Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kumekucha... Yanga yacheza akili kubwa

Muktasari:

  • ASIKWAMBIE mtu, kushinda vita kubwa kunahitaji akili kubwa. Hicho ndicho Yanga inachojaribu kufanya kwenye vita yao ya kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

ASIKWAMBIE mtu, kushinda vita kubwa kunahitaji akili kubwa. Hicho ndicho Yanga inachojaribu kufanya kwenye vita yao ya kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Katika ratiba ya awali, Yanga mechi yao ijayo ilikuwa Aprili 30 dhidi ya watani wao wa jadi, Simba uwanjani kwa Mkapa.

Imechungulia na kuona ingekuwa soo, hivyo imewasilisha maombi ya kucheza mechi moja ya ligi kabla ya kuwakabili Simba.

Unajua Yanga imecheza akili kubwa kiasi gani kwa kuomba kucheza mechi moja ya ligi kabla ya kuwakabili Simba?

Cheki msimamo. Yanga ipo kileleni kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya Simba, ikiwa na pointi 51 baada ya mechi 19.

Nyuma yao kwenye nafasi ya pili, wapo mahasimu wao wakuu, Simba na pointi 41, nao wamecheza mechi 19. Vigogo hao wawili ndio wanaochuana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu huu.

Na Yanga itashuka uwanjani kuwakabili Namungo ikifahamu umuhimu mkubwa wa mchezo huo. Inafahamu inahitaji kuvunja miiko kwenye mchezo huo ili kujiweka pazuri. Yanga haijawahi kupata matokeo ya ushindi dhidi ya Namungo kwenye ligi, lakini hesabu zinawaweka wazi, wanafahamu wakishinda pengo la pointi dhidi ya Simba litakuwa 13, hiyo itakuwa na faida kubwa zaidi kwa upande wao. Wakitoka sare pengo litakuwa pointi 11 na wakipoteza litabaki kuwa pointi 10, huku Simba wao wakiwa nyuma kwa mchezo mmoja.

Na kama ingesubiri kucheza na Simba Aprili 30, basi ushindi ungewafanya kuweka pengo la pointi 13, sare pointi 11, lakini kichapo kingefanya pengo la pointi kushuka na kuwa saba. Na bado mechi 10 mbele. Presha ingekuwa kubwa upande wao.

Kitu ambacho Yanga itapigana kwa kila namna ni kukwepa kipigo kwenye mechi ya Namungo. Ushindi utawafanya waingie uwanjani kuwakabili Simba watakaokuwa wametoka kucheza mechi ngumu ugenini Afrika Kusini wakiwa juu kwa pointi 13.

Hivyo ushindi kwenye mechi ya watani itawafanya waweke pengo la pointi 16 na hapo watahitaji kushinda mechi tano tu kati ya tisa zitakazokuwa zimebaki kubeba ubingwa bila kujali kiporo cha wapinzani. Sare itafanya pengo la pointi kuwa 14 na Simba hata ikishinda kiporo chake pengo litabaki kuwa pointi 11.

Wakishinda dhidi ya Namungo na kupoteza kwa Simba, pengo litakuwa pointi 10 na kusikilizia matokeo ya kiporo cha Simba yatakavyokuwa. Na hapo kutakuwa na mechi tisa za kucheza mbele sawa na pointi 27. Simba ikishinda kiporo chake, Yanga itahitaji kushinda mechi saba kati ya tisa kumaliza kazi. Lakini, kama kiporo cha Simba kikiisha kwa sare, Yanga itahitaji kushinda mechi sita na kama itapoteza, basi itahitaji mechi tano kufunga msimu. Ni mchezo wa hesabu tu. Lakini, kila kitu kinaanzia Jumamosi hii kwenye mchezo wa Namungo uwanjani wa Mkapa.

Kigezo chao cha kuomba icheze mechi moja kabla ya kuwakabili Simba ni kuona wangekuwa mapumziko ya muda mrefu bila ya kucheza mechi, wakati Simba watakuwa fiti kimchezo kwa kucheza mechi dhidi ya Orlando Pirates kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF) kabla ya kipute hicho chao cha watani.

Ombi la Yanga limekubaliwa na sasa watakipiga na Namungo Jumamosi hii kwa Mkapa.


MAKOCHA

Akizungumzia ushindani baina ya timu hizo kuelekea ubingwa wa ligi, kocha mkongwe nchini Abdul Mingange alisema mechi ya Namungo na Yanga ni faida kwa Yanga ambayo ina mechi muhimu Aprili 30.

“Kwa utaratibu wa mpira inatakiwa mkiwa kwenye mashindano kila baada ya siku tatu mpaka nne mnacheza mechi,” alisema Mingange.

“Yanga kama isingecheza na Namungo na kuendelea kujifua ikisubiri mechi ya Simba isingekuwa na afya kwao hasa kwa wachezaji kutunza utimamu kwa kufanya mazoezi.”

Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza alisema mechi hiyo itamsaidia kocha wa Yanga kuangalia viwango vya wachezaji wake waliotoka kwenye majeruhi.

“Itamsaidia kocha kuangalia ‘mechi fitinesi’ ya wachezaji wake kuelekea kwenye mechi yao ya Aprili 30,” alisema.

“Hii ni faida kwao tofauti na wangekaa muda mrefu bila kucheza mechi wakiisubiri Simba ambayo itakuwa imetoka kucheza mashindano ya kimataifa, hivyo mechi na Namungo itaisaidia Yanga kujiweka fiti kabla ya kuikabili Simba.”