Prime
Kocha afichua Mwalimu alivyowaua Gaborone United
SHABIKI wa Yanga kuanzia juzi usiku kama kuna staa amewafanya kutamba ni mshambuliaji, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ baada ya kufunga bao ambalo limepeleka masikitiko kwa wapinzani. Sasa kocha mmoja wa Kizungu amefunguka juu ya staa huyo alivyofanikiwa kuwaadhibu.
Gomez aliifungia Yanga bao la kwanza la Kimataifa, akiisawazishia wakati ikilazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Gaborone United, kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha wa Gaborone United, Sean Connor, aliliambia Mwanaspoti, walifanya kazi kubwa ya kuwajua Yanga lakini kuna kosa lilifanyika kwa kukosa taarifa za kutosha kuhusu Gomez ambaye aliingia kutokea benchi.
Connor raia wa Ireland Kaskazini, amesema wakati wanakusanya taarifa kuhusu Yanga hususan wachezaji wa mabingwa hao, walipata karibu kila kitu lakini hawakujua ubora wa Gomez ambaye alikuwa anaonekana muda mwingi anatokea benchi.
“Kuna kosa moja tulifanya kwenye maandalizi yetu, wakati tunakusanya taarifa za Yanga, tulipata kila taarifa kuhusu wachezaji wao kuanzia wale ambao wamekuwa wanacheza mechi tano zilizopita n ahata wale ambao walikuwa wanatokea benchi,” amesema Connor.
“Huyu mshambuliaji anayevaa jezi namba 30 (Gomez) tulimuona kwenye mechi moja aliingia lakini bado hatukuwa na taarifa za ubora wake zaidi na bahati mbaya ndiye aliyekuja kufanya kitu tofauti.
Connor ameongeza, walifanikiwa kumdhibiti Peter Shalulile lakini kama wangejua ubora wa Gomez wangetafuta mbinu za kukabiliana naye.
“Ana ubora mkubwa sana (Gomez) angalia namna alivyoomba mpira akiwa katikati ya mabeki na kujitengenezea njia sahihi ya kwenda kushambulia, alifunga bao ambalo anafunga mshambuliaji mwenye ubora na bahati mbaya zaidi kipa wetu akashindwa kukabiliana na shuti lake,” amesema.
Yanga kwenye bao hilo ilianza kugongeana vizuri, pasi ya Maxi Nzengeli ikapasua katikati na kumkuta Mudathir Yahya, ambaye aligusa kwa kisigino kwenda kwa Gomez ambaye akiwa katikati ya mabeki, akauchukua mpira kwa mguu wa kulia kisha kweda kufunga na mguu wa kushoto.
Hilo linakuwa bao la kwanza kwa Gomez tangu atue kikosini hapo msimu huu kwa mkopo akitokea Wydad Casablanca, pia la kwanza kwa timu hiyo katika mechi za kimataifa.