Prime
Libasse Guèye aliamsha Simba
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Libasse Guèye, amesema ushindi wa mechi tano mfululizo katika Ligi Kuu Bara umeipa timu hiyo nguvu na kujiamini kuelekea mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kesho Jumapili dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi.
Simba imekuwa katika mwenendo mzuri kwenye michezo ya ligi, jambo ambalo limeifanya timu hiyo kuingia kwenye kibarua cha kimataifa ikiwa na morali kubwa baada ya kuanza msimu kwa matokeo yanayoridhisha.
Guèye ambaye tayari amefunga bao moja na kutoa asisti tano katika ligi, amesema mwenendo huo umekuwa sehemu muhimu ya maandalizi yao kuelekea mchezo huo ambao utawapa picha ya uwezo wao katika hatua ya kimataifa.
“Ushindi wa mechi tano mfululizo umetupa kujiamini zaidi na umetufanya kuwa tayari kwa mchezo huu. Tunajua Ligi ya Mabingwa ni mashindano tofauti, hivyo tunapaswa kuwa makini na kupambana kwa dakika zote,” amesema Guèye.
Hata hivyo, kazi iliyo mbele yao si nyepesi kutokana na kukutana na Mighty Wanderers, moja ya klabu zenye historia kubwa katika soka la Malawi na ambayo imekuwa sehemu muhimu ya ushindani wa soka la nchi hiyo kwa muda mrefu.
Wanderers ilianzishwa mwaka 1962 jijini Blantyre na ni moja ya klabu kongwe Malawi, ikiwa imetwaa ubingwa wa Super League ya Malawi mara saba.
Guèye anaamini maandalizi mazuri na umakini wa kikosi ndio vitakuwa silaha muhimu kwa Simba katika kuhakikisha inaanza safari yake ya kimataifa kwa matokeo mazuri.
“Tunawaheshimu wapinzani wetu, tunajua wana historia yao na wanacheza nyumbani, lakini sisi tumejiandaa vizuri. Tumekuja Malawi kwa malengo yetu na tunataka kuonyesha uwezo wetu,” amesema.
Mchango wa Guèye pia unaweza kuwa muhimu katika mchezo huo kutokana na uwezo wake wa kutengeneza nafasi, jambo linaloonekana kupitia asisti zake tano alizotoa kwenye mechi tano za ligi hadi sasa.
Simba ilianza msimu huu wa 2026/27 kwa kupoteza bao 1-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kabla ya kushinda mechi tano mfululizo katika ligi kwa kuzichapa Kagera Sugar (2-0), Pamba Jiji (2-1), Singida Black Stars (2-1), Coastal Union (1-0) na Geita Gold (2-0).