Saluti ya Bakari Msimu kwa Mpanzu, Gueye
Muktasari:
- Kipindi hiki cha usajili wa dirisha kubwa, kumekuwa na taarifa nyingi za wachezaji kutoka timu moja kwenda nyingine, huku wengine wakiboresha mikataba yao sehemu walipo.
ULIPOTAMATIKA msimu wa 2025-2026 katika Ligi Kuu ya NBC, ndipo imeanza safari ya 2026-2027 huku dirisha la usajili likifunguliwa kuanzia Julai 6, 2026 na kutarajiwa kufungwa Agosti 15, 2026.
Kipindi hiki cha usajili wa dirisha kubwa, kumekuwa na taarifa nyingi za wachezaji kutoka timu moja kwenda nyingine, huku wengine wakiboresha mikataba yao sehemu walipo.
Kiungo mshambuliaji Bakari Msimu, amekuwa miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuhusishwa na usajili wa kwenda Simba kwa ajili ya msimu ujao, huku ikielezwa kwamba amesaini mkataba wa miaka miwili, ingawa mwenyewe hakutaka kabisa kuzungumzia suala hilo, akisisitiza kwamba hana nafasi ya kuzungumzia mipango ya klabu hiyo.
Msimu, ambaye alicheza katika kiwango cha juu kilichowavutia vigogo wa Simba kuonyesha nia ya kumsajili, amesema anaheshimu maamuzi ya viongozi wa klabu hiyo na kwamba wao ndio wanaowajua wachezaji wanaowahitaji.
Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, kiungo huyo ambaye ni zao la Coastal Union ya Tanga, iliyomlea tangu akiwa kwenye kikosi cha U-17 na baadaye U-20, amefunguka kuhusu safari yake ya soka, namna msimu uliopita ulivyombadilisha, pamoja na wachezaji anaowakubali ndani ya Ligi Kuu ya NBC.
Kiungo huyo amesema msimu wa 2025-2026 umekuwa wa kipekee kwake kutokana na mafanikio aliyoyapata binafsi ndani ya uwanja na maendeleo makubwa aliyopiga katika maisha yake ya soka.
“Kwangu utabakia kuwa msimu uliyonipa hatua kubwa katika safari ya maisha yangu ya soka, kucheza mechi nyingi kumenijengea kujiamini, nidhamu na kunikomaza kiakili jinsi ya kuishi kama mchezaji mwenye ndoto kubwa,” anasema Msimu.
Kiungo huyo alipandishwa kuichezea timu ya wakubwa ya Coastal Union katika msimu wa 2023-2024, hivyo tayari ameshacheza misimu mitatu katika Ligi Kuu ya NBC, jambo analosema limempa uzoefu mkubwa wa kukabiliana na changamoto za ushindani.
Anasema hakupata nafasi kirahisi mwanzoni mwa msimu wa 2025-2026, kwani alianza akiwa mchezaji wa akiba, lakini hakukata tamaa. Kupitia bidii yake binafsi na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi, aliweza kujihakikishia nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.
“Nina elimu ya kawaida, hivyo lazima niweke bidii katika kazi ninayoona ndiyo chanzo cha kipato cha kuendesha maisha yangu, pamoja na kwamba sikuanza kwa kupata nafasi, niliamini kujituma kutanipa matunda na imekuwa hivyo,” anasema kiungo huyo ambaye msimu wa 2024-2025 aliteuliwa kuwa nahodha wa Coastal Union na alimaliza akiwa na mabao manne na asisti tatu.
MAKOCHA WALIOMBEBA
Msimu anasema mafanikio aliyoyapata hayawezi kutenganishwa na mchango wa makocha mbalimbali waliompitia katika safari yake ya soka. Kwa mujibu wake, kila mmoja alimjengea kitu tofauti, lakini wote walikuwa na msisitizo mmoja mkubwa ambao ni nidhamu.
Anasema amejifunza mambo mengi mikononi mwa Mwinyi Zahera aliyempandisha timu ya wakubwa msimu wa 2023-2024, pamoja na David Ouma, Juma Mwambusi, Joseph Lazaro, Ali Mohammed Ameir na Mohamed Muya.
Kwa mujibu wa Msimu, makocha hao walimfundisha kwamba kipaji pekee hakitoshi kufanikiwa katika soka la ushindani, bali nidhamu ndiyo msingi wa mafanikio ya muda mrefu. Alipoulizwa kama nidhamu hiyo ndiyo iliyochangia yeye kutajwa kuwania kusajiliwa na Simba, Msimu alikataa kuingia katika mjadala huo.
