Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makata, Katwila kuviziana kimbinu Ushirika kesho

MOSHI Pict

Muktasari:

  • Pambano hilo litakalopigwa kesho, Novemba 1, 2026 kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, linakutanisha Polisi Tanzania inayotafuta kurejea kwenye ushindi nyumbani baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Pamba Jiji, huku Geita Gold, iliyopata pointi moja ugenini dhidi ya TRA United, ikiahidi kuwapa presha wenyeji na kuwalazimisha kufanya makosa ili iyatumie kupata ushindi.

UWANJA wa Ushirika unatarajiwa kushuhudia vita ya mbinu kesho, Novemba 1, 2026 wakati makocha wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata, na Geita Gold, Zuber Katwila, watakapokutana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Makocha hao wameanza kuonyesha mikakati yao kuelekea pambano hilo, kila mmoja akiamini ana mbinu sahihi za kumshinda mwenzake na kuondoka na pointi tatu.

Wakati Makata akisisitiza umuhimu wa tahadhari, kurekebisha makosa na kutumia udhaifu wa wapinzani, Katwila amesema Geita Gold itatumia presha kuwafanya wenyeji wakose umakini na kufanya makosa yatakayowapa nafasi ya kuadhibu.

Polisi Tanzania inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kiu ya kurejea kwenye ushindi nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Pamba Jiji katika uwanja huo wa Ushirika.

Kwa upande mwingine, Geita Gold inawasili ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya TRA United katika mchezo uliopita, matokeo yanayoipa matumaini ya kufanya vizuri hata inapokuwa ugenini.

MOSH 01

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Makata amekiri kuwa haitakuwa kazi rahisi kuikabili Geita Gold, akisema matokeo ya timu hiyo katika mchezo uliopita yanaonyesha ina uwezo wa kupambana hata inapokuwa ugenini.

Amesema Polisi Tanzania imejiandaa kwa umakini, huku benchi la ufundi likifanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika michezo iliyopita ili kuepuka kupoteza pointi nyingine mbele ya mashabiki wake.

“Matokeo yao yananiweka katika changamoto kwa kuwa wamejipanga vizuri. Katika mchezo wa ugenini dhidi ya TRA walipata pointi moja, jambo linaloonyesha kuwa ni timu inayojipanga vizuri hata inapocheza nje ya uwanja wake.

“Kwa hiyo tutaingia kwa tahadhari, tukirekebisha makosa tuliyofanya na pia kuchunguza udhaifu wa Geita ili tuweze kuutumia kupata ushindi,” amesema Makata.

Amesema sare waliyopata dhidi ya Pamba Jiji nyumbani imeongeza umuhimu wa mchezo huo, kwani wanahitaji pointi tatu ili kurejesha furaha kwa mashabiki wao.

“Tunayo kazi kubwa ya kuhakikisha tunapata pointi tatu mbele ya Geita katika uwanja wetu wa Ushirika. Tukizingatia mchezo uliopita tulitoka sare na Pamba, hatuna budi kupambana ili kuwafurahisha wananchi wa Kilimanjaro na wadau wa Polisi Tanzania,” amesema.

MOSH 02

Kwa upande wake, Katwila amesema Geita Gold haitaruhusu Polisi Tanzania kutawala mchezo kwa urahisi, akieleza kuwa mpango wao ni kuwapa presha wenyeji na kuwalazimisha kufanya makosa.

Kocha huyo amesema wanafahamu ubora na mapungufu ya Polisi Tanzania, lakini wamejiandaa kutumia kila nafasi itakayojitokeza ili kupata matokeo mazuri.

“Tunajua wana ubora wao na udhaifu wao, lakini mpira unachezwa na binadamu, hivyo lazima kutakuwa na makosa ambayo wanaweza kuyafanya. Sisi tutajitahidi kuwalazimisha wafanye makosa hayo ili tuyatumie kupata matokeo,” amesema Katwila.

Ameongeza kuwa wanafahamu Polisi Tanzania itakuwa na shinikizo la kutafuta ushindi kutokana na kucheza nyumbani, hasa baada ya kutoka sare katika mchezo uliopita, lakini Geita Gold imejiandaa kukabiliana na changamoto hiyo.

“Ugumu utaanzia hapo, kwa sababu wao watatumia juhudi na maarifa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri nyumbani. Sisi tumejiandaa kisaikolojia kukabiliana na hali hiyo na kupambana kuhakikisha tunapata matokeo,” amesema.

Katwila amesema kikosi chake kitachagua mbinu kulingana na aina ya mpinzani, huku kikiheshimu uwezo wa Polisi Tanzania.

Mbali na vita ya kimbinu kati ya makocha hao, wachezaji wa timu zote mbili wameeleza utayari wao kuelekea mchezo huo.

Joseph Majagi wa Polisi Tanzania, amesema morali ya kikosi iko juu na wachezaji wamejipanga kutekeleza maelekezo ya benchi la ufundi ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Amewaomba mashabiki wa Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Ushirika ili kuwapa hamasa wachezaji wakati wa mchezo huo.

Kwa upande wa Geita Gold, Datius Peter, amesema wamejiandaa kukabiliana na changamoto ya kucheza ugenini, huku akiwaomba mashabiki kuendelea kuwaunga mkono na kuwaombea.

Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Inspekta Frank Lukwaro, amesema kikosi hicho kimewasili salama mjini Moshi kikitokea Ruangwa, mkoani Lindi, ambako kilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Namungo.

Amesema timu tayari imeanza maandalizi ya mchezo huo na inatambua ugumu wa pambano hilo, lakini anaamini ubora wa wachezaji waliopo kikosini utawasaidia kupata ushindi.

Naye Ofisa Habari wa Geita Gold, Samuel Dida, amesema timu hiyo haina hofu ya kucheza katika Uwanja wa Ushirika kwa kuwa inaufahamu vizuri.

“Polisi, sisi Ushirika si wageni. Tunaufahamu vizuri uwanja huo, nao wanatufahamu. Kwa hiyo hatuwezi kuingia uwanjani tukiwa na hofu yoyote,” amesema Dida.

Amesema wanaiheshimu Polisi Tanzania, lakini wamejiandaa kupambana kuhakikisha wanaondoka Moshi na matokeo yatakayoiweka timu yao katika nafasi nzuri zaidi.