Maandalizi yaiva Simba, Yanga
Katibu wa Chama cha Soka mkoa wa Kigoma (KFA), Omary Gindi amesema maandalizi ya mchezo wa fainali kati ya Simba dhidi ya Yanga yanaendelea vizuri licha ya changamoto kadhaa ambazo wamekuwa wakipitia katika maandalizi ya uwanja huo.
"Maandalizi hasa ya Uwanja yamefikia hatua nzuri, tulikuwa na changamoto kidogo ya mgao wa maji ila kwa sasa kila kitu kinaenda vizuri, nina imani mpaka kufikia fainali yenyewe tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa kuelekea mchezo huo mkubwa hapa mkoani kwetu" alisema Gindi.
Aidha Gindi alisema kuwa kitendo cha mchezo huo kupigwa Kigoma utatoa fursa kwa wakazi wa mkoa huo katika suala nzima la kukuza uchumi na kutoa fursa mbalimbali ambazo zitapatikana kwa wakazi hao huku akiwasihi kujitokeza kwa wingi kushuhudia mtanange huo.
"Tumepata fursa kubwa kama mkoa ya kuandaa mechi kubwa hapa nchini ni wakati mzuri sana kwa wakazi wa Kigoma kupata fursa ya kukuza uchumi kwa wafanya biashara mbalimbali kujitokeza kwa wingi kutumia nafasi hiyo adhimu hapa kwetu" alisema
Gindi aliendelea kwa kusema kuwa hivi karibuni watapata ugeni wa maofisa wakaguzi kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kukagua uwanja huo na kujionea mwendendo mzima wa maendeleo ya uwanja huo kabla ya mchezo mwenyewe wa fainali.
"Julai 7 tutapata ugeni wa maofisa kutoka TFF lengo nikuja kuangalia hatua mbalimbali za uwanja ambazo tumefikia, na nina imani kubwa kutokana na jitihada ambazo kama mkoa tunazifanya wataridhika na maandalizi ya uwanja kwa ajili ya mchezo huo kwani tunafanya maandalizi ya kutosha ili kuhakikisha mchezo huo hauondolewi mkoani kwetu" alisema
Akizungumza kuhusu suala nzima la ulinzi wakati wa mchezo huo, Gindi alisema kuwa walikuwa na kikao na Serikali ya Mkoa wa Kigoma kuhusu kujadili suala hilo huku Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, akiahidi kutoa ulizi wa kutosha kwenye mchezo huo kuanzia ndani na nje ya uwanja.
"Mkuu wetu wa mkoa katuahidi kutupa ulinzi wa kutosha kwenye mechi hiyo hivyo niwatoe hofu wadau wa michezo nchini kuhusu suala nzima la ulinzi, nawasihi sana wapenzi wa soka kujitokeza kwa wingi uwanjani kufurahia burudani." alisema Gindi.
Mchezo wa fainali ya kombe la shirikisho la Azam (ASFC) kati ya Simba dhidi ya Yanga, utachezwa Julai 25 katika uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma ambao unaingiza mashabiki takribani 30,000.
IMEANDIKWA NA DAUDI ELIBAHATI, MWANASPOTI