Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nazielewa hasira za Clatous Chama dhidi ya Yanga

JICHO Pict


AMEUFUNGUA moyo. Labda alihitaji kusema ili ajisikie vizuri. Clatous Chota Chama majuzi alikuwa akipiga stori na Fatma Dewji, mdogo wa tajiri wa timu yake Simba, Mohamed Dewji na akafunguka mengi kuhusu uhamisho wake wa kwenda Yanga.


Nilitazamia awe na hasira na Yanga. Na hiki ndicho alichokidhihirisha wakati anaongea na Fatma. Kuna mambo machache hajaeleweka lakini mengine ameeleweka. Suala la kwamba alilazimishwa kusaini Yanga sidhani kama lina ukweli.


Chama ni mtu mzima na hakushikiwa Bastola wakati anasaini. Hakushikiwa panga. Alikuwa anatimiza maandiko tu kwamba baada ya ghasia za siku nyingi Yanga walikuwa wamefanikiwa kumpata mtu wao.

Kwamba anajuta kwenda Yanga. Hili ni kweli. Ilikuwa lazima ajute. Yanga ‘walimdhalilisha’ Chama. Walimchukua akiwa lulu pale Msimbazi wakampeleka katika timu yao na kumuonyesha kwamba licha ya kuwa alikuwa muhimu Simba lakini kwao hakuwa na umuhimu wowote ule.

Chama alipaswa kulipima hili mapema. Yanga walikuwa na Pacome Zouzoua, Aziz Ki na Maxi Nzingeli. Alipaswa kujua kwamba maisha yake Jangwani yasingekuwa kama Msimbazi. Ilipaswa kuwa akili ya kawaida tu.

Wazungu wana msemo wao kwamba ‘Grass is not always greener on the other side’. Sio kila mahala kuna malisho mema. Tatizo ushawishi wa Yanga ulikuwa mkubwa kwake na hakuja sana maumivu ambayo angewaachia Wanasimba. Hili ni bila ya kujali ambacho angekutana nacho Jangwani.

JICH 01

Alihitaji maamuzi magumu ya kuendelea kubakia Simba na kuitumikia kwa nguvu zote. Katika hili anapaswa kujilaumu zaidi yeye mwenyewe. Kuna wakati unaridhika na ulipo. Unachukua mshahara mzuri huku ukiendelea kuwa mfalme wa timu.

Antoine Griezamann alikuwa mfalme pale Atletico Madrid. Akaamua kwenda kujitumbukiza katika Barcelona yenye Lionel Messi na mastaa wengine. Umuhimu wake ukatoweka. Mwishowe akaamua kugeuza zake Atletico. Mifano kama hii ipo mingi.

Kwamba mara baada ya kusaini tu mkataba alimuomba Injinia Hersi Said asiichezee Yanga na Simba walikuwa wamemuita Dubai kwenda kukutana na tajiri Mohamed Dewji ukweli ni kwamba hapa Chama mwenyewe alikuwa anaonyesha hakuwa na msimamo.

JICH 02

Lakini pia linatudhihirishia kwamba Simba huwa wanachelewa sana katika suala la maamuzi ya usajili. Kuanzia wachezaji wanaotaka kuingia klabuni hadi wale ambao wangependa wawaongezee mikataba mipya.

Sidhani kama Simba walikuwa na msimamo kamili kuhusu Chama. Kuna wale ambao walitaka aendelee kubaki na kuna wale ambao walitaka aondoke kwa madai kwamba alikuwa anatumika na Yanga. Yeye na Aishi Manula walikuwa wana uhusiano wa mashabiki na watu wa Simba.

Labda ndio maana mpaka wakati anaanza mazoezi na Yanga watu wa Simba hawakuwahi kumpa Chama ‘Thank you’ katika ukurasa wao wa Instagram tofauti na wachezaji wengine ambao walikuwa wameondoka klabuni hapo.

JICH 03

Kitu kingine ambacho ni wazi lazima Chama aichukie Yanga ni ukweli kwamba mwishoni mwa msimu wake wa kwanza tu waliamua kutoendelea naye. Waliamua kutomuongezea mkataba mpya.

Hii ilikuwa inamaanisha nini? Kwamba Yanga walikuwa wametangaza rasmi kuwa Chama ameisha. Kwanza kabisa kwa namna ambavyo Chama alikuwa lulu hakupaswa kupewa mkataba wa mwaka mmoja Yanga. Lakini wao walimpa mkataba wa mwaka mmoja.

Lakini pili baada ya huo mwaka kwisha Yanga wakatangaza kutomuongezea mkataba. Hili lilikuwa linawaweka katika mtego Simba na Azam. Kwamba Yanga walikuwa na viwango vya hali ya juu kiasi cha kumuona Chama hafai. Kwamba kama wakubwa wengine wangemchukua basi ina maana viwango vyao vilikuwa vya chini.

Kiaina huu ulikuwa udhalilishaji. Na nadhani katika mtego huu Simba na Azam waliamua kutomchukua. Akaenda zake Singida Big Stars katika kile kilichoonekana kuwa Yanga walikuwa sahihi. Dirisha la Januari Chama alirudi zake Simba kupitia mlango wa nyuma.

Simba waliamua lolote na liwe. Hawakuwa na muda wa kuona aibu kumrudisha Chama. Bora uwe na Chama ambaye anacheza katika asilimia 40 ya ubora wake kuliko kucheza na Joshua Mutale au Leonel Ateba uwanjani.

JICH 04

Na kweli. Ingawa miguu inaonekana kumsaliti lakini Chama amewasukuma Simba mbele kuliko ambavyo Mutale angefanya. Kwa kushirikiana na Aniceth Oura na Libasse Gueye Simba ya sasa ina unafuu mkubwa kuliko ile ya akina Mutale. Hii inau bora.

Kuhusu suala la kutopokelewa vizuri na baadhi ya wachezaji wa Yanga hilo ni jambo la kawaida katika mpira. Sidhani kama linahitaji mjadala sana. Ndivyo walivyo walimwengu. Wengine watakupokea vizuri wengine hawatakupokea vizuri. Hata makazini kwetu kuna maisha ya namna hii.

Vyovyote ilivyo Chama hajaongea kitu kipya sana kuhusu dili lake la kwenda Yanga. Ni kweli kwamba ana mapenzi makubwa na Simba na anajutia kwenda Yanga. Hata hivyo ni yeye pekee ambaye alipaswa kuhakikisha jambo hili halitokei.

Nadhani kwa sasa atakuwa amejifunza kuipenda zaidi na kuiheshimu Simba. Nadhani atapambana zaidi kuliko awali. Tatizo pekee ambalo nimeanza kuliona ni ukweli kwamba umri unamtupa mkono.

Chama amekuwa akitolewa nje katika mechi muhimu za Simba wakati ikisaka ushindi. Uliwahi kufikiria kwamba siku moja Chama atatolewa uwanjani wakati Simba wakisaka ushindi? Sidhani kama umewahi kufikiria hivi.

Vipi kuhusu mkataba mpya mwishoni mwa msimu huu? Itategemea na namna ambavyo ataendelea kuonyesha umuhimu wake katika mechi kubwa na ndogo. Itategemea pia na utundu wa mabosi wa Simba kusaka wachezaji mahiri wa nafasi yake ambao watamuondolea umuhimu klabuni. Hali ikiwa hii hii basi wanaweza kudumu naye hata misimu mitatu mbele.