Nabi ampa tano Manula
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi alisema Manula alikuwa na mchango mkubwa katika kuisaidia Azam kutoka salama kwenye mchezo huo, akieleza kuwa bila uhodari wa kipa huyo, timu yake ingeweza kupata wakati mgumu zaidi.
KOCHA Nasreddine Nabi amemsifu kipa wa Azam FC, Aishi Manula, akisema kiwango alichoonyesha katika mchezo dhidi ya wapinzani wao ni uthibitisho kuwa bado ana uwezo mkubwa wa kulinda lango, huku akiwataka mabosi wa timu hiyo kumlinda na kumthamini kutokana na uzoefu alionao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi alisema Manula alikuwa na mchango mkubwa katika kuisaidia Azam kutoka salama kwenye mchezo huo, akieleza kuwa bila uhodari wa kipa huyo, timu yake ingeweza kupata wakati mgumu zaidi.
Akizungumzia kiwango cha kipa huyo, Nabi alisema Manula ni mlinda mlango mwenye ubora mkubwa, akisisitiza kuwa makipa wanavyozidi kukomaa na kupata uzoefu wa michezo mingi ndivyo wanavyozidi kuwa bora.
“Manula ni kipa mwenye daraja la juu. Kwa makipa ambao nimewahi kukutana nao, ana kiwango kikubwa. Kama si yeye, Azam isingeweza kutoka salama kwenye mchezo huo,” alisema Nabi.
Manula alianza kucheza soka la kulipwa akiwa Azam FC kabla ya kuhamia Simba mwaka 2017. Alidumu Simba kwa miaka minane, kuanzia 2017 hadi Julai 2025, akicheza nafasi muhimu katika mafanikio ya timu hiyo na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo kuanzia msimu wa 2017/2018 hadi 2020/2021.
Akiwa Simba, Manula alijijengea jina kama mmoja wa makipa waliotegemewa zaidi nchini na pia alikuwa chaguo la kwanza Taifa Stars. Rekodi zinaonyesha alicheza mechi 21 za ligi msimu wa 2021/2022 na mechi 22 msimu wa 2022/2023, kabla ya kucheza mechi tano za ligi msimu wa 2023/2024. Msimu wa 2024/2025 hakucheza mechi za ligi akiwa Simba.
Julai 2025, Manula alirejea Azam FC, klabu aliyokuwa akiichezea kabla ya kuhamia Simba. Ujio wake uliipa Azam mchezaji mwenye uzoefu wa ligi, mashindano ya kimataifa na timu ya taifa. Katika msimu wa 2025/2026, akimaliza mwaka wa kwanza akiwa na rekodi za kucheza mechi 16 kati ya 30.
Mechi ijayo ya kimataifa ya Azam FC ni dhidi ya ZED FC ya Misri mchezo wa marudiano wa raundi ya pili Kombe la Shirikisho Afrika.