“Simba tena, hapana sitaki kabisa kuzungumzia mambo ya Simba, kwani viongozi wa timu hiyo wao ndio wanaowajua wachezaji wao siyo mimi,” anasema.
ANAOWAKUBALI
Ingawa hakutaka kuzungumzia usajili wake unaodaiwa kuelekea Simba, Msimu hakuwa na kigugumizi kuelezea maoni yake kuhusu baadhi ya nyota wa klabu hiyo na wengine wanaocheza Ligi Kuu ya NBC.
Alipotakiwa kutoa tathmini yake kuhusu kiwango cha Libase Gueye aliyefunga mabao saba na Elie Mpanzu (mabao saba na asisti 10), Msimu alisema wote ni wachezaji wenye uwezo mkubwa.
“Ni wachezaji wazuri wenye uwezo mkubwa, wapo wachezaji wengi ninao wakubali,” anasema.
Hakusita kuongeza majina mengine ya mastaa ambao kwake wamekuwa wakimvutia kutokana na namna wanavyoutumia ubora wao ndani ya uwanja.
“Ukiondoa hao namkubali Pacome Zouzoua na Clatous Chama jinsi ambavyo wanacheza kwa kutumia akili kubwa, pengine kuliko nguvu, wanafanya mpira wa miguu uonekane rahisi,” anabainisha.
AMTAJA SAMATTA
Mbali na kuzungumzia mastaa anaowakubali, Msimu pia amefichua mchezaji ambaye amekuwa akimpa hamasa tangu akiwa mtoto.
Kwa mujibu wake, Mbwana Samatta, ndiye aliyemjengea ndoto ya kuamini kwamba inawezekana mchezaji wa Tanzania kufika mbali katika soka la kimataifa.
Anasema historia ya Samatta imekuwa somo kubwa kwa vijana wengi wanaotafuta mafanikio kupitia soka.
“Historia ya Samatta ni yakuvutia na halisi kwetu sisi vijana wa Kitanzania kama amezaliwa Mbagala, halafu kacheza timu kubwa nje kama Aston Villa, Genk, PAOK, Le Havre na zingine, imetufanya wengi kuamini katika kupambana na sasa tumefika hatua hii,” anasema.
Kwa mtazamo wake, bado Tanzania ina vipaji vinavyoweza kufika katika viwango vya juu zaidi nje ya nchi ikiwa vitapata mazingira sahihi.
KUHUSU FEI TOTO
Msimu anamwelezea kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, kuwa ni mmoja wa wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza soka la kiwango cha juu nje ya Tanzania.
“Fei Toto ana kipaji cha aina yake, ndiyo maana tunasikia kila siku, Simba Yanga zinatamani huduma yake,” anasema.
SAFARI YAKE
Akizungumzia safari yake ya soka, Msimu anasema alianza kucheza mpira wa mitaani kama vijana wengi wa Kitanzania, lakini Coastal Union ndiyo klabu iliyompa nafasi ya kwanza ya kucheza soka la ushindani na kujitengenezea jina.
Anasema kupitia mfumo wa maendeleo ya vijana wa Coastal Union alipitia timu za U-17 na U-20 kabla ya kupandishwa katika kikosi cha wakubwa, hatua iliyokuwa mwanzo wa kutimiza ndoto zake.
“Coastal ndio timu ya kwanza kucheza na ndiyo imenionyesha kwa Watanzania, hivyo soka la ushindani nimejifunza kuanzia timu ya vijana U-17 na U-20 hadi nikapandishwa timu ya wakubwa msimu wa 2023/24.”
Mbali na mafanikio yake katika ngazi ya klabu, Msimu pia amekuwa sehemu ya mafanikio ya timu za taifa za vijana.
Mwaka jana alikuwa miongoni mwa nyota wa Ngorongoro Heroes walioiwezesha Tanzania kutwaa ubingwa wa CECAFA U-20 baada ya kuifunga Kenya kwenye mchezo wa fainali, mafanikio yaliyoongeza thamani yake na kumweka kwenye rada za klabu mbalimbali zinazohitaji huduma yake.
Licha ya tetesi zinazoendelea kuhusu mustakabali wake, Msimu ameonyesha wazi kwamba kwa sasa ameweka nguvu zaidi katika kuendelea kufanya kazi kwa bidii, huku akiacha uamuzi wa usajili ubaki mikononi mwa viongozi wa klabu zinazomuhitaji.