Pointi nne zampa jeuri kocha Wembe
Muktasari:
- Katika mechi hizo nne za ugenini ilizocheza kisiwani Unguja, Wembe inayotokea Pemba imeshinda moja, sare moja na kupoteza mbili, huku ushindi wao wa kwanza wa msimu ukiwa ni wa mabao 2-0 dhidi ya Black Sailors.
KOCHA wa Wembe, Said Mbarouk amesema pointi nne walizovuna katika mechi nne za Ligi Kuu ya Zanzibar walizocheza Unguja si matokeo mabaya, akisisitiza ni ishara ya mwanzo ya mkakati wao wa kushindana ugenini kuanza kuzaa matunda.
Katika mechi hizo nne za ugenini ilizocheza kisiwani Unguja, Wembe inayotokea Pemba imeshinda moja, sare moja na kupoteza mbili, huku ushindi wao wa kwanza wa msimu ukiwa ni wa mabao 2-0 dhidi ya Black Sailors.
Mbarouk amesema matokeo hayo yanapingana na dhana timu zinazotoka Pemba huwa zinapata wakati mgumu zinapokwenda kucheza Unguja na maandalizi mazuri na mpango sahihi wa mechi vinaweza kuziwezesha kupata matokeo.
Amesema Wembe iliingia katika mechi dhidi ya Black Sailors ikiwa na malengo yaliyowazi na mpango maalumu wa namna ya kumkabili mpinzani, jambo alilowataka wachezaji kulitekeleza kwa umakini ndani ya uwanja.
"Wembe iliingia katika mchezo huo ikiwa na malengo yaliyowazi na mpango wa namna ya kukabiliana na mpinzani, jambo ambalo niliwataka wachezaji kulitekeleza kwa umakini ndani ya uwanja. Hatukuja kubahatisha," amesema.
Kocha huyo amesema jambo kubwa walilolenga ni kuhakikisha wachezaji wanafuata maelekezo ya benchi la ufundi na kutekeleza kwa nidhamu mfumo waliouandaa kabla ya mchezo.
Ameongeza, mafanikio ya timu hayawezi kuhusishwa na kucheza nyumbani au ugenini pekee, bali yanategemea zaidi maandalizi, nidhamu ya wachezaji na uwezo wa kutekeleza mpango wa mchezo.
Mbarouk pia amezitaka timu nyingine zinazotoka Pemba kutokuwa na hofu zinapokwenda Unguja na hazipaswi kujikita katika kujilinda pekee, bali kuamini uwezo wao na kucheza kwa mpango unaoweza kuwapatia matokeo.
Wembe inatarajiwa kushuka dimbani Septemba 20, 2026 dhidi ya Zimamoto kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba na benchi la ufundi la timu hiyo limelenga kuimarisha maeneo ambayo bado yanaonekana kuwa na upungufu ili timu hiyo iendelee kuwa bora.