Lukindo aipa pointi tatu Namungo
Muktasari:
- Namungo ilipata penalti hiyo baada ya Rashid Chambo kuangushwa kwenye eneo la hatari katika dakika ya tano ambapo mwamuzi Isahaka Mwalile baada ya kujiridhisha kwenye teknolojia ya FVS aliamua kuipa Namungo pigo hilo lililowekwa kambani na Lukindo.
BAO moja alilofunga Herbert Lukindo kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 11 limeipa pointi tatu Namungo FC ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Namungo ilipata penalti hiyo baada ya Rashid Chambo kuangushwa kwenye eneo la hatari katika dakika ya tano ambapo mwamuzi Isahaka Mwalile baada ya kujiridhisha kwenye teknolojia ya FVS aliamua kuipa Namungo pigo hilo lililowekwa kambani na Lukindo.
Baada ya bao hilo, TRA United ilijaribu kusaka njia ya kurejea mchezoni, lakini Namungo iliendelea kuwa makini katika kulinda faida yake.
Hadi mwamuzi Mwalile anapuliza filimbi ya mwisho, bao hilo la Lukindo liliendelea kubaki katika mchezo huo, likiipa Namungo pointi tatu muhimu huku TRA United ikiondoka mikono mitupu.
Kwa upande wa TRA, huo ulikuwa mchezo wa pili kwa kocha Hemedi Suleiman ‘Morocco’ tangu alipokabidhiwa mikoba ya timu hiyo Septemba 10, 2026, akichukua nafasi ya Ettienne Ndayiragije. Morocco alianza kwa ushindi baada ya kuiongoza TRA United kushinda 3-1 dhidi ya Pamba Septemba 13.
Mechi yake ya pili akiwa ugenini amepoteza kwa Namungo inayofundishwa na kocha Juma Mgunda ambaye alikuwa kocha msaidizi wa Timu ya Taifa, Taifa Stars.