachama wakiona umeshuka kiwango hakuna ambaye alifikiria labda kuna tatizo fulani la kiafya au uvivu, wengi walikuwa wanashauri mchezaji aende kwa mganga kwa sababu walikua wakiamini kuwa kushuka kiwango kulitokana na wachezaji wengine kuwa wamekufanyia mambo ya kishirikina,” anasema.

Kikosi Bora

Malota aliyejiunga Simba 1981 akitokea Tumbaku Morogoro iliyokuwa ikishiriki Ligi na alipojiunga na Simba aliweza kucheza kwa miaka tisa bila kuhama.

Kwa kipindi chote alichokuwa Msimbazi anasema hakuwahi kucheza kwenye kikosi bora kama kilichokuwa kati ya 1981 hadi 1984. Anakitaja kikosi hicho kuwa ni cha Kipa Moses Mkandawile, mabeki Mussa Kihwelu, Mohammed Kajole, Thobias Nkoma na Lilla Shomari.

Viungo walikuwa ni Mtemi Ramadhani, Sunday Juma, Nico Njohole na George Kulagwa, huku mastraika wakiwa ni Mogella na yeye Malota.

Anasema aliikacha Simba na kwenda Oman kucheza soka la kulipwa kabla ya kurejea mwaka 1991 hadi 1995 akiendelea kuichezea ambapo anadai pia kiliundwa kikosi matata ambacho hawezi kukisahau.

Kikosi hicho ni kile kilichoundwa na kipa Mohammed Mwameja, Deo Mkuki, Kasongo Athuman, Godwin Aswile, George Masatu, Ramadhani Lenny, Abdul Ramadhani ‘Mashine’, Hussein Masha, Thomas Kipese, Edward Chumila na yeye Malota Soma.

Wasumbufu

Mkongwe huyo anakiri kuwa licha ya umakini na uhodari wake Uwanjani, lakini alijikuta katika wakati mgumu kila alipokuwa akikutana na baadhi ya wachezaji waliomsumbua.

Anawataja mabeki Kasanga Bwallya wa Nyota Nyekundu kabla ya baadaye kuichezea Simba, alimnyima raha kama ilivyokuwa pia akikutana na Athuman Juma Chama ‘Jogoo’ wa Yanga.

“Hawa jamaa walinipa wakati mgumu. Walikuwa wakininyima furaha nilipokuwa nikicheza dhidi yao. Hakika siwezi kuwasahau kwa sababu ya ubabe na soka lao la nguvu,” anasema.

Singano acha kabisa

Licha ya kuwashuhudia wachezaji kadhaa nyota wa kizazi cha sasa, hata hivyo Malota ameshindwa kuficha hisia zake kwa kuwataja baadhi ya waliomkuna ndani ya Simba.

Anawataja Juma Kaseja, Boniface Pawasa, Yusuf Macho, Patrick Mutesa Mafisango, Haruna Moshi ‘Boban’, Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Ramadhan Singano ‘Messi’ kuwa ni wachezaji wa kipekee tangu astaafu kucheza kwake soka.

“Wamepita wengi Simba na wengi niliwakubali, ila nimevutiwa zaidi na Singano, ni mchezaji wa kipekee, mdogo, haogopi beki na hata kama mchezaji anacheza rafu vipi haogopi chochote.”

Itaendelea jumanne ijayo...