Polisi Tanzania, Pamba Jiji mechi ya kibabe
Muktasari:
- Polisi iliyotumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini, Arusha kwa mechi zake za nyumbani tangu msimu huu wa 2026-2027, umeanza, leo inarudi kwenye Uwanja wa Ushirika kwa mara ya kwanza.
BAADA ya miaka mitatu na siku 161, Uwanja wa Ushirika, Moshi utashuhudiwa mechi ya raundi ya tisa ya Ligi Kuu ikichezwa kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2022-2023, kati ya wenyeji maafande wa Polisi Tanzania dhidi ya Pamba Jiji ya Mwanza.
Polisi iliyotumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini, Arusha kwa mechi zake za nyumbani tangu msimu huu wa 2026-2027, umeanza, leo inarudi kwenye Uwanja wa Ushirika kwa mara ya kwanza.
Timu hizo zinakutana katika Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza, hazina uwiano mzuri wa safu ya kujilinda na ile ya ushambuliaji, ambapo Polisi Tanzania imefunga mabao 11 na kuruhusu 10, huku kwa Pamba Jiji ikifunga tisa na kuruhusu 14.
Polisi itaendelea kumtegemea mshambuliaji wake, Anuary Jabir anayeongoza katika mbio za ufungaji, baada ya kuchangia mabao saba kati ya 11, akifunga sita na kuasisti moja.
Pamba Jiji wenyewe tegemeo lao ni mshambuliaji, Deogratius Mafie aliyechangia mabao matatu kati ya tisa ya kikosi hicho, baada ya kufunga mawili na kuasisti moja, akifuatiwa na kiungo, Idriss Diomande mwenye mabao mawili pia.
Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata amesema kucheza katika uwanja wao wa nyumbani utatoa nafasi kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi na kuwapa sapoti wachezaji, tofauti na ilivyokuwa mwanzo wakati wanacheza jijini Arusha mechi zao.
“Mashabiki zetu walitupa sapoti msimu uliopita tukiwa Championship na kupata tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara, hii ni fursa nyingine ya kuiona timu ikiwa uwanja wa nyumbani,” amesema Makata.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Mkenya Francis Baraza amesema anategemea mechi ngumu kutokana na wapinzani wao kuimarika zaidi, ingawa wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi, ili kutengeneza morali ya wachezaji wa kikosi hicho.