Lukindo afichua jambo Namungo FC
Muktasari:
- Kasi hiyo inamfanya staa huyo wa zamani wa Mbao, KenGold na Tanzania Prisons kufikisha mabao matano nyuma ya kinara wa ufungaji Ligi Kuu, Anuari Jabir wa Polisi Tanzania mwenye saba.
WAKATI Namungo ikiendelea kupata matokeo mazuri katika Ligi Kuu Bara, imefichuka nyuma yake kuwapo nyota Helbert Lukindo ambaye amezidisha utamu akifunga mabao matatu katika michezo mitatu mfululizo, huku akianza kuisoma Simba kuandika rekodi mpya.
Kasi hiyo inamfanya staa huyo wa zamani wa Mbao, KenGold na Tanzania Prisons kufikisha mabao matano nyuma ya kinara wa ufungaji Ligi Kuu, Anuari Jabir wa Polisi Tanzania mwenye saba.
Lukindo amefunga mabao hayo mfululizo kuanzia Namungo iliposhinda 1-0 dhidi ya TRA United, kisha 2-1 dhidi ya Coastal Union na 1-0 mbele ya Polisi Tanzania akisaidia kupatikana pointi tisa na kuiweka timu hiyo nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 15.
Baada ya ushindi mfululizo wa mechi tatu kwenye dakika 270, Namungo inatarajia kushuka tena uwanjani Novemba 2, 2026 ugenini dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Bara, Simba ambayo haijapoteza mchezo wowote, ikifunga mabao 20 na kuruhusu manne.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lukindo amesema juhudi binafsi, utulivu na akili ya mpira ndio siri ya kung’ara kwake, lakini kufuata maelekezo ya benchi la ufundi linalomuamini kumpa nafasi.
Amesema msimu huu umeanza vyema kwake, akieleza kuwa kinachomuumiza zaidi ni majeraha ya mara kwa mara, lakini vinginevyo uwezo wake ni mkubwa, akiahidi kuipa makubwa zaidi Namungo.
“Nashukuru si mwanzo mbaya japokuwa inahitaji kuendelea kupambana kutokana na ugumu wa ligi na vita kali ya namba, nimeaminiwa lazima nifanye kazi yangu,” amesema Lukindo.
Winga huyo ameongeza kuwa, matarajio yake ni kuendelea kufunga mabao na lolote litakalojitokeza itakuwa ni mipango ya Mungu, akisisitiza kuwa kiu yake ni kuona timu ikitakata kila mchezo.
Ameongeza kuwa, kwa sasa wanaendelea kujipanga na mchezo ujao dhidi ya Simba, akieleza kuwa malengo yao ni kuendeleza ushindi ili kujiweka pazuri kwenye msimamo.
Amefafanua kuwa anafahamu ugumu na uwezo wa Simba haswa kuwa timu pekee hadi sasa ambayo haijapoteza mchezo wowote Ligi Kuu, akitamba kuwa huenda akawa wa kwanza kuwasimamisha wababe hao wenye ukuta mgumu.
“Mpira ni mchezo wa wazi, tunajua Simba ni timu kubwa na hawajapoteza hadi sasa, ila lolote linawezekana kwakuwa mkakati wetu ni kushinda kila mechi inayofuata, huenda tukawa wa kwanza kuwasimamisha,” ametamba Lukindo.