Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KMKM yawapiga mkwara kina Mayele CAF

Muktasari:

  • Amesema, licha ya KMKM kupoteza mechi mbili za msimu huu ambazo ni Ngao ya Jamii dhidi ya KVZ na Ligi Kuu Zanzibar mbele ya Kipanga, hilo wamelisharekebisha, hivyo hawataingia uwanjani kinyonge zaidi ya kuhitaji ushindi nyumbani bila ya kujali ubora na ukubwa wa mpinzani wanayekutana naye.

ZANZIBAR; KOCHA MKUU wa KMKM, Ali Vuai Sheni, amesema timu hiyo imejiandaa kuondoka na ushindi dhidi ya Al Ahli Tripoli anayochezea Fiston Mayele katika mechi ya Kombe la Shirikisho la Afrika hatua ya kwanza.


Amesema, licha ya KMKM kupoteza mechi mbili za msimu huu ambazo ni Ngao ya Jamii dhidi ya KVZ na Ligi Kuu Zanzibar mbele ya Kipanga, hilo wamelisharekebisha, hivyo hawataingia uwanjani kinyonge zaidi ya kuhitaji ushindi nyumbani bila ya kujali ubora na ukubwa wa mpinzani wanayekutana naye.

Kesho Jumamosi, KMKM itaikaribisha Al Ahli Tripoli kutoka Libya katika mechi ya mkondo wa kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja kuanzia saa 10:00 jioni.

Akizungumzia maandalizi kuelekea mchezo huo, Vuai amesema: "Tumejiandaa kufanya hiyo kazi ya kuiwakilisha Zanzibar kimataifa, KMKM tumejiandaa kuondoka na pointi tatu nyumbani na si vinginevyo."

Amesema, kwa kawaida timu hujifunza kupitia makosa na kuyafanyiakazi kwenye uwanja wa mazoezi, hivyo KMKM haikujiandaa kushiriki bali kushindana.

"Tunakubali kuwa tunacheza na timu kubwa yenye wachezaji bora lakini na sisi ni washindi ambao tunaiwakilisha Zanzibar, hivyo tumefanya usajili wenye uwezo wa kushindana katika mashindano hayo," amesema.

Kocha huyo, amesisitiza kuwa, katika mashindano hayo KMKM haiendi kutembea badala yake wanaingia kushindana na dakika 90 zitatoa uamuzi kwa namna walivyojiandaa.

Naye, Naohdha Msaidizi wa KMKM, Martin Charles, amesema wanaamini mechi hiyo itakuwa ngumu upande wao kwani wanaenda kukutana na timu bora lakini hilo haliwakatishi tamaa.

Amebainisha kwamba, mshambuliaji wa Al Ahli Tripoli, Fiston Mayele hawezi kuwa tishio kwao kwa sababu uwanjani hachezi peke yake, hivyo wamejiandaa kuwazuia wapinzani wao na kuondoka na alama tatu nyumbani.

"Haiwezekani Fiston afanya kila kitu mwenyewe, lazima atakuwa na wengine anaowategemea na KMKM tunahakikisha tunamdhibiti na tunafanya vizuri dhidi yao," amesema Charles.

Mayele ni miongoni mwa maingizo mapya ndani ya Al Ahli Tripoli msimu huu, wengine baadhi ni Mohamed Amine Tougai, Mohammed Khalil, Mostafa Shakshak, Mamadou Lamine Camara, Abouqassim Rajab, Maruwan Al-Hbeishi, Hamdou El Houni na Omar El-Harek.

Naye, Katibu wa Habari na Masoko wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Mohamed Kabwanga, amesema mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni, mageti yatafunguliwa mapema kuanzia saa 8:00 mchana, huku viingilio vikiwa Sh2,000 mzunguko na Sh5,000 wings.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kila bao litakalofungwa na KMKM pamoja na KVZ katika mashindano ya CAF litanunuliwa kwa Sh1 milioni, huku kila ushindi utakuwa na thamani ya Sh5 milioni.

Katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2025-2026, KMKM iliishia hatua ya pili baada ya kuondolewa na Azam kwa jumla ya mabao 9-0. Mechi ya kwanza iliyochezwa Zanzibar, KMKM ilifungwa 2-0, kisha marudiano kwenye Uwanja wa Azam Comlex jijini Dar es Salaam, wenyeji Azam wakashinda 7-0 na kufuzu makundi kwa mara ya kwanza.

Kabla ya hapo, hatua ya kwanza KMKM ilifanya vizuri ikiitoa AS Port ya Djibout kwa jumla ya mabao 4-2, mechi ambazo zote mbili zilichezwa New Amaan Complex, Zanzibar. Zote KMKM ilishinda kwa mabao 2-1.