Maajabu ya no 25 Azam VS Yanga

Muktasari:
Kesho Yanga SC na Azam FC zenye pointi 25 kila moja zinakutakana katika mchezo wa 25 kuzikutanisha Ligi Kuu ikiwa ni tarehe 25 pia.
Kila namba ina maajabu yake; kisayansi, kiimani, kiitikadi na hata kihistoria.
Leo nataka kujadili maajabu ya namba 25 ambayo kesho itakuwa na maana kubwa sana Tanzania kwenye ulimwengu wa michezo, hususan soka.
Kesho, Jumatano ya Novemba 25, Azam FC na Yanga SC zitakutana kwenye mchezo wao wa 25 wa Ligi Kuu Bara huku zote zikiwa na alama 25.
Ni Novemba 25
Ni mchezo wao wa 25.
Zote zina alama 25.
Zaidi ya mambo haya, namba 25 inawaunganisha wachezaji ambao wapo kikosini wakiwa wamezitumikia timu zote.
Kuna wachezaji wawili kwenye kikosi cha Azam FC ambao walicheza Yanga; Francis Chirwa na Frank Domayo.
Na kuna wachezaji watano wa Yanga SC ambao wamepita au kutokea Azam FC; Metacha Mnata, Ramadhan Kabwili, Farid Mussa, Ditram Nchimbi na Waziri Junior.
2 (Azam FC) na 5 (Yanga SC) = 25.
Ni mgongano huu wa matukio katika namba 25 ndiyo unanifanya niichambue zaidi namba hii na kukuletea maajabu yake.
NAMBA YENYEWE
Kwa mujibu wa mtandao wa Angel Numbers, 25 ni namba inayoshia mabadiliko.
Ikiwa ni kipeo cha pili na 5, 25 ni moja kati ya namba mbili tu ambazo kipeuo chake cha pili kinaishia na namba hiyohiyo...yaani 25² = 625. Namba nyingine ni 76.
MAAJABU YAKE
Namba hii ina maajabu yake katika nyanja tofauti tofauti za maisha.
I. Kidini
Desemba 25 ni sikukuu ya Krismasi ikiashiria kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Hii ni kwa imani ya Kikristo
Kwenye kitabu cha Ezekiel 40 : 1 - 48 : 35, mwandishi anautaja mwaka wa 25 kama mwaka alioziona nguvu za Mungu.
Lakini pia kwenye Quran tukufu, jumla ya manabii waliotaka ni 25, kwa mujibu wa imani ya kiislamu
II. Kisayansi (mtanisamehe mliokimbi sayansi)
Idadi ya atomic kwenye manganese (mn) ni 25.
Wastani wa vinasaba (DNA) vya mtu vinavyoendana na ndugu yake wa damu ni 25.
REKODI ZAO
Katika mapambano yao 24 yaliyopita kwenye Ligi Kuu, kila timu imeshinda mara 8, na zimetoka sare mara 8. Hakuna mbabe hadi hapo.
Lakini kwenye wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, ndipo Yanga wanapoumizwa.
Azam FC wamefunga mabao 31, Yanga wamefunga mabao 30. Hii ina maana kwamba Yanga wanazidiwa bao moja. Kwa hiyo mchezo wa kesho ni maalumu kwa kumpata mbabe baina yao ambaye atamzidi mwenzake kwa mabao na alama.
Kwa kuwa 25 ni namba ya mabadiliko, yawezekana kesho kukawa na mabadiliko yaani mbabe akapatikana.
MATOKEO ya MUDA WOTE
1. LIGI KUU
Zimekutana mara 24 tangu zikutane mara ya kwanza mwaka 2008.
Yanga imeshinda mara 8
Azam imeshinda mara 8
Wametoka sare 8
Yanga wamefunga mabao 30
Azam wamefunga mabao 31
2. MAPINDUZI CUP
Zimekutana Mara 5 tangu zikutane mara ya kwanza mwaka 2011
Makundi 2011: Yanga 2-1 Azam
Makundi 2012: Azam FC 3-0 Yanga
Makundi 2016: Yanga 1-1 Azam FC
Makundi 2017: Azam FC 4-0 Yanga
Makundi 2019 : Yanga 0-3 Azam FC
KOMBE LA KAGAME
Zimekutana mara 2 tangu zikutane mara ya kwanza mwaka 2012.
Fainali 2012: Yanga 2-0 Azam
Robo fainali 2015: Yanga 0-0 Azam (penalti 3-5)
NGAO YA JAMII
Zimekutana mara 4 tangu zikutane mara ya kwanza mwaka 2012
2013: Yanga 1-0 Azam
2014: Yanga 3-0 Azam
2015: Yanga 0-0 Azam (pen. 8-7)
2016: Yanga 2-2 Azam (pen. 1-3)
MECHI YA HISANI KUCHANGIA WALEMAVU
Zimekutana mara mara 1 mwaka 2011
Yanga 0-2 Azam FC
KOMBE LA SH IRIKISHO LA AZAM SPORTS
Zimekutana mara 1
Fainali 2016 : Yanga 3-1 Azam
VINARA WA MABAO
JOHN BOCCO
(Azam FC) Mabao 13.
-Ligi Kuu 10
-Mapinduzi Cup 2
-Mechi ya hisani kuchangia walemavu 1
KIPRE TCHETCHE
(Azam FC) Mabao 8
-Ligi Kuu 5
-Mapinduzi Cup - Mabao 3
DIDIER KAVUMBAGU
(Kotekote) - Mabao 5
-Ligi Kuu - 3 Mabao (Akiwa Yanga: Mabao 2 na akiwa Azam FC: Bao 1)
-Kombe la Shirikisho la Azam Sports (Azam FC) 1
HAMIS KIIZA (Yanga)
- Mabao 5
-Ligi Kuu - Mabao 4
-Kombe la Kagame 1
BONIFACE AMBANI
(Yanga) - Mabao 4
-Ligi Kuu - Mabao 4.
OBREY CHIRWA
(Kotekote) - Mabao 4
-Ligi Kuu 2 (Yanga)
-Kombe la Mapinduzi 2 (Azam FC)