KMKM matumaini kibao Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Mkuu huyo amesema kutokana na usajili ambao timu hiyo umeifanya ni dhahiri kwamba imedhamiria kufanya makubwa Ligi Kuu Zanzibar na hata katika Kombe la Shirikisho Afrika inapokwenda kushiriki.
LICHA ya KMKM kushindwa kutetea taji lake la Ngao ya Jamii Zanzibar 2026, lakini mkuu wa kikosi hicho, Comdore Azan Hasaan Msingiri, amesema bado anaimani na timu hiyo kufanya vizuri katika Ligi Kuu Zanzibar 2026-2027.
Mkuu huyo amesema kutokana na usajili ambao timu hiyo umeifanya ni dhahiri kwamba imedhamiria kufanya makubwa Ligi Kuu Zanzibar na hata katika Kombe la Shirikisho Afrika inapokwenda kushiriki.
Amesema timu hiyo imepanga kufanya marekebisho dirisha dogo la usajili kwa lengo la kuimarisha kikosi katika mbio za ubingwa baada ya kugundua mapema wanahitaji maboresho baada ya kupoteza mechi ya Ngao ya Jamii kwa kufungwa penalti 8-7 na KVZ baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
“Katika mchezo huu wa Ngao ya Jamii, timu imeonesha uwezo mkubwa na bado ina mikakati ya kufanya vizuri, tutahakakisha mipango ya utendaji kazi inakaa vizuri na dirisha dogo tutafanya marekebisho ya kikosi,” amesema Msingiri.
Mkuu huyo amesema, KMKM msimu wa 2026-2027 wa Ligi Kuu Zanzibar haina utani na wanapanga kurudisha heshima iliyokuwanayo awali kwa kulirejesha kombe hilo. Amesema kama walivyoimwaga jasho KVZ kwenye mechi hiyo ya ufunguzi wa msimu, ndivyo ambavyo wanahakikisha kikosi hicho kinafanya vizuri Ligi Kuu Zanzibar.
KMKM imeshindwa kutetea Ngao ya Jamii baada ya kupoteza mechi dhidi ya KVZ iliyochezwa Agosti 23, 2026 kwenye uwanja wa Mao Zedong, Unguja ambapo KVZ imeandika historia ya kutwaa ubingwa huo mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa kikosi hicho miaka 22 iliyopita.
Mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa, Jusper Babalika aliitanguliza KMKM kufunga bao dakika ya 14 lililodumu hadi mapumziko, kisha dakika ya 52 Matheo Antony akaongeza la pili kwa mkwaju wa penalti.
KVZ ilisawazisha mabao hayo kupitia Mudrik Gonda dakika ya 65 na Akram Muhina ‘Haland’ dakika ya 89.
Katika mechi hiyo, Matheo Antony aliibuka mchezaji bora na Suleiman Kidawa mchezaji mwenye nidhamu na muungwana.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma, amesema amefurahishwa namna timu hizo zilivyokuwa na ushindani hadi kufikia kupatikana kwa bingwa.