Prime
Libasse Gueye ashtua Simba!
UMEKIONA kiwango cha winga wa Simba, Libasse Gueye, jamaa ameanza kwa moto msimu wa 2026-2027 huku kocha wa kikosi hicho, Steve Barker akichekelea na kutuma salamu kwamba hakuna beki atakayekabana na kiungo huyo kisha kulala vizuri baadaye.
Gueye kwenye mechi mbili za Simba za Ligi Kuu Bara, ametengeneza mabao matatu kupitia asisti ambapo kati ya hizo, mbili ni kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Kagera Sugar katika ushindi wa 2-0, nyingine ilipocheza na Pamba Jiji, Wekundu wa Msimbazi wakishinda 2-1, zote zikichezwa ugenini.
Winga huyo raia wa Senegal, anakuwa mchezaji wa kwanza wa Simba msimu huu kubeba tuzo mbili za mchezaji bora wa mechi, hali inayoonesha ameuanza msimu kwa moto.
Kiwango hicho cha Gueye kimemuibua Kocha Barker, akiliambia Mwanaspoti kuwa, sio rahisi kwa beki yeyote atakayekutana na Gueye, kisha akawa bora kuliko winga huyo.
Barker amesema Gueye yuko kwenye kiwango bora akiendelea kutoka pale alipoishia msimu uliopita, ambapo kasi yake na mbinu za kuwatoka mabeki ndio vitu ambavyo vimekuwa vikiwapa wakati mgumu walinzi wengi.
Kocha huyo amesema anaamini msimu huu Gueye atakuwa na wakati bora kutokana na nishati yake ambapo amemtaka kuwa na muendelezo huo ili kuzidi kuipa mafanikio klabu hiyo.
“Libasse yuko kwenye kiwango bora, anafanya mambo kama ambavyo amekuwa akifanya siku zote mazoezini, ni winga hatari anapokuwa na mpira na anakwenda kwenye lango la wapinzani, kasi yake na mbinu zake ni silaha nzito sana,” amesema Barker.
“Unajua sio rahisi kwa beki akutane na Libasse kisha akaonekana beki amecheza vizuri kwa kumdhibiti, anastahili kupata tuzo ambazo amezipata kwenye mechi hizi mbili, ni mchezaji ambaye anapambana muda wote.
“Kitu anachotakiwa kufanya kwasasa ni kuwa na muendelezo huo wa kiwango chake, kama atafanya hivyo huu unaweza kuwa msimu wake bora zaidi akiwa hapa Tanzania na hilo linawezekiana kabisa.”
Msimu wa 2025-2026 ambapo Libase aliingia Simba kupitia usajili wa dirisha dogo la Januari 2026, alimaliza Ligi Kuu Bara akifunga mabao saba na asisti moja huku akiwa na mchango wa mabao manane.
Kwa namna ambavyo ameanza msimu huu, kuna uwezekano mchango wake wa mabao ukawa mkubwa zaidi kwani hadi sasa ana mchango wa mabao matatu akitoa asisti pekee, bado hajaanza kufunga.
Mbali na hilo, Barker amesema hivi sasa anashughulikia suala la nidhamu ya mchezo baada ya nyota wake wawili kuonyeshwa kadi nyekundu ambao ni David Kameta ‘Duchu’ na Ibraheem Jabaar.