LECHANTRE Mambo yake makubwa aisee
Muktasari:
- Kocha Lechantre aliyetua nchini mapema mwaka huu ili kuchukua nafasi ya Joseph Omog aliyetimuliwa katikati ya msimu na kupewa mkataba wa miezi sita tu.
MWANDISHI WETU. NI kweli kwa sasa zinahesabiwa saa tu kwa ndoa kati ya Kocha Pierre Lechantre na klabu ya Simba kuvunjwa rasmi.
Kocha Lechantre aliyetua nchini mapema mwaka huu ili kuchukua nafasi ya Joseph Omog aliyetimuliwa katikati ya msimu na kupewa mkataba wa miezi sita tu.
Mkataba huo umemalizika na bado mabosi wa Simba hawajampa mkataba mpya na kumfanya Mfaransa huyo kuzira na kurudi jijini Dar es Salaam kutoka Nakuru Kenya, timu ilipokuwa ikishiriki michuano ya SportPesa Super Cup.
Lechantre alikuwa anasubiri hitimisho la michuano ya SportPesa ambapo jana Simba ilikuwa ikivaana na Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wa fainali, ili ajue kama atabaki Msimbazi ama la!
Hatma ya kocha huyo ipo mikononi mwa Bilionea Mohammed Dewji aliyefanya naye mazungumzo ya awali na kushindwa kuafikiana na kuahidiana kumalizana baada ya fainali hizo za SportPesa.
Leo Jumatatu kocha huyo atakuwa katika sherehe za tuzo za klabu ya Simba na pia ana mpango wa kula Idd El Fitri, lakini Mwanaspoti inakuletea kwa ufupi takwimu za Mfaransa huyo namna miezi yake Simba ilivyobamba.
MSHAHARA WA HESHIMA
Lechantre aliyetambuliwa na mabosi wa Simba Januari 19, alipoingia mkataba wa kuinoa timu hiyo ameweka rekodi Msimbazi ya kuvuta mkwanja wa nguvu kama mshahara wake kwa kila mwezi.
Chanzo kutoka ndani ya Simba linadokeza kuwa, Lechantre na Msaidizi wake Aymen Mohammed Habib aliyetua naye Msimbazi, kwa mwezi wanavuta si chini ya Sh 45 milioni kwa kila mwezi ikiwa na maana katika muda aliokaa amevuta mkwanja wa kutosha.
Katika muda wote aliokuwa Msimbazi, Kocha Lechantre amevuta si chini ya Sh 225 milioni.
USINGIZI WAKE BALAA
Tangu Lechantre alivyotua nchini amekuwa akiishi katika hoteli ya Golden Tulip iliyopo Dar es Salaam, lakini mapema Februari alihama hotelini hapo na kupelekewa Sea Scape iliyopo Kundundi alipokodishiwa Apatimenti ambayo kwa siku moja akipiga mbonji tu analipiwa Sh200,000.
Mpaka unasoma hapa, Lechantre atakuwa amekaa katika hoteli hiyo kwa siku 131 na kuitia Simba gharama isiyopungua Sh 26 milioni.
REKODI YAKE TAMU
Lechantre ameiongoza Simba katika mechi 15 za Ligi Kuu Bara bila kusahau nne za mechi za kimataifa za Kombe la Shirikisho Afrika na moja ya Kombe la Sportpesa.
Katika mechi 15 za Ligi Kuu akiwa Kocha Mkuu, Simba imeshinda mechi 10 kupoteza moja na kutoka sare nne.
Lechantre iliisaidia Simba kufunga mabao 30 katika mechi hiyo ikiwa ni sawa tu na yale aliyoyaacha Mcameroon, Joseph Omog na Masudi Djuma aliyeiongoza kwa muda Simba kabla ya kumpisha Mfaransa huyo.
Chini ya Lechantre Simba imefungwa mabao saba kati ya 15 ambayo timu hiyo iliruhusu kwa msimu mzima.
TAJI LA KIHISTORIA
Hakuna asiyejua kama Simba kwa misimu mitano ilikuwa inatoka kapa katika Ligi Kuu kabla ya safari hii chini ya Lechantre kubeba taji tena mapema kabla ligi haijamalizika.
Simba ilikuwa imebeba taji la mwisho mwaka 2012 na miaka sita ilikuwa ikihaha kulisaka kabla ya Mfaransa huyo kuwapa taji la kihistoria wakiwapoka watani zao wa Yanga waliokuwa wakilisaka kwa mara ya nne mfululizo thamani yake ni zaidi ya Sh 85 milioni.
KAGERA YAMPIGA TOBO
Lechantre huenda akaondoka Msimbazi akiiwaza Kagera Sugar iliyomtibulia kwa kuifunga Simba siku ya kukabidhiwa taji lao na Rais wa Tanzania, John Magufuli.
Hiyo ndiyo iliyokuwa mechi pekee kwa kocha huyo kuiona Simba ikipoteza akiwa kama Kocha wa timu hiyo katika Ligi Kuu na hata kwenye mechi nyingine za kimataifa.
NDINGA LAKE SASA
Mfaransa huyo msimchukulie poa kabisa, kwani licha ya kuonekana ghali katika malipo, lakini pia hata gari analotumia tangu atue nchini nalo sio la mchezo mchezo kwani anaendesha Honda CRX la mwaka 2007 lenye thamani si chini ya Sh 40 milioni.
MSIKIE MSOLLA
Kocha wa zamani wa Taifa Stars Dk. Mshindo Msolla, anasema timu za Tanzania hasa Simba na Yanga, huwa hazifanyi uchunguzi mzuri kabla ya kuleta makocha wa kuzifundisha timu zao.
Dk Msolla anasema ili klabu hizo ziweze kufanikiwa ni lazima ziwe na makocha wa hadhi ya kina Lechantre, lakini gharama zao huwa sio nyepesi kama wanavyofikiria.
“Simba na Yanga ndio maana zinashindwa kumudu au kukaa na makocha kwa muda mrefu kwa vile hazifanyi uchunguzi makini wa makocha wanaowahitaji ila si jambo zuri kwa timu ambayo inataka mafanikio kushindwa kukaa na kocha wake kwa muda mrefu,” anasema Dk. Msolla akirejea tukio la Simba kutaka kuachana na Lechantre.