Kocha Zimamoto afichua siri ZPL
Muktasari:
- Bares amefichua hayo hivi karibuni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Zimamoto katika mwendelezo wa Ligi Kuu Zanzibar, mechi iliyochezwa Septemba 11, 2026.
KOCHA Mkuu wa Zimamoto, Abdallah Mohammed ‘Bares’ amesema kutokana na malengo yake ya kuhitaji ushindi kila mechi anayocheza, amekuwa akiingia kwa mitindo tofauti ili mpinzani asimsome kirahisi.
Bares amefichua hayo hivi karibuni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Zimamoto katika mwendelezo wa Ligi Kuu Zanzibar, mechi iliyochezwa Septemba 11, 2026.
“Binafsi huwa natamani kupata ushindi kwa kila mechi iliyopo mbele yangu ndio sababu ya kuja na mpango kazi na mkakati mpya ili mpinzani iwe ngumu kunielewa,” amesema.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Mao kisiwani Unguja, mabao ya Zimamoto yalifungwa na Rashid Said dakika ya 17 na Samson Emmanuel dakika ya 89.
Kocha huyo amesema licha ya ushindi huo, lakini kikosi chake hakikuwa kwenye kiwango kizuri cha uchezaji.
Amesema hali hiyo hutokana na wachezaji kuwa na presha kubwa ya mchezo, ingawa hutumia fursa hiyo kuwatuliza ili wasipoteze.
“Kuna wakati timu inapoteza umakini kwa kushindwa kufanya ambacho kinastahili kwa muda huo, lakini hawatoki nje ya mpango kazi tuliouweka,” amesema Bares.
Hadi kufikia sasa, Zimamoto imecheza mechi tatu za ligi hiyo ikishinda mbili, sare moja, haijapoteza, huku ikikusanya pointi saba ikiwa nafasi ya tano ya msimamo wa ligi hiyo kabla ya mechi za jana.
Kwa sasa Zimamoto inajiandaa kuikabali Wembe, mechi itakayochezwa Septemba 26, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.