Kondo akomalia washambuliaji Bandari Tanzania
Muktasari:
- Bandari ilimaliza vinara kundi A na pointi 32, katika Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2025-2026, baada ya kushinda mechi 10, sare mbili na kupoteza mbili kati ya 14, iliyocheza, huku ikifunga mabao 25 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa tisa.
KOCHA Mkuu wa Bandari Tanzania, Habibu Kondo amesema licha ya kiwango kinachoendelea kuonyeshwa na timu hiyo hadi sasa, ila bado hajaridhishwa na eneo la ushambuliaji, jambo analoendelea kulifanyia kazi kabla ya kuisha kwa raundi ya kwanza.
Kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Azam FC, Coastal Union, Majimaji, Mbeya Kwanza na timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 18 (U-18), amesema kwa kila mechi kuna wastani wa kutengeneza nafasi nne hadi tano, ila umaliziaji bado ni tatizo.
"Kinachonifurahisha ni kuona nafasi tunatengeneza zaidi na kilichobakia kwa sasa ni kuangalia namna nzuri ya kuzitumia, kwa sababu mwenendo wa ligi umekuwa ni mgumu sana na utaendelea kutokana na mahitaji ya kila mmoja wetu," amesema Kondo.
Kocha huyo amesema malengo ya timu hiyo ni kupanda daraja na kwenda kushiriki Ligi Kuu Bara, jambo ambalo wanaendelea kulipigania, licha ya ushindani mkali kutoka kwa wapinzani wao, hususani kwa mechi za ugenini ambazo huwa ndizo ngumu.
Timu hiyo ya Mtwara, imecheza mechi 11, za Championship, ikishinda tano, sare tatu na kupoteza pia tatu na safu ya ushambuliaji imefunga mabao 12 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita, huku ikiwa nafasi ya nne na pointi zake 18.
Bandari ilimaliza vinara kundi A na pointi 32, katika Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2025-2026, baada ya kushinda mechi 10, sare mbili na kupoteza mbili kati ya 14, iliyocheza, huku ikifunga mabao 25 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa tisa.